Nakubaliana na Rais John Magufuli kuwa Watanzania wanahitaji maarifa.
Nakubaliana naye kuwa watoto wa maskini wanahitaji elimu, tena elimu yenye maarifa siyo kurundikana darasani tu pasipo maarifa wala kujifunza.
Nakubaliana naye kuwa ni lazima tuelimishe watu wetu ili wawe na nguvu za kuzalisha na kuchangamkia fursa za kiuchumi ndani na nje ya nchi yetu.
Nakubaliana naye kuwa ili uchumi wa nchi uweze kuendelea, tunahitaji kuwa na wananchi wengi wenye ujuzi, maarifa, ubunifu utaalamu na wenye uwezo mkubwa kufikiri, kujituma na kufanyakazi kwa bidii.
Hatuna njia za mkato kufikia maendeleo. Maana iko wazi kuwa watu wanyonge duniani ni watu wasio na maarifa ya kutosha. Ndani ya utandawazi maarifa kidogo ni umaskini zaidi na maarifa mengi ni fursa zaidi za kipato. Hakuna jamii inayoweza kupata maendeleo kwa kubahatisha.
Hakuna nchi iliyowahi kuendelea kwa miujiza. Maendeleo ni sayansi ya kufikiri na kutenda ambayo inaratibiwa na ubongo wenye maarifa na ujuzi. Huo ndiyo ukweli!
Nilipoandika kuhusu athari hasi za elimu bure, nilipigiwa simu nyingi na kutumiwa ujumbe mfupi kuhusu hoja hii. Wengi wanasema mbona iliwezekana enzi za Mwalimu Nyerere bila kuwa na athari mbaya, iweje sasa ionekane kama mpango huu wa elimu bure utakuwa na madhara?
Nakubaliana na mawazo yao yenye ukweli na mantiki, ila tunahitaji kuchambua zaidi mifumo ya uendeshaji wa nchi na uchumi wa jamii kipindi cha Nyerere na sasa. Hapo ndipo tutajua ubaya wa huduma za bure. Ni vyema kudurusu misingi ya tofauti ya elimu bure ya Nyerere na elimu bure ya Dk Magufuli.
Enzi za Nyerere mfumo wa uendeshaji wa nchi na uchumi ulikuwa ni ujamaa. Serikali ilihodhi njia kuu za uzalishaji mali, na uchumi wa nchi ulimilikiwa na Serikali. Misingi ya ujamaa ni usawa, kujitegemea na haki kwa wote. Ndiyo maana enzi za ujamaa njia zote za uchumi viwanda, benki, shule na taasisi zote zilikuwa mali ya Serikali. Hata shule bora enzi hizo zilikuwa za Serikali. Hakuna mtu alikuwa anahangaika kusomesha watoto wake shule binafsi, japo zilikuwapo kama seminari, shule za dini na mashirika kadhaa, watu hawakuona haja ya kukimbizana huko. Walisomesha watoto wao shule za umma.
Kwa msingi wa usawa na haki, tuliona mtoto wa rais wa nchi akikaa dawati moja na mtoto wa msukuma mkokoteni. Mtoto wa Gavana wa Benki Kuu, alilima bustani shuleni wakiwa na mtoto wa mlinzi. Elimu ilitolewa kwa usawa kwa sababu mfumo wa ujamaa ulitaka hivyo, siyo matakwa ya Mwalimu Nyerere.
Ujamaa ulihimiza kazi. Watu wote walifanya kazi, tena kwa bidii kubwa. Kila mtu alikuwa na shamba. Hakukuwa na vijana wa kijiweni wanaovuta bangi na kulalamika bila kufanyakazi. Walimu walifundisha, wakulima walilima. Hata shule zetu zilizalisha chakula na ujuzi mbalimbali wa kujitegemea.
Shule hazikuwa na upungufu wa vifaa kwa sababu Serikali ilithamini elimu kwa usawa, ilitumie fedha kwenye elimu hasa, siyo matamasha ya elimu. Mafungu ya elimu yaligharamia elimu. Shule nyingi zilikuwa na vyanzo vya mapato kutokana sera ya ujamaa na kujitegemea. Sera na falsafa ya elimu ilikuwa wazi.
Tofauti kabisa na elimu bure ya Dk Magufuli. Kwa sasa, mfumo wa uendeshaji wa nchi siyo ujamaa ni ubepari. Sifa kuu za ubebari ni njia kuu za uchumi kumilikiwa na watu binafsi; uchumi wa nchi unakuwa huria, ushindani na kuwapo kwa soko huria kwenye kila kitu, ushindani wa kuchangamkia fursa na wenye nguvu kuwanyonya wanyonge.
Ndiyo mfumo wa maisha wa sasa. Matajiri wachache tu wameshika uchumi wa nchi. Angalia kila sekta kuanzia viwanda hadi benki, kampuni za simu vyote ni binafsi. Hata elimu bora sasa inatolewa na shule binafsi.
Ushindani hauna vya bure. Ukipewa bure fahamu kuwa umepewa makombo au bidhaa bandia. Ndiyo maana nasema elimu bure ndani ya utandawazi ni sumu ya maendeleo. Kwa sasa mfumo wa uendeshaji wa nchi unaruhusu ushindani na uhuru wa kuchagua wapi pa kupata huduma unayotaka, ndiyo maana hata viongozi wetu wameacha shule zao walizojenga wamepeleka watoto nje ya nchi au shule binafsi.
Wanahimiza watoto wa wanyonge wasome kwa Kiswahili ilihali watoto wao wanasoma kwa Kiingereza (lugha ya ajira na fursa) kuanzia chekechea. Wanatafuta elimu bora siyo unafuu wa gharama.
Nilisema wiki iliyopita kuwa shule zetu hazina pesa ndiyo maana walimu wanawaomba wazazi michango. Na kila taasisi inahitaji pesa ili iweze kujiendesha. Serikali iliandaa sera ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shule kupitia ruzuku kwa kila mwanafunzi. Kila mwaka, Serikali inapaswa kutoa Sh 10,000 kwa kila mwanafunzi wa elimu ya msingi, cha kushangaza fedha hizi hazifiki shuleni, na zikifika ni kwa kuchelewa au pungufu.
Kuna shule hazijapokea ruzuku kwa miaka miwili mafungu hayatumwi. Waulize walimu wakuu wana majibu. Tunahitaji fedha ziende shuleni siyo kufurahia bure. Iweje iwe vibaya wazazi kuchangia elimu ya watoto wakati mambo mengine wanafanya kwa fedha hiyohiyo?
Ni faida wazazi kuchangia harusi, misiba na kulewa pombe kila siku kuliko kuchangia karatasi za mitihani ya watoto wao? Ni rahisi kuchangia mbio za Mwenge wa Uhuru kila mwaka kuliko kuchangia vitabu vya mwanao?
Tusipokuwa makini, bure itatufikisha pabaya. Tukiruhusu fikra zetu zitawaliwe na bure hatutafikiri tena, hatutafuta majibu ya matatizo yetu. Tutabweteka. Maisha ni mapambano. Tunatakiwa kupambana na maisha usiku na mchana.
Wenzetu hawalali usiku na mchana wanapambana kutafuta mbinu mpya za kurahisisha maisha. Wanakwenda kila kona ya dunia, wanamfikia kila mtu na kutafiti kujua anaishi vipi na fursa ni zipi.
Wanakwenda hadi kwenye sayari ambazo hazina watu, wanataka kupata fursa za kiuchumi, kupata maarifa zaidi ya dunia ilivyo na fursa zake ili waitawale. Sasa kuna ugunduzi wa kila aina ya teknolojia ambayo inarahisisha maisha. Wanafikiri na kufanyakazi siyo kubweteka. Sisi tunashindwaje kugharamia elimu ili tuutawale ujinga?
Kwa mzazi makini anayetamani mtoto wake afanikiwe hawezi kushindwa kulipa ada ya Sh 20,000 wakati kila siku anaweka vocha ya simu, kila siku analewa, kila siku ananunua mafuta ya pikipiki. Huwezi kushindwa kulipa Sh 10,000 kama mchango wa mitihani, wakati una kuku wengi, ng’ombe, mbuzi na mazao ya biashara. Kama unanunua vocha kwa nini ushindwe kununua karatasi za mitihani ya mtoto wako?
Nitamshangaa mzazi mwenye ng’ombe 300 anayetamani watoto wake wasome bure shule ya kata yenye walimu wawili na ruzuku hakuna. Nitamsitikia mzazi anayelewa pombe kila siku na hataki kununua daftari la mtoto wake eti Rais Magufuli kasema elimu bure.
Nitamshanga kijana wa kijiweni anashinda kumlipia mtoto wake Sh2,000 za mtihani wakati anatumia Sh30,000 kununua bangi na dawa za kulevya akisubiri bure ya Magufuli. Nawahurumia wazazi wanaotamani bure huku vipaji vya watoto wao vikiuawa shuleni wakati wana uwezo wa kulipia elimu bora popote.
Siamini kama kuna familia inapata unga bure, kibiriti bure, sukari bure. Elimu ni zaidi ya sukari, zaidi vya vocha za simu. Ni uwekezaji wa kudumu kwa watoto wetu. Tuigharamie na kuitafuta kwa nguvu zote zote.
Tukiendelea kubweteka na vya bure, tutakuwa maskini wa kudumu. Kutamani elimu bure ndani ya utandawazi ni kutamani mauti ya kifikra na maendeleo.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya sera aliyejikita kwenye masuala ya kijamii hasa elimu. 0713-000027
0 comments:
Post a Comment