LONDON, ENGLAND
KOCHA wa Chelsea, Jose Mourinho, amesema kuwa mshambuliaji wake, Diego Costa, hawezi kumsumbua kutokana na tabia yake ya utovu wa nidhamu.
Mchezaji huyo juzi hakupata nafasi ya kucheza katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tottenham, ambapo timu hizo zilitoka suluhu, lakini alisimamishwa dakika ya 82 na kuanza kufanya mazoezi ya kupasha misuli ili aweze kuingia, lakini hadi dakika 90 zinamalizika hakupata nafasi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Costa aliamua kuvua jezi ya juu ambayo alikuwa anaitumia kwa ajili ya mazoezi na kumrushia Mourinho, kitendo hicho kimeonekana kuwa ni utovu wa nidhamu.
Hata hivyo, Mourinho amesema hakuna jambo lolote baya kati yake na mchezaji huyo, japokuwa alimuacha benchi.
“Hakuna ubaya wowote Costa kumuacha benchi, yalikuwa ni maamuzi yangu sahihi, pia nadhani tumecheza vizuri bila ya mchezaji huyo, huku wachezaji wengine kama Hazard na Oscar walifanikiwa kufika katika eneo la hatari, lakini hawakufanikiwa kupata bao.
“Lakini kwa kitendo cha Costa kurusha jezi ni utovu wa nidhamu, hata hivyo, wala hainisumbui kwa kuwa najua nilikuwa na maamuzi sahihi ya kumuweka benchi, lakini siyo lazima wachezaji wote wacheze, ila wanatakiwa kuwa tayari kwa kucheza wakipata nafasi na ndiyo maana wanakuwa pale,” alisema Mourinho.
Source: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment