RAIS John Magufuli amegeuka gumzo kimataifa, kutokana na kasi ya mabadiliko ya kweli ya uongozi wake katika kipindi kifupi, hasa kudhibiti matumizi na kueleza fedha katika huduma za jamii.
Aidha, uongozi wake umeelezwa kuwa wa mfano, kwani miongoni mwa mambo anayoyafanya, yanagusa ulimwengu na anatekeleza yote bila kufanya safari yoyote ya nje ya nchi kama wanavyofanya viongozi wengine.
Tangu aingie madakarani mwezi mmoja na siku chache zilizopita, Dk Magufuli amedhibiti mabilioni ya fedha na kuwezesha fedha hizo kuboresha huduma za afya, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s), shule na miundombinu ya barabara.
Gazeti la The Sunday Independent linalochapishwa na chombo cha habari chenye nguvu nchini Afrika Kusini, liliandika katika tahariri yake hivi karibuni katika kichwa cha habari kisemacho, “Afrika ifuate mfano wa Tanzania.” Tahariri hiyo iliyochapishwa Jumapili iliyopita, ilisisitiza kuwa utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Sita wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC), unahitaji Rais kama Magufuli ambaye ameonesha kwa dhati nidhamu katika matumizi ya serikali.
Gazeti hilo limekuwa miongoni mwa vyombo vya habari vinavyosifu utendaji wa Dk Magufuli, ambaye anafanya kazi bila Baraza la Mawaziri kwa zaidi ya siku 30 tangu aapishwe. Baadhi ya waandishi wa habari kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, walilieleza gazeti dada la gazeti hili, Daily News katika siku za mwisho wa mkutano wa FOCAC kwamba wameguswa kwa utendaji wa Dk Magufuli na kuwataka viongozi wengine wa Afrika kuiga.
Mwandishi wa gazeti la Daily Graphic la Ghana, Emmanuel Adu- Gyamerah alisema kazi anayofanya Dk Magufuli, ikiwamo kubadili sherehe za Uhuru ambazo mataifa mengi huzifanya kwa gharama kubwa, ni jambo ambalo viongozi wengi wa Afrika wameshindwa, lakini yeye amefanya kwa muda mfupi tangu aingie madarakani. “Hii hatua ya kupunguza matumizi inapaswa kufanywa na Waghana pia,” alisema Adu-Gyamerah.
Dk Magufuli alibadili namna ya kusherehekea sikukuu ya Uhuru na kuagiza Watanzania wote wafanye usafi katika maeneo yao ya kazi na makazi ili kupambana na magonjwa ya mlipuko, ikiwamo kipindupindu na kutunza mazingira. Baadhi ya wananchi wa Rwanda, walieleza kuwa hatua aliyochukua Dk Magufuli kuhusu sherehe za uhuru ni “ya Kinyarwanda” kwa kuwa kwao serikali ilifanya Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi kuwa siku rasmi ya usafi nchi nzima.
Mtangazaji wa Televisheni ya China (CCTV) wa Kenya, alisema kufuta safari za nje ni moja ya hatua muhimu na alisema Wakenya wamekuwa wakizungumzia safari za Rais wao, Uhuru Kenyatta anazofaa nje ya nchi.
“Natamani hatua kama hizi zifanyike pia nchini mwangu,” alisema mtangazaji huyo huku akiionesha Daily News ujumbe wa twita unaoonesha sifa kemkem kwa Dk Magufuli. Gazeti la Sunday’s Paper of New Zimbabwe liliandika hivi, “Tanzania’s Magufuli: A new African” (Magufuli wa Tanzania: Mwafrika Mpya”, ikieleza kuwa Dk Magufuli ameleta mapinduzi na njia mpya katika kutawala.
Gazeti hilo lilieleza kuwa, uongozi wa Dk Magufuli umelenga kushughulika na wavivu na wala rushwa na kuandika, “Mpaka sasa mambo ni mazuri; hongera Magufuli.” Gazeti la mtandaoni la Nigeria, naij.com, lilieleza kuwa hatua ya kupunguza matumizi ni ya kuchukuliwa na serikali ya Nigeria vile vile. Naij.com ilimnukuu mhariri wake, Abang Mercy akitwiti hivi karibuni na kuandika ujumbe huu, “Tangu achaguliwe, Rais wa Tanzania, John Magufuli ametekeleza mabadiliko makubwa; na ndivyo ninavyotarajia kwa Rais Buhari (Rais wa Nigeria).”
Gazeti hilo la mtandaoni lilimfananisha Dk Magufuli na Baba wa Taifa wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, mwasisi na mtu asiyekwepeka katika historia ya Tanzania. Gazeti la Daily Nation la Kenya limeripoti kuwa hatua ya Dk Magufuli kuzuia safari za nje, inapaswa kuchukuliwa pia nchini humo, hasa kutokana na wananchi kuonesha kutokupendezwa na safari za Rais Kenyatta nje ya nchi.
Aidha, suala la kupunguza matumizi kwa kuzuia kuchapisha kadi za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa taasisi na mashirika ya umma, limepongezwa pia na kumtaka Kenyatta kuiga mfano huo.
Source: Mwananchi
Kwa wale wanaohitaji kutengeneza kipato cha ziada mtandaoni, kama vile kina mama walioko majumbani, wanafunzi, wastaafu na wafanyakazi wanaopenda kujipatia kipato kingine zaidi ya walicho nacho.
0 comments:
Post a Comment