HATARI YA VITA VYA KIMADHEHEBU KATIKA NCHI ZA GHUBA

Wapiganaji wa ISIL wakiwa kwenye mazoezi. Picha

Wapiganaji wa ISIL wakiwa kwenye mazoezi. Picha ya Maktaba 
By Othman Miraji, Mwandishi
Hatua ya karibuni ya kunyongwa kwa pamoja watu 47 waliokuwa wamepewa hukumu ya kifo nchini Saudi Arabia imezusha malalamiko duniani.
Kisiasa hatua hiyo imesababisha hasira kwa vile miongoni mwa watu walionyongwa alikuwamo shehe wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia ambaye pia ni mpinzani wa Mfalme wa nchi hiyo, Ayatollah Nimr al-Baqir al-Nimr, aliyekuwa na umri wa miaka 56.
Yeye aliwahi kuongoza maandamano ya Washia walio wachache katika Saudi Arabia wakati ilipozuka mwaka 2011 ile michafuko iliyopewa jina la Mapinduzi ya Machipuko katika nchi kadhaa za Kiarabu.
Al-Nimr- tafsiri yake kwa Lugha ya Kiarabu ni Chui. Ni mtu ambaye alikuwa akipinga matumizi ya nguvu katika maandamano. Alihiyari kupaza sauti kali dhidi ya watawala, akiamini kwamba silaha ya maneno ina nguvu zaidi kuliko risasi.
Kunyongwa kwa Al-Nimr kumezidisha mivutano ya kimadhehebu ndani ya Saudi Arabia na pia mzozo baina ya nchi hiyo na Iran.
Maandamano yalifanywa katika mji mkuu wa Iran, Tehran, kupinga kuuawa kwa Ayatollah wakati jengo la Ubalozi wa Saudi Arabia lilipovamiwa na kuchomwa moto.
Saudi Arabia yajibu
Saudi Arabia ilivunja uhusiano wa kibalozi na Iran, ikawapa saa 24 wanadiplomasia wa Kiirani waondoke nchini humo na pia kuwarejesha wanadiplomasia wake waliokuwako Riyadh. Marekani imewataka viongozi wa nchi hizo mbili za Kiislamu wapunguze munkari na warejee kufanya mazungumzo baina yao.
Kwa hakika, Iran, iliyo hasimu wa Saudi Arabia katika eneo la Ghuba, inajihisi ni mlinzi wa Washia duniani. Hadi asilimia 15 ya wakazi wa Saudi Arabia wanajitambulisha kuwa ni Waislamu wa madhehebu ya Shia. Wengi wao wanaishi katika majimbo ya Mashariki ya Al-Qatif na Al-Ahsa ambayo yana utajiri wa mafuta.
Katika nchi jirani ya Bahrein, ambako kumekuwa na maandamano ya kupinga utawala wa kifalme wa madhehebu ya Kiislamu ya Sunni, wakazi wa madhehebu ya Shia ndiyo wengi.
Kwa mujibu wa Shirika la kutetea haki za binadamu duniani la Human Rights Watch, Washia katika Saudi Arabia wanabaguliwa.
Kwa mujibu wa wanaharakati watu wa madhehebu hayo huwekewa vikwazo katika shughuli zao za kidini, huumbuliwa na kuitwa Makafiri na mara kadhaa hunyimwa nafasi za kukamata nyadhifa za kiserikali.
Hayo ni baadhi ya mambo ambayo alikuwa akiyalalamikia Al-Nimr. Shirika hilo la Human Rights Watch limesema kuuawa Al-Nimr si haki na kutazidisha kuwapo mgawanyiko na mivutano katika nchi hiyo. Lilitaka kukomeshwe mtindo wa kuwabagua Washia. Rais Ali Khamenei wa Iran aliwaambia Wasaudia kwamba wangojee hasira za Mwenyezi Mungu kwa kumuua Al-Nimr.
Lakini Saudi Arabia imejitetea. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa nchi hiyo, Al-Jubair, alisema kuchomwa moto ubalozi wa nchi yake mjini Tehran ni kwenda kinyume na maafikiano ya kimataifa na kwamba siasa ya uadui ya Iran ina madhumuni ya kuhatarisha usalama katika eneo la Ghuba.
Alidai kwamba Iran inapeleka kwa njia za magendo silaha na milipuko na kuwapa mafunzo watu ili waende Saudi Arabia na nchi nyingine katika eneo la Ghuba kufanya ugaidi. Alisema nchi yake haitairuhusu Iran ihatarishe usalama wake.
Al-Nimr alikamatwa mara kadhaa
Ayatollah Al-Nimr aliwahi kukamatwa mara kadhaa hapo kabla, mwishowe ikiwa mwaka 2012. Yeye aliamini kwamba bila ya kuwekewa ngumu utawala wa Saudi Arabia hautaleta mabadiliko nchini humo.
Idara ya Usalama ya nchi hiyo nayo ilimshuku Al-Nimr kuwa na maingiliano na Iran. Jambo hilo si la ajabu kwa vile kwa miaka mingi alikuwa masomoni katika nchi hiyo. Mwaka 2009 ilipotokea machafuko na mapambano katika mji mtakatifu wa Madinah, magharibu ya Saudi Arabia, baina ya mahujaji wa Kishia na majeshi ya usalama inasemekane al-Nimr alitoa mawaidha akitaka majimbo ya mashariki ya Saudi Arabia wanakoishi Washia wengi ijitenge.
Lakini wafuasi wake wamekanusha kwamba aliwahi kusema hayo. Alipokamatwa mwaka 2012 alijeruhiwa kwa kupigwa risasi nne mguuni. Baadaye polisi ilisema Al-Nimr alikuwa na silaha, jambo ambalo pia limethibitishwa na familia yake.
Inadaiwa hakupatiwa matibabu ya kufaa alipokuwa kizuizini. Baada ya kukamatwa kwake kulitokea machafuko yaliyodumu siku kadhaa katika mji alikozaliwa wa al-Qatif ambako watu watatu walikufa. Baadaye alipewa hukumu ya kifo kwa shtaka la kushirikiana kusaliti nchi ya kigeni na kutomtii mkuu wa nchi.
Kuuawa Al-Nimr kumewashangaza watu wengi kwa vile alikuwa mtu aliyeamini kuendesha mapambano kwa njia ya amani.
Serikali ya Saudi Arabia mara hii imekwenda mbali zaidi. Ni kama imemwaga mafuta katika moto. Imewafanyia uchokozi Washia wanaoishi katika majimbo yenye utajiri wa mafuta na ambako hadi sasa hakuna kikundi chochote miongoni mwao kinachoendesha harakati za kutumia nguvu.
Wachunguzi wanaiona hatua hiyo ya watawala wa Saudi Arabia ni jibu kutokana na kitisho wanachokabiliana nacho kutoka kwa wapiganaji wa ile inayoitwa Dola ya Kiislamu ISIL. Wapiganaji hao wanaendesha harakati zao katika maeneo ya Iraq, karibu na mpaka wa Saudi Arabia. Pia ndani kwenyewe Saudi Arabia kuna wafuasi na wapenzi wa ISIL. Mwaka jana waliishambulia misikiti kadhaa ya Washia.
Wachunguzi wa mambo wanahoji kwamba kwa vile Al-Nimr na Washia wengine watatu ni miongoni mwa hao watu walionyongwa, hiyo ni kuonyesha kwa Wasunni kwamba Serikali haibagui baina ya makundi ya kidini au kimadhehebu linapokuja suala la matumizi ya nguvu kwa madhumuni ya kisiasa.
Mamia waandamana
Mamia ya watu waliandamana katika mji wa Karbala, Iraq, wakipinga kitendo hicho, licha ya mamia kufanya vivyohivyo huko Masahriki ya Saudi Arabia.
Kulitolewa vitisho vya kuchukuliwa hatua kali dhidi ya watawala wa Saudi Arabia na wale wa Bahrein. Wizara ya mambo ya kigeni ya Iran imetishia na kusema kwamba Saudi Arabia italipia gharama kubwa kwa kumuuwa Al-Nimr.
Kwa mujibu wa Shirika la Amnesty International linalotetea haki za binadamu duniani, hadi Novemba mwaka jana si chini ya watu 151 walinyongwa Saudi Arabia. Mwaka 2014 idadi ilikuwa 90. Hukumu ya kifo katika nchi hiyo huwa kukatwa kichwa au kupigwa risasi.
Ushindani na uhasama baina ya Iran na Saudi Arabia unadhihirika waziwazi hivi sasa. Iran inamuunga mkono Rais Bashar al-Assad katika vita vya kienyeji vya Syria, wakati Wasaudi wako upande wa waasi wa Kisunni.
Huko Yemen Iran inawaunga mkono ndugu zao wa madhehebu ya Shia, Wahuthi, wakati Saudi Arabia inaiunga mkono Serikali iliopinduliwa ambayo viongozi wake ni wa madhehebu ya Sunni. Tutumai uhasama huu wa kimadhehebu hautapelekea kupigana vita kwa nchi hizo mbili kubwa katika Ghuba.     
Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment