Dar es Salaam. Ndani ya mwezi mmoja wa kwanza kazini, Rais John Magufuli kashika kila kona.
Jina lake limepenya na kutikisa maeneo mbalimbali duniani kwa kasi, ndani ya kipindi hicho kifupi. Shukrani kwa uamuzi mgumu anaoufanya katika kuboresha utumishi wa umma na kubana matumizi ya fedha za umma.
Umaarufu wa Rais Magufuli unazidi kuongezeka kuanzia kwa Watanzania ambao hawaamini yanayotokea hadi katika mabara mengine nje ya Afrika ambao wanaona kama miujiza mambo hayo kufanyikaTanzania, hasa katika bara ambalo awali liliitwa “jeusi.”
Tangu alipopiga marufuku safari za nje ya nchi kwa maofisa wa Serikali na shughuli hizo zifanywe na mabalozi waliopo katika mataifa husika, alipofanya ziara za kushtukiza Wizara ya Fedha, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kufuta sherehe za maadhimisho ya uhuru na kuelekeza kufanya usafi, Rais amekonga mioyo za wengi na kuacha mjadala mkubwa katika mtandao na vyombo vya habari.
Kwa kipindi cha wiki mbili na nusu sasa viunganishi vya #Magufuli, #WhatWouldMagufuliDo na #MagufuliEffect vinatamba kwenye mitandao ya kijamii hasa ya Twitter, Facebook na Instagram.
Katika mijadala hiyo Wakenya wamechukua nafasi kubwa kiasi cha kufanya kiunganishi #Magufuli kiongoze kwa muda mrefu nchini humo, licha ya kuwapo Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis.
Mtaalamu wa Tehama wa Kituo cha Kukuza Ubunifu na Ujasiliamali cha Buni Hub, Jumanne Mtambalike anasema Rais alishika kasi katika mitandao ya kijamii kwa sababu Wakenya ambao ni watumiaji wakubwa wa mtandao wa Twitter barani Afrika waliongoza kampeni hiyo.
0 comments:
Post a Comment