Kampuni hiyo ilitumika kama wakala wa ununuzi wa dhamana ya serikali (hati fungani) ya serikali zenye thamani ya Trilioni 1.2 katika serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwataja wamiliki wengine wa kampuni hiyo kuwa ni marehemu Dk. Fratern Mboya na Gasper Njuu na kwamba serikali inawataka kutoa ushirikiano kuhusu uchunguzi huo.
Akifafanua zaidi, Balozi Sefue alisema serikali ya Tanzania ilikopa Dola za Kimarekani milioni 600 kwa ajili ya maendeleo ya kawaida kutoka Benki ya Standard kupitia kampuni yake tanzu, Benki ya Stanbic Tanzania.
Alisema ada yake ilikuwa ni asimia 1.2, lakini iliongezwa nyingine kama hiyo kwa ajili wakala anayepokea fedha hizo ambaye hakuwamo kwenye makubaliano kati yao.
Balozi Sefue alisema kwamba akaunti ya kampuni ya Egma inayodaiwa kumilikiwa na Kitilya na wenzake iliyopo benki ya Stanbic Tanzania iliingiziwa Dola za Kimarekani milioni sita na zote zilitolewa mara moja.
CHENJI KUPANGIWA MATUMIZI
“Benki ya Standard haikuhitaji wakala wa kupokea fedha hizo na serikali na ushahidi huo umesababisha mahakama kutoa uamuzi wa Tanzania kurejeshewa dola hizo ambazo ni sawa na Shilingi billion 15… Rais Dk. John Magufuli ameagiza kwamba fedha hizo tutakapozipata kama atakuwa hajateua Baraza la Mawaziri, makatibu wakuu tutakaa kupanga matumizi yake,” alisema Balozi Sefue.
Akifafanua zaidi, alisema serikali inawaomba vigogo hao kutoa ushirikiano kwa serikali wakati wa uchunguzi ili kubaini namna gani zilitumika.
“Tunataka kujua fedha hizo kama zilitumika kuhongwa, tujue zimehongwa kwa nani … lazima tujue ilikuwaje zikaongezeka benki Stanbic Tanzania,” alisema Balozi Sefue.
TAKUKURU KIMYA
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, jana alishindwa kufafanua kwa undani suala hilo kama alivyoahidi juzi.
Hata baada ya mwandishi wetu kufika ofisini kwake kwa ajili kuelezea sakata hilo, hakupatikana, badala yake alimtumia Afisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, kuchukua maswali ambayo alitaka kuyapitia kwanza.
Baada ya kupelekewa maswali hayo, Kapwani alitoa barua yenye jibu kwamba tatizo hilo wanalifahamu na wanaendelea na uchunguzi kwa ajili ya kuchukua hatua.
“Tunafahamu tatizo hilo na uchunguzi unaendelea, ukikamilika hatua stahiki zitachukuliwa,” alisema.
Kwa upande wake, memejimenti ya Benki ya Stanbinc haikupatikana kuzungumzia suala hilo, baada ya wafanyakazi waliokutwa mapokezi kueleza kuwa msemaji yupo safarini Afrika Kusini kwa mafunzo.
“Mtu anayeweza kuzungumzia suala hilo yupo Afrika Kusini, hatujui atarudi lini na sisi tuliobaki hatua mamlaka ya kuzungumzia taasisi,” alisema mfanyakazi mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini.
SAKATA LENYEWE
Sakata hilo liliibuliwa juzi na Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kwamba Serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la kuchunguza makosa ya jinai (SFO), imeibua kashfa ya rushwa katika ununuzi wa hati fungani ya serikali katika kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete.
Katika taarifa yake, Zitto alidai kuwa biashara hiyo iliyofanyika kati mwaka 2011 na 2012, iliyohusisha serikali na benki ya Standard Group ya Afrika Kusini kupitia Stanbic ya Tanzania ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 600 (Sh. Tanzania trioni 1.2).
Benki ya Standard Group ambayo ni benki mama ya Stanbic Tanzania, imekiri makosa hayo na kukubali kulipa faini ya Dola milioni 25.2 (Sh. bilioni 54 ) kwa kosa hilo.
Ilikubali kulipa faini hiyo mbele ya Jaji Lord Justice Leveson, wakati shauri hilo liliposikilizwa juzi kwenye Mahakama ya Southwark nchini Uingereza.
Benki hiyo ilikubali shauri hilo limalizwe kwa njia ya muafaka baada ya kukiri ilitoa kiasi cha fedha ili kuwahonga maofisa wa Tanzania kinyume cha Sheria ya Rushwa ya Uingereza ya mwaka 2010 kufanikisha mpango wao.
Pia benki hiyo imekubali kulipa kiasi cha Dola milioni saba (Sh. bilioni 15.1) kwa Serikali ya Tanzania kama fidia ya shauri hilo baada ya kubainika walihonga baadhi ya maofisa wa Tanzania kufanikisha mpango huo.
Hata hivyo, fedha hizo hazitakabidhiwa moja kwa moja kwa Serikali ya Tanzania bali zitapitishwa kwenye Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza ili kupangiwa kazi ya kufanya.
Pia benki hiyo inatakiwa kulipa kiasi cha pauni 300,000(sawa na Sh. milioni 974) ikiwa ni gharama za shauri hilo kusikilizwa nje ya mahakama.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment