Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais John Magufuli kukaa zaidi ya mwezi mmoja bila kuteua Baraza la Mawaziri huenda ukawa umeisaidia Serikali kwa kuokoa takribani Sh683.3 milioni za walipa kodi, bila kuhusisha gharama za ununuzi wa ‘mashangingi’.
Kiasi hicho cha fedha kimetokana na hesabu inayokadiriwa kuwa matumizi ya waziri iwapo Rais Dk Magufuli angeendelea na ukubwa wa Baraza la Mawaziri la mwisho la Rais Jakaya Kikwete la mawaziri 55, kati ya hao 24 wakiwa manaibu waziri.
Hata hivyo, Dk Magufuli ameshatangaza kuwa na baraza dogo la mawaziri, ingawa hajaweka bayana litakuwa na jumla ya mawaziri wangapi.
Kwa mujibu wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole-Medeye, Waziri hulipwa mshahara wa kati ya Sh3.8milioni mpaka Sh 5milioni kwa mwezi ambazo ni sawa na mshahara wanaolipwa wabunge.
Kwa mantiki hiyo, kwa mawaziri 55, Serikali ilitakiwa ilipe Sh209 milioni kwa ajili ya mishahara ya Novemba, lakini hazikulipwa kwa kuwa bado kiongozi huyo hajawateua.
Kanuni za kudumu za utumishi wa umma toleo la mwaka 2009, zinaitaka Serikali kumpatia nyumba mtumishi anayetakiwa kupatiwa huduma hiyo kwa aidha kumpa nyumba ya Serikali au kumkodishia nyingine yenye hadhi ili aweze kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Kanuni hizo zinamtaka Wakala wa Majengo (TBA) kufanikisha zoezi hilo la kutoa huduma za nyumba au kusimamia ukodishaji wa nyumba husika ya mtumishi.
Mawaziri ni miongoni mwa watumishi wanaopatiwa nyumba za Serikali ambazo nyingi zinapatikana katika maeneo ya vigogo ya Masaki, Oysterbay au Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa tovuti ya uuzaji na ukodishaji nyumba na viwanja ya Lamudi, nyumba za bei ya wastani ambayo inaweza kwenda na hadhi ya waziri inakodishwa kwa kiasi kisichopungua Sh5 milioni kwa mwezi.
Hivyo basi, kama nyumba za mawaziri hao ambazo hukarabatiwa na kuhudumiwa na TBA, zingekuwa zimekodishwa kutoka kwa watu binafsi kwa kipindi cha mwezi mzima basi Serikali ingelipa Sh275 milioni.
Ili kutimiza majukumu yao vyema wakiwa bungeni mjini Dodoma, mawaziri pia hupatiwa nyumba za kuishi tofauti na zile za Dar es Salaam ambazo zipo chini ya TBA.
Hata hivyo, Ole-Medeye alisema Serikali huwalipa mawaziri Sh800, 000 kwa mwezi kwa ajili ya huduma za nyumba za Dar es Salaam, mawasiliano na ankara nyingine za kumsaidia kimaisha.
Iwapo kiwango hicho cha Sh800, 000 kwa mwezi kingetumika kumlipa kila waziri kama sehemu ya fedha za makazi, bado Serikali ingehitajika kutoa Sh44 milioni kwa ajili ya gharama za kuhudumia nyumba na mawasiliano.
“Hivi Sh800, 000 utapata wapi nyumba ya kukodi akaishi waziri? Kwa bei ya sasa nyumba za kiwango hicho ni Dola za Marekani 3,000 (Sh6 milioni) au zaidi.
“Sasa fedha hiyo umlipe mtumishi wa ndani, gharama za umeme, mawasiliano na maji ndiyo maana nasema uwaziri ni kazi ya kuhudumia jamii,” alisema Ole-Medeye akieleza kuwa waziri hupatiwa posho ya Sh80, 000 kwa siku akiwa mikoani kwenye ziara.
Gharama za posho za mawaziri hao zingetegemea na siku ambazo wangekaa mikoani kwa kipindi hicho cha siku 31, na hivyo si rahisi kujua kiwango chake.
Gharama za samani
Miongoni mwa mambo ambayo Serikali hugharamia kwa mawaziri wake ni samani za ndani ya nyumba, ambazo pia huongezeka au kupungua kulingana na ukubwa wa baraza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Adelhelm Meru alisema ununuzi wa samani za ndani ya nyumba za waziri husimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa wizara zote na hununuliwa kila baada ya miaka mitano.
Hata hivyo, Dk Meru alitoa angalizo kuwa matumizi ya waziri husika huchangiwa pia na ukubwa wa wizara na kiwango cha bajeti.
“Mawaziri wengine wanaishi kwenye makazi yao na siyo wote wamepewa makazi ya Serikali.
“Lakini wanapewa huduma ya umeme, maji, posho ya majukumu na gari,” alisema Dk Meru.
Mashangingi
Mawaziri pia hupatiwa magari kwa ajili ya usafiri na mara nyingi huwa na ama Toyota Land Cruiser VX V8 au GX V8 ambayo hujulikana kama “mashangingi.”
Ili kufanikisha shughuli zao, kila waziri hupatiwa lita 1,000 kwa mwezi za mafuta. Kwa bei elekezi ya sasa ya Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (Ewura), iliyoanza kutumika Desemba 2, bei ya dizeli jijini Dar es Salaam ni Sh1,823 kwa lita.
Gari moja la waziri mmoja iwapo lingetumia lita zote 1,000 Serikali ilitakiwa kulipa Sh1.823 milioni ambazo kwa baraza zima ingekuwa jumla ya Sh100.3 milioni.
Pia, magari hayo huitaji kufanyiwa matengenezo kwa kila baada ya kilomita zinazoshauriwa na mtengenezaji.
Dk Meru alisema kwa kawaida kila gari hufanyiwa matengenezo baada ya kilomita 5,000 kwa kiasi cha wastani Sh1.8 milioni kila moja.
Kwa maana hiyo, katika Serikali ya “hapa kazi tu” inayohimiza viongozi wa kutoka maofisini kwenda kusikiliza shida za wananchi vijijini, hapana shaka kuwa mawaziri hao wangekuwa ama wameshatimiza kilomita zinazohitaji matengenezo au wanakaribia.
Serikali kufanikisha matengenezo hayo, ingeweza kulipa kampuni husika ya matengenezo Sh99 milioni kwa mwezi.
Gharama hizo ni mbali na fedha za kununua magari hayo ambayo kila moja linakadiriwa kugharimu Sh250 milioni, hivyo mawaziri 55 wangetafuna Sh13.75 bilioni.
Unafuu wa gharama katika eneo la ununuzi wa mashangingi hayo utakuwa dhahiri iwapo Rais Magufuli atatekeleza ahadi yake ya kuteua baraza dogo, mathalan, akiteua mawaziri 20 atakuwa ameokoa mashangi ya mawaziri 35, sawa na Sh8.75 bilioni.
Ukimya wa Rais Magufuli kutoteua Baraza la Mawaziri kwa kipindi cha mwezi kumeibua mtizamo tofauti miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya Siasa na utawala, wengi wakisema kuna faida nyingi kuliko hasara.
Source: Mwananchi
Kwa wale wanaohitaji kutengeneza kipato cha ziada mtandaoni, kama vile kina mama walioko majumbani, wanafunzi, wastaafu na wafanyakazi wanaopenda kujipatia kipato kingine zaidi ya walicho nacho.
0 comments:
Post a Comment