Dar es salaam. Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Ben Usaje amesema kuwa watu waliosafirisha makontena tisa na kuyahifadhi sehemu isiyo rasmi wamekiuka taratibu.
Kauli ya Usaje imekuja kufuatia kukamatwa kwa makontena tisa yakiwa yamehifadhiwa eneo ambalo siyo bandari kavu na nyaraka za kutolea mzigo bandarini hazionyeshi kama yanatakiwa kuhifadhiwa eneo hilo.
Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa ndani ya makontena hayo kuna nguzo za chuma, mabati ya kuingizia mwanga kwa ajili ya ujenzi na wahusika kueleza kuwa wamefuata taratibu zote ikiwamo kulipa kodi na ushuru wa forodha
Hata hivyo, Usaje alisema bado wanaingia matatani kwa sheria za usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini.
Alisema ukaguzi wa kilichomo ndani unaendelea na ukimalizika atatoa taarifa kulingana na masuala yaliyokiukwa.
“Kupeleka mzigo nyumbani ni kosa, hivyo moja kwa moja wamekiuka taratibu, tutajiridhisha kulingana na taarifa nitakayopata, nitafahamu wamekiuka sheria gani na adhabu yao ni faini kiasi gani, hawana jinsi ya kukwepa kuwa wamekiuka kanuni na taratibu za usafirishaji ambazo ni kali kuliko za kodi,” alisema Usaje.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi, Richard Kayombo alisema kuwa baada ya kumalizika ukaguzi na kujiridhisha ndiyo watatoa ufafanuzi kuhusu nyaraka iwapo zilikuwa zimelipiwa.
Alisema mizigo hiyo ni ya msamaha wa kodi ambayo ni kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda katika Kituo cha Uwekezaji EPZ Bagamoyo, lakini watakuwa na uhakika baada ya kukaguliwa makontena yote kwa sababu siyo rahisi kutambua ndani ya kontena kwa kutazama vilivyopo mbele.
0 comments:
Post a Comment