Muonekano wa maji
yakiwa mtoni kabla ya kuanza kusafishwa kupitia hatua mbalimbali kwa matumizi.
(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
Na Eleuteri Mangi
Mamlaka ya Maji Safi na
Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea kuboresha na kuimarisha miundombinu
ya maji ili kuwanufaisha wakazi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kupata maji
kwa mahitaji yao ya kila siku.
Mioundombinu hiyo
inayoboreshwa ni pamoja na bomba la Ruvu Chini lenye urefu wa Jumla ya km 55
ambapo hadi sasa km 52.6 zimekamilika na zimebaki km 2.4 ili kukamilisha
mradi huo ambao utasaidia kusimamia moja ya sentensi ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya “Kuwatua akina
mama ndoo za maji kichwani”
Ili kufikia azma hiyo ya
kuwapatia maji safi na salama wakazi wa mikoa hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi na
Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang'ingo alisema kuwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu
Chini na ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu Chini hadi matanki ya Chuo Kikuu cha
Ardhi ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la maji katika jiji la Dar es salaam na
maeneo ya mkoa wa Pwani.
Akiongea na waandishi wa
habari ofisini kwake kabla ya waandishi hao kwenda kujionea hatua iliyofikiwa,
Mwang'ingo alisema kuwa ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo
Februari 2016 na kuondoa adha ya maji kwa wananchi na kuwaunganishia wengine
ambao hawakuwa na huduma ya maji.
“Tumelazimika kufikia
hatua ya kupanua huduma ya upatikanaji wa maji katika mikoa ya Dar es salaa na
Pwani kutokana na ongezeko la watu kulingana na sensa ya watu ya mwaka 2012,
mkoa wa Dar es salaam una jumla ya zaidi ya watu milioni 5 ambao watatumia maji
zaidi ya lita milioni 5 kwa siku”,
“Katika upanuzi huo,
kumekuwa na changamoto ya makazi ya watu kuwa ndani ya mradi ambapo kulikuwa na
kesi 17 katika mahakama mbalimbali katika maeneo hayo ikiwemo mahakama ya ardhi,
hadi sasa DAWASA imeshinda kesi 13 na kupewa haki ya kutumia njia hiyo
kukamilisha upanuzi wa mradi” alisema Mwang'ingo.
Kwa mujibu wa Mwang'ing'o
kesi nne bado zipo mahamani na ambazo zimefikia hatua mbalimbali kulingana na
taratibu za kimahakama. Lengo la mradi huu ni
kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 182 hadi 270 kwa siku. Mradi
ambapo awamu itakayofuata ni lita milioni 360 kwa siku.
Chanzo cha maji cha Ruvu
Chini ndiyo chenye kiwango kikubwa ambacho kina wapatia maji wakazi wa Dar es
salaam kwa zaidi ya asilimia 75 ikilinganishwa na asilimia 25 kutoka Ruvu
Juu. Mradi wa upanuzi wa
mtambo wa Ruvu Chini unalenga kuongeza uzalishaji maji na kuwahudumia wakazi wa
maeneo ya uwekezaji (EPZ) Bagamoyo, Chasimba, Buma, Zinga, Kerege na Mpiji mkoa
wa Pwani
Maeneo mengine
yatakayonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Dar es salaam ni Bunju, Wazo,
Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu, Goba, Kawe, Makongo, Mwenge, Msasani,
Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza, kijitonyama, Manzese, Konondoni, Magomeni,
Kigogo, Vingunguti, Buguruni, Kariakoo na Ilala.
Source: Michuzi Blog
0 comments:
Post a Comment