Dar es Salaam. Operesheni ya bomoabomoa inayoendelea kwa waliojenga nyumba mabondeni jijini Dar es Salaam itawaacha zaidi ya watu 200,000 wakiwa hawana makazi.
Ubomoaji huo ulioanza katikati ya Desemba mwaka jana, umezikumba nyumba takriban 600 katika mitaa ya Hananasif na Suna, Manispaa ya Kinondoni.
Wakazi hao ni wale ambao Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeziwekea alama ya X nyumba zao ambazo ni zaidi ya 10,000 hadi kufikia juzi, kwa mujibu wa Ofisa Mazingira Mwandamizi wake, Arnold Kisiraga.
Hadi jana mchana, Kisaraga alisema walikuwa wakiweka alama ya X katika nyumba za mabondeni zilizopo eneo la Stakishari, Segerea na kwamba wataendelea hadi Pugu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Idadi hiyo imefikiwa kwa kuzingatia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ambayo inabainisha kuwa kila kaya jijini hapa inakadiriwa kuwa na wastani wa watu wanne chini kidogo ya wastani wa Tanzania Bara wa watu watano (4.7) kwa kaya.
Mkurugenzi wa Sensa za Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo alisema kwa sasa wana takwimu za kaya pekee ambazo sehemu kubwa ya watu wake wamepanga.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Suna, Salim Hamis alisema katika mtaa wake kuna nyumba zaidi ya 900 ambazo kila moja inaweza kuwa na kaya kati ya tano hadi saba.
“Wapangaji ni wengi katika nyumba hizi usione nyingi ni ndogo. Wengi wana hali ya chini ndiyo maana tumebanana hapahapa kwa kuwa hakuna namna tena,” alisema Hamis.
Kisiraga alisema makadirio ya awali ya nyumba 8,000 yalijikita kwa kuangalia zinazotambuliwa na Wizara ya Ardhi na manispaa lakini wamebaini “vijumba vidogo” vinavyoonekana kama vimeungana na nyumba kubwa za jirani kumbe vinajitegemea. Sehemu kubwa ya nyumba hizo zipo Kinondoni. Alisema kadri wanavyozidi kupita mabondeni kuweka alama ya X ndivyo idadi ya nyumba zilizojengwa maeneo hatarishi zinavyoongezeka.
“Hii inatokana na mito kuendelea kupanuka kutokana kingo zake kuharibiwa na wachimba mchanga na kufanya nyumba za jirani kuingia kwenye mita 60 zinazokatazwa kisheria. Kuna baadhi ya nyumba zilikuwa maeneo salama miaka 10 iliyopita lakini kwa sababu mto umesogea kwao basi watabomolewa kwa kuwa wapo maeneo hatarishi,” alisema Kisiraga.
Kuhusu hatua hiyo, mmoja wa wakazi walioathirika, George Mkondoa alisema: “Bado tupotupo tu hapa hatuna pa kwenda. Baadhi ya vitu nimejaribu kuvipeleka nyumbani Bagamoyo lakini vimebaki nusu. Hivyo ilinibidi nijenge kibanda kidogo kwa muda tuishi na familia yangu.”
Chiku Salim aliyekuwa na nyumba ya vyumba viwili aliyoibomoa mwenyewe, alisema hana pa kwenda kujenga licha ya kuokoa mabati na vifaa vingine katika nyumba yake.
Mmoja wa wapangaji, Steven Herman alisema: “Ubomoaji ulikuja ghafla na wengi unakuta walikuwa wamebakiza miezi mitatu au minne kodi zao ziishe hivyo kuhamishwa ghafla kumeleta mtihani wa kupata nyumba haraka ndiyo maana unakuta tunahaha hapa.” Alisema shida hizo zingeepukika iwapo wangekuwa na elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya ardhi na mipango miji.
Mkurugenzi wa kampuni ya maendeleo ya ardhi na makazi ya Space & Development, Renny Chiwa alisema:
“Ili kuwaokoa wananchi hao, ni lazima kuweka mazingira rafiki ya ukuaji wa sekta binafsi katika maendeleo na makazi. Kampuni zikipata mikopo ya nyumba kwa riba na masharti nafuu ushindani utakua na zitajenga maghorofa ambayo vyumba vyake vinaweza kupangishwa kati ya Sh30,000 hadi 100,000 kwa mwezi.”
Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Patience Mlowe alisema wananchi walifanya makosa kuvamia maeneo hayo kinyume na sheria na Serikali ilikosea kwa kuwaacha waendeleze makazi kwa kuwasogezea huduma za Serikali za Mitaa, maji na umeme hivyo kuwapa uhakika wa maisha ya kudumu na kushauri utengenezwe mpango maalumu wa kuwasaidia.
“Hakuna Mtanzania anayeunga mkono wananchi hawa waendelee kukaa maeneo hatarishi ya mabondeni. Ila kinachoendelea sasa kinawaathiri kisaikolojia, kinawaumiza. Wale ni Watanzania, Serikali lazima iwasaidie tu. Watafutiwe makazi mbadala kwa muda wanapojipanga kusimama tena,” alisema Mlowe.
Alisema ubomoaji huo, unaowaacha wananchi hao kama wakimbizi katika nchi yao, unavunja haki za binadamu na unalitia doa Taifa kimataifa.
“Hatujui mpaka sasa mpango wa Serikali juu ya watoto wadogo waliobaki bila makazi na ambao wanasubiri kwenda shule baada kuanza kufunguliwa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment