MFAHAMU ZITTO ZUBER KABWE KWA UNDANI

MFAHAMU ZITTO ZUBER KABWE KWA UNDANI
__________________________________________________________
ZITTO Zuberi Kabwe ni mwanasiasa mdogo kiumri lakini mwenye mafanikio na changamoto nyingi kiuongozi na kisiasa kuliko umri wake. Katika makala haya tunajadili wasifu wa mwanasiasa huyu katika maeneo mbalimbali yanayohusu sifa muhimu za Rais ajaye.
Zitto alizaliwa tarehe 24 Septemba 1976 katika Kijiji cha Mwandiga, Wilaya ya Kigoma. Alisoma katika Shule ya Msingi Kigoma kutoka mwaka 1984 hadi mwaka 1990. Alisoma katika Shule ya Sekondari Kigoma (1991-1994) na kumalizia katika Shule ya Sekondari Kibohehe (Moshi) kati ya mwaka 1994 na 1995, akiwa amepata daraja la kwanza (Division 1:8).
Alisoma katika Shule ya Juu ya Sekondari Galanos (Tanga) mwaka 1996 na kumalizia katika Shule ya Sekondari Tosamaganga (Iringa) mwaka 1998, akiwa amepata daraja la pili huku akiibuka mwanafunzi bora katika somo la uchumi katika Mkoa wa Iringa.
Zitto ana shahada ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyoisomea kati ya mwaka 1999 na 2003, akiwa amepata alama 3.5 (second upper class). Zitto ana Diploma ya Juu katika Masoko ya Kimataifa kutoka Chuo cha Inwent-IHK kilichopo mjini Bonn nchini Ujerumani aliyehitimu mwaka 2004, na ana shahada ya umahiri katika sheria na biashara kutoka Chuo cha Sheria cha Bucerius nchini Ujerumani aliyohitimu mwaka 2010.
Mambo mawili yanajitokeza kuhusu elimu ya Zitto
Mosi, amesoma vizuri; hii ni sifa muhimu kwa kiongozi wa kisiasa katika nyakati za sasa kwa sababu elimu ni msingi wa fikra na falsafa unaohitajika kwa kiongozi kuweza kutoa dira na ushawishi.
Aidha, tafiti nyingi zinaonyesha kwamba elimu ni sifa ya kwanza ya kiongozi miongoni mwa wapiga kura walio wengi nchini Tanzania.
Pili, ukichunguza miaka aliyosoma Zitto utaona kwamba amesoma miaka mingi zaidi kwa elimu ya sekondari na Chuo Kikuu kuliko ilivyo kawaida.
Hii ni kwa sababu alipokuwa akisoma Shule ya Sekondari Kigoma alifukuzwa shule kwa kudaiwa kuwa alianzisha, kuendesha na kufanikisha mgomo yeye akiwa Kiranja Mkuu. Ndipo akalazimika kuhamia Shule ya Sekondari Kibohehe mkoani Kilimanjaro.
Aidha alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zitto alilazimika kurudia mwaka baada ya kusimamishwa masomo kutokana na kuhusishwa na mgomo wa kupinga sera ya uchangiaji wa gharama za elimu ya juu.
Alikuwa ametuhumiwa kuwa alikuwa miongoni mwa viongozi waliochochea mgomo huo yeye akiwa Mwenyekiti wa wanafunzi waliokuwa wanakaa Hosteli ya Kijitonyama.
Hii maana yake ni kwamba ‘ukorofi’ wa Zitto tunaouona leo ulianza siku nyingi.
Zitto amefanya kazi katika maeneo kadhaa kabla ya kuwa mbunge. Alipata kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Wanafunzi nchini (TSNP) kati ya mwaka 2001 na 2003.
Na kabla hajagombea ubunge na kushinda, Zitto alipata kuajiriwa na Shirika la Ujerumani (FES) kama Meneja wa Miradi kati ya mwaka 2004 na 2005.
Kiuongozi, Zitto alikuwa Kiranja Mkuu wakati akisoma Shule ya Sekondari Kigoma na baadaye kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) kati ya mwaka 2001 na 2003.
Ndani ya CHADEMA, Zitto alishika nafasi kadhaa za uongozi kabla ‘hajakorofishana’ na viongozi wenzake. Kwanza, alikuwa Mkurugenzi wa Mambo ya Nje mwaka 2004 na wakati huo huo akiwa pia Mkurugenzi wa Uchaguzi na kampeni wa chama hicho.
Mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2005, Zitto alichaguliwa kuwa Katibu wa wabunge wa CHADEMA. Mwaka 2007 alichaguliwa na Baraza Kuu la CHADEMA kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka jana baada ya kuondolewa na Kamati Kuu ya chama hicho.
Ndani ya Bunge, Zitto alipata kuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC) na baadaye kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Ni katika kipindi cha uenyekiti wa Zitto, ndipo ambapo kamati hizi zilijulikana sana kwa jamii.
Kihaiba, Zitto ana sifa mbili muhimu ambazo ni taswira chanya ya uongozi lakini wakati huo huo ikiwa ni taswira tata ya kiuongozi katika mazingira ya kitanzania.
Sifa ya kwanza ni tamaa na ujasiri wa kupenda kufanya makubwa ambayo hugeuka kuwa kero kwa baadhi ya viongozi wenzake anaofanya nao kazi.
Kwa mfano, akiwa anamaliza muda wake kama Katibu Mkuu wa DARUSO ‘alilazimisha’ hesabu za taasisi hiyo zikaguliwe na wakaguzi wa hesabu (auditors) kabla hawajakabidhi ripoti kwa uongozi mpya.
Hii haikuwa kawaida ya DARUSO na baadhi ya viongozi wenzake hawakulipenda jambo hili na wakamnunia.
Zitto amekuwa kinara wa kuibua ‘madudu’ mengi serikalini kuanzia kashfa ya Buzwagi, mabilioni ya Uswisi na sasa sakata la kashfa ya akaunti ya Escrow.
Pengine, taswira ya Zitto kuhusu tamaa na ujasiri wa kupenda kufanya mambo makubwa ni kitendo cha kamati anayoiongoza ya PAC kuwasweka ndani viongozi wa juu wa TPDC kwa kushindwa kutekeleza amri ya kamati hiyo.
Bila kuingia ndani ya sakata hili, ni wazi kwamba hili ni jambo ambalo lilikuwa halijawahi kutokea huko nyuma na linaweza likawa limefungua ukurasa mpya katika mahusiano kati ya Kamati za Bunge na uongozi wa taasisi za umma.
Sifa ya pili kihaiba kuhusu Zitto ni uvumilivu. Katika maisha yake ya kisiasa, Zitto amekumbana na misukosuko mingi hasa kuhusu kashfa mbalimbali zinazomlenga.
Tangu azozane na viongozi wenzake ndani ya CHADEMA kufuatia uamuzi wake wa kugombea uenyekiti mwaka 2009, Zitto amekuwa akirushiwa kashfa mbalimbali zenye lengo la kuchafua taswira yake kisiasa katika jamii.
Pamoja na kwamba hakuna hata kashfa moja ambayo imepata kuthibitishwa kimantiki na kisheria, kashfa hizo zimefanikiwa kutikisa taswira yake kiuadilifu.
Kifamilia, Zitto Kabwe hajaoa lakini ana mtoto mmoja wa kiume maarufu kwa jina la Chachage.
Hili ni jina alilompa mtoto wake kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa mhadhiri maarufu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, marehemu Profesa Chachage Seithy Chachage.
Kikazi, Zitto ana sifa tatu zinazomtenga kwa mbali na wanasiasa wengi hapa Tanzania. Mosi, Zitto anaamini kikamilifu katika itikadi, falsafa na sera kama msingi wa uongozi wa kisiasa.
Katika kipindi ambacho ujamaa umepoteza mashiko katika Bara la Afrika, yeye anajipambanua waziwazi kwamba ni mjamaa akiamini katika falsafa ya Unyerere.
Zitto anaamini kwamba kijiji ndiyo kitovu cha maendeleo ya Mtanzania na ni muhimu kuwekeza katika kilimo. Ndiyo mwanasiasa pekee nchini na pengine katika bara la Afrika aliyeweza kuisimamia kwa vitendo dhana ya hifadhi ya jamii kwa mwananchi wa kawaida hadi katika ngazi ya kijiji.
Ni kwa sababu hii, amekuwa mwanasiasa wa kwanza barani Afrika kushinda tuzo ya hifadhi ya jamii. Zitto pia anaamini katika demokrasia rasilimali kama msingi wa kuwapa wananchi fursa ya kumiliki na kufaidika na rasilimali za taifa.
Pili, Zitto anajipambanua kifikra. Hili linajitokeza katika ukweli kwamba Zitto ni miongoni mwa wananasiasa wachache hapa nchini wanaosoma sana. Mimi na yeye kila mwisho wa mwaka huwa tunapeana hesabu kuhusu idadi ya vitabu ambavyo kila moja wetu amevisoma kwa mwaka huo.
Aidha, Zitto ni mwandishi mzuri akiwa ni miongoni mwa wanasiasa wachache kabisa hapa nchini wenye uwezo na utayari wa kuandika makala. Kwa sababu hii sio kazi ngumu kujua anachofikiri na kukiamini Zitto kwani fikra zake zipo wazi kupitia maandishi yake.
Sifa ya tatu kikazi inayomtenga na wanasiasa wenzake wa upinzani hapa nchini ni mtandao mpana alionao ndani na nje ya nchi.
Kwa hapa nchini, Zitto ni mwanasiasa pekee wa upinzani aliyeonyesha uwezo wa kufanya kazi na kushirikiana na wanasiasa wa vyama vingine bila kujali tofauti zao za kisiasa.
Zitto ana uhusiano mzuri na viongozi mbalimbali nchini, wakiwemo viongozi wastaafu wanaoheshimika nchini.
Zitto ana mahusiano mema ya kikazi na viongozi wa vyombo vya dola ndani ya Jeshi la Wananchi, Polisi na Usalama. Hii ni sifa muhimu kwa kiongozi anayejiandaa kuwa mkuu wa nchi na dola.
Aidha, Zitto ana mahusiano mema ya kikazi na viongozi mbalimbali katika bara la Afrika, Amerika, Ulaya na Asia, pamoja na taasisi za kimataifa.
Hii nayo ni sifa muhimu kwa kiongozi anayejiandaa kushika uongozi wa juu wa nchi kwa sababu mafanikio ya kiongozi wa juu hutokana kwa kiasi kikubwa na mahusiano yake na Jumuiya ya Kimataifa.
Mafanikio ya Zitto Kabwe ndiyo pia udhaifu wake, hasa katika mazingira ya siasa za Tanzania. Kikazi, Zitto anaponzwa na tabia yake ya kutokuendana na utamaduni wa kimaisha na kisiasa wa Tanzania.
Kwa mfano, katika jamii yetu watu wanaofanya kazi kwa bidii sana hutazamwa kwa jicho lisilo chanya sana. Tangu tukiwa shuleni, mwanafunzi anayesoma sana hupachikwa majina ya ajabu ajabu kama vile ‘mnoko’, ametumwa na kijiji, ‘msongo’, n.k.
Tukiwa kazini, watu wanaofanya kazi sana kwa kuzingatia taratibu si miongoni mwa watu wanaopendwa.
Watu wa namna hii huonekana kama wanajipendekeza na ‘kujifanya wajuaji’ na hivyo hupachikwa majina mbalimbali na hata kupakaziwa.
Utamaduni huu pia upo katika siasa na kwa kiasi umemponza sana Zitto kwani anaonekana kama ni mwanasiasa mwenye kimbelembele kwa tabia yake ya ‘kung’ang’ania’ hoja mbalimbali zenye maslahi mapana kwa jamii na nchi.
Pili, ukaribu wa Zitto na viongozi wa serikali umefifisha taswira yake kisiasa kama mpinzani.
Tangu mfumo wa vyama vingi uanze katika nchi yetu viongozi wa upinzani wamejitahidi kujenga taswira kwamba wapinzani ni wakombozi na CCM ni wakoloni weusi.
Kwa hiyo siasa za upinzani ni siasa za harakati mithili ya wapigania uhuru enzi za ukoloni.
Kwa sababu ya taswira hii, kiongozi yeyote wa upinzani anayekuwa karibu na viongozi wa CCM na serikali kwa uwazi huonekana kwamba ni msaliti wa harakati za ukombozi.
Kwa utamaduni wetu wa kisiasa upinzani si ushindani wa hoja kati ya chama cha upinzani dhidi ya CCM, bali ni harakati za kumtoa ‘mkoloni’ mweusi kwa kile kinachoelezwa kwamba ni ukombozi wa pili.
Eneo la tatu la udhaifu wa Zitto katika maziingira ya siasa za upinzani Tanzania lipo katika aina ya siasa anazofanya.
Wakati yeye huamini kwamba kazi ya upinzani ni kujenga hoja mbadala, viongozi wenzake wa upinzani wanaamini kwamba kazi ya msingi ya upinzani ni kushambulia haiba na matendo ya viongozi wa chama tawala.
Kwa sababu ya tofauti hizi za kimtazamo, Zitto amejikuta yupo mbali kabisa na viongozi wenzake wa upinzani na hivyo kujikuta kama mtoto yatima akilelewa na walezi wasio mpenda.
Nilipomuuliza yeye anaamini ni kwa nini aligombana na viongozi wenzake ndani ya CHADEMA, Zitto alikuwa wazi kabisa kwamba ilikuwa ni mapema mno kwa yeye kugombea uenyekiti wa CHADEMA mwaka 2009.
Kwamba tangu agombee uenyekiti mwaka 2009, wenzake walimuona ni msaliti na mahusiano yao hayajawahi kurudi katika hali ya kawaida.
Ni wazi kuwa Zitto ameshindwa kuenea katika utamaduni wetu wa kisiasa, ambao hauruhusu ushindani wa kisiasa hasa ndani ya vyama vya upinzani.
Kiongozi wa upinzani huongoza hadi pale atakapochoka au kuchokwa sana na hata pengine atakapoitwa na mola.
Kwa hiyo Zitto alikuwa ‘mjinga’ kwa kuamini kwamba angeweza kupata uenyekiti wa CHADEMA kwa kujaza fomu na hatimaye kupigiwa kura.
Nami lazima nikiri kwamba nilikuwa ‘mjinga’ kwa kumshawishi na hatimaye kumtia moyo kugombea nikiamini kwamba ushindani wa kisiasa ndani na baina ya vyama ndiyo msingi na kiashiria cha kukua kwa demokrasia katika nchi.
SOURCE:RAIA MWEMA
Share on Google Plus

About Mind 2022

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment