MABADILIKO BILA MAADILI KWENYE KATIBA MPYA KAZI BURE - WARIOBA

“Tangu mwaka 1996 hadi leo rushwa bado ni
“Tangu mwaka 1996 hadi leo rushwa bado ni tatizo, tulisema kila kitu kiwe  wazi, lakini bado sijaona uwazi na uwajibikaji.” Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba 
By Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema nchi haiwezi kuwa na mabadiliko ya kweli, kama miiko na maadili ya viongozi havitaingizwa kwenye Katiba Mpya.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo ya maisha ya utumishi wa umma uliotukuka juzi, Warioba alisema kwa miaka mingi akishirikiana na rafiki zake, walijaribu kuleta mabadiliko makubwa katika jamii, bila mafanikio.
“Huwezi kuwa na mabadiliko kama huna miiko na maadili kwenye Katiba, lazima kuwe na separation of power (kutenganishwa kwa madaraka), naamini kanuni hizi zitaingia kwenye Katiba Mpya,” alisema.
Mara kadhaa Jaji Warioba amekuwa akisisitiza umuhimu wa vipengele hivyo viwili kuingizwa kwenye Katiba Mpya. Katika rasimu ya pili ya Katiba, Tume  ya Mabadiliko ya Katiba, aliyokuwa akiiongoza ilipendekeza miiko na kanuni za uongozi kama tunu za Taifa, lakini Bunge Maalumu la Katiba  liliyaondoa na kuyaweka katika msingi wa utawala bora.
Jaji Warioba amekuwa akihoji kuwa uzalendo na uadilifu si mpaka mtu awe kiongozi na kwamba mambo hayo mawili si misingi ya utawala bora ni  ya kitaifa na inamhusu kila Mtanzania.
Azungumzia tuzo
Akiizungumzia tuzo hiyo aliyopewa na Umoja wa Maofisa Watendaji wakuu wa Kampuni Binafsi (CEOrt), Warioba alisema anaamini alipewa heshima hiyo, kutokana na mchango wake alioutoa kwenye sekta binafsi alipokuwa Waziri Mkuu wakati wa Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi.
Alisema kutokana mabadiliko ya mfumo wa maisha duniani wakati huo, Tanzania ilijikuta imeingia kwenye soko la uchumi bila kujiandaa, ndipo alipoomba msaada wa kitaalamu kutoka sekta binafsi.
“Nikiwa Waziri Mkuu nikasema sekta binafsi wasaidie, nikaunda tume walikuwapo pia wasomi, mchango wao ulikuwa mkubwa sana,” alisema.
Kuhusu rushwa
Pia, alizungumzia ushiriki wake katika tume ya kuchunguza mianya ya rushwa aliyokuwa mwenyekiti wake. Alisema ilifanya kazi kubwa ya kupambana na rushwa, lakini haikufanikiwa kiasi cha kutosha kwa kuwa bado vitendo hivyo vinaendelea mpaka sasa.
“Tangu mwaka 1996 hadi leo rushwa bado ni tatizo, tulisema kila kitu kiwe  wazi, lakini bado sijaona uwazi na uwajibikaji. Tulisema rais amtake kila kiongozi baada ya miezi sita aonyeshe alivyofanya kupambana na rushwa kwa uwazi,” alisema.
Awali, Mwenyekiti wa CEOrt, Ali Mufuruki, alisema takribani miaka 20 iliyopita Warioba aliweka msingi wa namna ya kupambana na rushwa ambao mpaka sasa bado unaendelea kutumika.
“Pia amefanya hivyo katika mchakato wa kupata Katiba Mpya,” alisema.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva na Katibu Mkuu mstaafu wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim.
Source: Mwananchi


Kwa wale wanaohitaji kutengeneza kipato cha ziada mtandaoni, kama vile kina mama walioko majumbani, wanafunzi, wastaafu na wafanyakazi wanaopenda kujipatia kipato kingine zaidi ya walicho nacho.

Share on Google Plus

About Mind 2022

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment