HOFU BANDARINI

1

MAJINA ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), waliohusika kutoa makontena 2,431 bila kulipa ushuru kati ya Machi hadi Septemba 2014 katika Bandari ya Dar es Salaam, yamepatikana na kufikishwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Taarifa zilizofikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa wahusika wote walioshiriki katika hujuma hiyo, majina yao yameshafikishwa kwa Waziri Mkuu na kinachoendelea ni uchunguzi wa kila mmoja wao.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Waziri Mkuu Majaliwa kufanya ziara ya ghafla wiki hii katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo alisema makontena hayo 2,431, yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu (ICD) nne ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM.
Kutokana na taarifa hiyo, Waziri Mkuu alimtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga, ampelekee majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo, ambapo jana ilithibitishwa kuwa kazi hiyo imekamilika na kinachofanyika ni uchunguzi wa watuhumiwa.
Mbali na kupeleka majina hayo, Mhanga pia alipewa wiki moja inayoisha Alhamisi ya wiki ijayo, kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo wa sasa bandarini na kuweka mfumo mpya wa malipo wa kielektroniki (e-payment). Uchunguzi Ingawa haijajulikana aina ya uchunguzi unaofanyika dhidi yao, lakini ni wazi moja ya hatua hizo za kiuchunguzi, itahusu namna walivyohusika na ukaguzi wa mali zao.
Tayari uchunguzi wa aina hiyo, umeshaanza kufanyika kwa watuhumiwa wa utoaji wa makontena 329 yaliyokuwa kwenye ICD ya Azam, ambayo yanakadiriwa kuipotezea Serikali zaidi ya Sh bilioni 80, ambapo taarifa zimeonesha kuwa baadhi walikaguliwa mpaka katika majumba yao.
Waziri Mkuu Majaliwa alipokwenda bandarini kwa mara ya kwanza kupitia ziara ya kushtukiza na kuibua upotevu wa mapato katika makontena hayo 329, aliagiza mali za watuhumiwa hao zichunguzwe, kama zinalingana na mapato ya mtumishi wa umma.
Aidha wiki hii katika utekelezaji wa agizo hilo, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango, aliagiza watumishi wote wa mamlaka hiyo, kuwasilisha taarifa sahihi ya orodha ya mali zote wanazomiliki kwa ajili ya uhakiki wa kina. Watumishi hao wametakiwa kuwasilisha taarifa hizo kwa uongozi wa juu wa mamlaka hiyo ifikapo Desemba 15 mwaka huu.
Agizo hilo limeambatana na onyo kuwa mtumishi yeyote, atakayebainika kuhusika na vitendo vyovyote vya ubadhirifu, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi, kulingana na makosa atakayokutwa nayo.
Wengi kupoteza kazi Hatua hiyo inazidisha wasiwasi wa kuongezeka watumishi wa Serikali walio katika hatari ya kusimamishwa kazi, baada ya wenzao 36 kusimamishwa kazi wiki hii na wiki iliyopita.
Walioanza kusimamishwa kazi Ijumaa ya wiki iliyopita walikuwa Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki; Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya; Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande; Hamisi Ali Omari (hakutajwa ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.
Siku hiyo hiyo waliyosimamishwa kazi vigogo hao, Rais John Magufuli, akamsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na kesho yake wakaongezwa watumishi wengine watatu; ambao ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
Kabla hali haijatulia, Alhamisi ya wiki hii watumishi wengine 27 wa TRA, walikamatwa katika geti namba tano na kusimamishwa kazi, kisha wakawekwa rumande kupisha uchunguzi wao.
Kortini Wakati uchunguzi huo ukiendelea, juzi maofisa waliosimamishwa kazi Ijumaa ya wiki iliyopita kwa upotevu wa mapato katika makontena hayo 329, akiwemo Masamaki (56), Mponezya (45), Mpande (28), Omari (48) na Eliachi (31), walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.
Washtakiwa hao pamoja na wafanyakazi wengine wa ICD ya Azam, walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi. Mbali na hao watumishi wa TRA, wengine waliopanda kizimbani kwa makosa hayo ni wafanyakazi wa Bandari Kavu (ICD) ya Azam, akiwemo Mkuu wa Ulinzi na Usalama, Raymond Louis (39) na Meneja Ashraf Khan (59).
Source: Habari Leo
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment