Mimi ni muimbaji wa nyimbo za injili pia nimeshiriki kuweka mashairi ("Lyrics" "Maneno") kwenye baadhi ya nyimbo kadha wa kadha. Wakati fulani mashairi haya huwa yanaashiria uzoefu fulani wa kweli alioupitia mwandishi halisi wa wimbo Katika uandishi kuna waandishi walioshindwa kusimulia uzoefu mgumu walioupitia kwa sababu kila akitaka kuandika anapata kumbukumbu mbaya na anatoa machozi.
Sina sababu ya kuandika kisa cha mtu fulani, kwasababu fulani la hasha!! Ninachofahamu wapo watu wengi wamepitia nyakati nyingi za machozi na hakuna aliyeweza kuwafuta, walidumu kulia na kulia bila faraja wala msaada wowote, wengine walikata tamaa wakiamini hakuna tena mwanga wa matumaini katika safari yao ya maisha.
Wapo watu wakiona giza linaingia, usiku kwao unakuwa ni nyakati za machozi, usingizi umekuwa adimu katika macho yao kwa miaka mingi, vitanda vyao vimekuwa mito ya machozi, wamedumu kutiririsha machozi katika macho yao hadi mwanga wa jua unapoanza kutoka tena.
Chozi linaweza kuelezewa kwa namna nyingi sana, ila chozi la maumivu hakuna kitambaa kitakachotosha kulirudisha na kuwa Chozi la furaha. Wapo watu wengi wamelia machozi kwasababu wameonewa na wameendelea kulia ndani ya mioyo yao, na machozi yao yamedumu miaka mingi na kuendelea kuyafanya maisha yao kuwa ya huzuni.
Kuna wakati mtu au watu waliokusababishia utoe machozi, wao hufurahi kwasababu wanakuona una huzuni kila wakati, hawaguswi na uchungu na maumivu unayoyapitia bila kuwa na kosa lolote. Huwa najiuliza machozi ya namna hii nani atayafuta?
Kuna watu wengi wanalia kwasababu wameachwa katika umaskini, kuna wengine wanalia kwakuwa waliowapenda na kuwathamini katika maisha yao wamewaacha bila kosa lolote, wapo wengine wanalia kwa kuwa hana kazi na hajui kesho yake itakuwaje, wapo wanaolia kwasababu wametendewa vitendo vya kikatili. Kuna vilio vingi sana kila sekunde inayopita kuna mtu analia. Sijui chozi lako ni aina gani!!!
Wimbo huu niliuandika nikiwa ninatoa chozi, Kila chozi lililodondoka lilikuwa linaashiria uchugu mwingi, hatimaye nikakumbuka kila jambo gumu linalokupata usitumie nguvu zako kupambana nalo mwamshe Yesu yeye ni Bwana wa Dhoruba, hakuna tufani yoyote maishani inayoweza kumshinda mwamshe yuko kando anakungoja.
Maneno haya niliyaandika mwaka 2004 nikiwa natoka Morogoro nikiwa ndani ya Bus la Abood na nilipofika Dar es Salaam nikaifundisha Kwaya yangu. Ni maneno machache lakini ya thamani sana kwangu.
1. Wakati wa majira ya usiku baharini dhoruba ilivuma, tufani ilipokuwa kubwa walikumbuka kumwamsha Yesu.
Akasema tufani ikakoma na upepo ukatulia mara, maishani dhoruba zikivuma ni wakati wa kumwamsha Yesu.
2. Wakati wa majira ya usiku unasongwa nazo dhoruba kali, tufani inapokuwa kubwa ni wakati wa kumwamsha Yesu.
Atasema tufani itakoma na upepo utatulia mara, maishani dhoruba zikivuma ni wakati wa kumwamsha Yesu.
Kama vile wanafunzi walivyomwamsha Yesu, naye akakemea dhoruba na upepo vikakoma kukawa shwari, hata sasa hatashindwa kukemea dhoruba na pepo za maisha haya. Pray for me and I wil pray for
Imeandikwa na Ahadi Sagatti Mwalimu na mwimbaji wa siku nyingi wa kwaya mbalimbali za Waadventista wa Sabato. Fuatilia simulizi zake nyingi katika ukurasa wake wa facebook utaona picha hiyo hapo juu kwenye ukurasa wake halisi. Yeye anaonekana upande wa kushoto.
0 comments:
Post a Comment