KIMBUNGA CHAWAKUMBA MABOSI TPA, TRL

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwaonyesha

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwaonyesha waandishi wa habari nyaraka zilizotumika kufanyia uchunguzi kabla ya kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kumsimamisha Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka kupisha uchunguzi, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue. Picha na Venance Nestory 
By Julius Mathias, Mwananchi
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametengua uteuzi na kumsimamisha kazi ya utumishi wa umma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka kwa kushindwa kusimamia uwajibikaji katika Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) na Kampuni ya Reli (TRL).
Mbali na Mwinjaka, Rais Magufuli pia amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe na kuagiza uchunguzi dhidi yao uanze mara moja.
Dk Magufuli hakuishia hapo kwani ameivunja pia Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa TPA sambamba na kutengua uenyekiti wa Profesa Joseph Msambichaka aliyekuwa anaiongoza  na utekelezaji wa maagizo yote umeanza tangu jana.
Miongoni mwa wajumbe wa bodi hiyo yumo, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu. Wengine ni Dk Francis Michael, Mhandisi Gema Modu, Mhandisi Musa Ally, Nyamsingwa, Crescentius Magori, Flavian Kinunda na Donata Mugassa.
Rais Magufuli amefanya uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na utendaji wa TPA ambao umedumu kwa muda mrefu bila kuchukuliwa hatua zozote za uwajibikaji miongoni mwa watendaji waandamizi wa taasisi hiyo na wizara husika.
Hata hivyo, ukiondoa mwenyekiti wa Bodi wa TPA, wajumbe wengine wapya ambao hawajadumu hata miezi miwili tangu aliyekuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba aizindue bodi hiyo Oktoba 29, mwaka huu.
Katika tukio la jana ambalo liliwakumba maofisa mbalimbali wa bandari, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Serikali haitavumilia kuona watu au kikundi chochote kilichojipanga kuhujumu mifumo au kuiba mapato yake kwa manufaa ya wachache kutokana na dhamana walizopewa.
“Ukaguzi wa ndani uliofanywa Julai 30, mwaka huu uligundua kuwapo kwa mianya mingi ya ukwepaji kodi yakiwamo makontena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi na Septemba mwaka jana kinyume cha taratibu. Vitendo hivi vimeonyesha kuwa bandari yetu hupitisha makontena mengi bila ya kulipiwa na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa,” alisema Majaliwa.
Novemba 27, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kwanza ya kushtukiza Bandari ya Dar es Salaam akiwa na nia ya kukagua shughuli zinavyoendelea na katika ukaguzi huo alifichua mwanya wa ukwepaji kodi kwa makontena 329 yenye thamani ya zaidi ya Sh80 bilioni na papo hapo akawasimamisha kazi watumishi sita akiwamo aliyekuwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na kuwazuia kusafiri kwenda nje ya nchi hadi uchunguzi utakapokamilika.
Katika mchakato huo, watumishi watatu walihamishwa kituo cha kazi, lakini siku iliyofuata nao walijumuishwa na wenzao sita na kutakiwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya uchunguzi ili kufanikisha ufuatiliaji wa namna ukwepaji huo wa kodi ulivyolikosesha Taifa mapato.
Majaliwa alirudi tena Bandari Desemba 4 kufuatilia hatua za kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali kabla hajagundua makontena zaidi yaliyopita bila kulipiwa ushuru, hali iliyoifanya TRA kuwachukulia hatua watumishi wake wote waliohusika.
Licha ya kufanikiwa kukusanya Sh5 bilioni ndani ya wiki moja baada ya ziara ya Majaliwa kutoka kwa wafanyabiashara wanaomiliki makontena hayo yaliyokwepa kodi, TRA iliwachukulia hatua watumishi 35 wa ngazi mbalimbali na kuwasimamisha kazi wengine wakiwamo 27 waliokamatwa gati namba 5 ambao wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano na uchunguzi zaidi.
Pamoja na hatua hizo za kuongeza uwajibikaji katika sekta ya umma, mamlaka hiyo ilifanikiwa kubaini kampuni 43 zilizohusika kwenye uingizaji wa makontena 329 ambayo yaliondolewa katika bandari kavu kinyume na taratibu.
Akionyesha kutoridhika na kile kilichofanywa, Majaliwa aliongeza idadi ya watumishi waliosimamishwa kutoka bandarini kwa kuwahusisha wengine 12 ambao watalazimika kutoa ushirikiano kwa vyombo vya uchunguzi baada ya kukabidhi ofisi zao.
“Bandari ni eneo muhimu ambalo likisimamiwa vizuri linaweza kukusanya fedha nyingi na kuchangia kwenye Pato la Taifa kwa kiasi kikubwa. Kwenye ziara nilizozifanya nimegundua kuna tatizo kwenye mfumo wa malipo. Nimeagiza mfumo uliopo ubadilishwe na badala yake uwekwe ule wa njia ya mtandao,” alisema.
Alienda mbali zaidi na kubainisha kwa kuwa ripoti ya uchunguzi iliwataja waliohusika na upitishaji wa makontena hayo na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao, alitangaza kuwasimamisha kazi wasimamizi wa bandari kavu (ICD) na viongozi wa sekta zilizoruhusu makontena hayo kutoka bandarini.
“Kuna watu waliruhusu makontena yatoke bandarini kwenda bandari kavu na wengine wakafanya hivyo wakiyatoa bandari kavu kwenda kwa wateja. Hawa wote nawasimamisha kazi kuanzia sasa,” alisisitiza Majaliwa katika mkutano wake na waandishi wa habari jana.
Waliosimamishwa kutoka idara ya usimamizi wa bandari kavu ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Mkango Alli na Steven Mtui. Wengine ni Titi Ligalwike, Lyidia Kimaro, John Elisante na James Kimwomwa aliyehamishiwa Mwanza ambaye atalazimika kutekeleza agizo hilo akiwa huko.
Kwa upande wa viongozi waliotoa ruhusa kwa makontena hayo kuondoshwa bandarini nao wamesimamishwa. Hao ni aliyekuwa Meneja Mapato ambaye amehamishiwa Kitengo cha Fedha cha Makao Makuu, Shaaban Mngazija, aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandarikavu ambaye pia amehamishiwa Makao Makao Makuu kwa Naibu Mkurugenzi Huduma za Biashara, Rajab Mdoe.
Wengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Ibin Masoud na Meneja Bandari Msaidizi Fedha, Apolonia Mosha.
Kwa upande wa Dk Mwinjaka, Waziri Mkuu alieleza kuwa amewajibishwa kutokana na kushindwa kuzisimamia mamlaka mbili, TRL na TPA ambazo zipo chini ya wizara yake.
Alifafanua kuwa TRL imepoteza Sh16 bilioni ambazo zilikuwa zitekeleze miradi kadhaa iliyopangwa, lakini haikuwa hivyo.
“Serikali ilitoa Sh13 bilioni na TRL wenyewe wakakopa Sh3 bilioni kutoka Benki ya TIB kwa ajili ya miradi, lakini fedha hizo hazikutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuisababishia serikali hasara. Rais ameagiza apishe uchunguzi wakati akisubiri kupangiwa majukumu mengine kama hatakutwa na hatia yoyote,” alisema Majaliwa.
Pamoja na hatua hiyo kuwakumba watendaji wa taasisi hizo na wizara, bila shaka zitakuwa zinawaweka njiapanda waliokuwa mawaziri wa wizara husika, Dk Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta.
Ufisadi TRL
Februari 2013, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Mwakyembe alizundua Bodi ya Wakurugenzi na kuwataka kuhakikisha wanasaidia kuimarisha TRL ili mizigo mingi inayokwenda mikoani na nje ya nchi isafirishwe kwa njia ya reli ili kuokoa ubora wa barabara na kupunguza gharama za kuzikarabati.
Machi 2013, TRL ilisainiana mkataba kununua mabehewa 25 aina ya Ballistic Hopper Bogie ya kubebea kokoto na kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries ya India. Mkataba huo ulikuwa na thamani ya Sh4 bilioni.
Aprili 2013, TRL iliipatia mkataba mwingine kampuni hiyo ya India  wa kutengeneza mabehewa mengine 274 ya mizigo na Serikali ikalipa Sh166 milioni kwa kila moja.
Julai 2014, mabehewa hayo yaliingia nchini na kuanza kutumika kwa ukarabati wa miundombinu ya reli hiyo kabla hayajagundulika kuwa hayakuwa na viwango vilivyokusudiwa.
Desemba 2014, mabehewa 20 kati ya 25 yaliyoingia yaligundulika kuwa yanamong’onyoka kama mihogo, hivyo kumlazimu waziri huyo kuunda kamati ya uchunguzi dhidi ya watendaji waliokwenda India kuyakagua.
Mwezi huo,  pia Dk Mwakyembe aliwatimua kazi watumishi sita wa TRL kutokana na tuhuma za wizi na kuliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na ikibainika kujinufaisha kwa namna yoyote mali zao zitaifishwe.
Januari 2015, baraza la mawaziri lilipovunjwa, Dk Mwakyembe alibadilishana wizara na Waziri Sitta. Wakati Mwakyembe akipelekwa Wizara ya Afrika Mashariki alikokuwa Sitta, Spika huyo wa Bunge la Tisa alipelekwa Wizara ya Uchukuzi.
Machi 2015, Sitta alizuia uingiaji wa mabehewa mengine 124 ya mizigo baada ya kubainika kuwa hayakuwa na ubora uliotarajiwa.
Aprili 2015, Sitta aliwatimua kazi vigogo wa TRL kutokana na zabuni mbovu ya mabehewa 274 na kuisababishia Serikali hasara ya Sh230 bilioni.
Madudu bandarini
Novemba 2012, Waziri wa Uchukuzi, Dk Mwakyembe alipokea ripoti ya uchunguzi wa tuhuma za upotevu wa mali na utendaji wa viongozi wa mamlaka hiyo.
Januari 2013, TPA ilibainika kubadili kipengele cha mkataba wa ujenzi wa mtambo wa kupakua mafuta melini (SPM) na kampuni ya Leighton ya Singapore. Bodi ya mamlaka hiyo ilitakiwa kujieleza.
Februari 2015, Sitta alimsimamisha kazi aliyekuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa TPA kutokana na malalamiko kwenye zabuni za mamlaka hiyo. Nafasi hiyo iliaza kukaimiwa na Awadhi Massawe.
Oktoba 2015, Awadh Massawe aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu Februari ya mwaka huu.
TRA
Moto unaofukuta hivi sasa TPA ulianzia TRA ambako watumishi 37 wa mamlaka hiyo ya kukusanya mapato ya Serikali walisimamishwa kazi akiwamo Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Rished Bade ili kupisha uchunguzi na baadhi yao tayari wamekishwa mahakamani.
Kusimamishwa kwa Bade na kuteuliwa kwa Kaimu Kamishna, Dk Phillip Mpango kulichangia kuchukuliwa kwa hatua za haraka ambazo zilifanikisha utambuzi wa kampuni zilizoondoa makontena hayo pamoja na bidhaa zilizokuwemo bila ushuru, hivyo kurahisisha ukusanyaji wa kodi inayostahili.
Makontena yaliyopotea yalibainishwa kuwa yanamilikiwa na kampuni 43 na yalikuwa na magurudumu  na betri za magari, samani, vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa nyingine mchanganyiko na tayari ukusanyaji wa mapato ya Serikali umeanza.
Licha ya hatua hizo, katika jitihada za kuzuia uwezekano wa baadhi kujichumia mali kwa njia zisizo rasmi, Dk Mpango aliwataka watumishi wa taasisi hiyo kuainisha mali zao kwa barua maalumu itakayopelekwa kwa uongozi wa TRA.
Katika kuuondoa mtandao wa uvunjifu wa taratibu bandarini hapo, siku ya kwanza ya ziara yake, Majaliwa aliwasimamisha kazi vigogo TRA kisha kuwahamisha wengine ingawa baadaye alibadili maamuzi hayo na kuwajumuisha ili uchunguzi ufanyike na kubaini ni kwa namna gani walivyoshiriki katika sekeseke hilo la kulihujumu taifa.
Source: Mwananchi

Kwa wale wanaohitaji kutengeneza kipato cha ziada mtandaoni, kama vile kina mama walioko majumbani, wanafunzi, wastaafu na wafanyakazi wanaopenda kujipatia kipato kingine zaidi ya walicho nacho.

        

                                          Bonyeza hapa ujiunge na uanze kuvuna hela
                 or 
               click here to join and start earning
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment