Dar es Salaam. Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe leo itafanya harambee chuoni hapo ya kumchangia mwanafunzi Bernadetha Msigwa kwa ajili ya matibabu ya macho ili aweze kuona tena.
Harambee hiyo itajumuisha wanafunzi, walimu pamoja na watu mbalimbali ambao wameamua kumsaidia binti huyo.
Mhadhiri wa Kitivo cha Utawala cha chuo hicho, Aloyce Gervas alisema harambee hiyo itafanyika kuanzia saa mbili asubuhi.
Alisema baada ya kubaini kuwa tatizo lake lina tiba ndipo walipoanza kampeni kupitia mitandao ya kijamii: “Tunashukuru kampeni ya Kipepeo inayoendeshwa na Clouds Media na wasamaria wengine wote kwa kupokea wito wetu wa kumchangia Bernadetha. Tunatoa shukrani zetu kwa Rais John Magufuli kwa kutoa mchango wake baada ya kuona kipindi cha Kipepeo katika kipindi cha ya 360 cha kituo hicho.
Akimzungumzia mwanafunzi huyo, Gervas alisema: “Kutokana na hali yake, huwa tunampatia mtihani wa kujieleza, hapo ndipo utajua ni mwanafunzi mwenye akili na ambaye ana malengo makubwa ya kufika mbali pamoja na nia kubwa ya kutaka kuona.”
Bernadetha (21) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa kozi Shahada ya Rasilimali Watu, kwa sasa anaendelea na vipimo katika Hospitali ya Muhimbili.
Alijiunga na Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 2011 baada ya kumaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilakala, Morogoro.
Akizungumza na Mwananchi, alisema alikuwa mzima wa afya kipindi hicho, alikuwa anaona na kufanya kila kitu mwenyewe.
“Mabadiliko yalianza mwanzoni mwa mwaka 2014 muhula wa mwisho baada ya kuanza kusumbuliwa na maumivu makali ya kichwa.”
Alisema alipata matibabu ya kichwa na macho katika hospitali mbalimbali na hatimaye katika hospitali maalumu ya macho, lakini haikusaidia.
“Macho yangu yalianza kupoteza nuru ya kuona kidogokidogo. Hata hivyo, mwishoni mwa mwezi wa tano, 2014 ilikuwa mara ya mwisho kwangu kuona.
“Naamini naweza kuona tena, ila hata kama sitaona, nitakushukuru kwa moyo na mchango mkubwa ninaoupata,” alisema.
Meneja wa kipindi cha 360 cha Clouds TV, Hudson Kamoga alisema jana kuwa mpaka sasa michango inaendelea vizuri na jumla yake itapatikana baada ya harambee ya leo.
Source: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment