MAKONTENA TISA YAKAMATWA DAR

Makontena yaliyokamatwa na polisi kwa

Makontena yaliyokamatwa na polisi kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika eneo la Mbezi Tangibovu Dar es Salaam jana baada ya kudaiwa kupitishwa bandarini bila kulipiwa ushuru. Picha na Said Khamis 
By Kalunde Jamal, Mwananchi
Dar es Salaam. Mamlaka ya Bandari Tanzania (PTA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamekamata makontena tisa yanayodhaniwa kukwepa kulipa kodi.
Makontena hayo yalikamatwa jana, ikiwa ni mwendelezo wa watumishi tisa wa Bandari na TRA waliosimamishwa wiki iliyopita na Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa kupisha uchunguzi wa upotevu wa makontena 349 na ukwepaji wa kulipa kodi. Katika mwendelezo huo, juzi TPA ilitangaza kuwasimamisha kazi maofisa wake watatu katika sakata hilo.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Ben Usaje jana alisema kuwa baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa makontena yanayoshushwa usiku katika eneo la Mbezi Tangi Bovu, alituma vijana wake wa pikipiki kufanya doria kuthibitisha.
Alisema aliwashirikisha polisi na TRA, na operesheni ilifanyika usiku na kubaini kuwapo kwa makontena hayo yakiwa yamesafirishwa kutoka bandari kavu ya PMM, iliyopo Vingunguti na kushushwa kwenye ghala lisilo rasmi.
Madereva wa magari yaliyobeba makontena hayo walikamatwa na makontena yenyewe na mizigo yake kuzuiliwa.
“Wananchi waiamini bandari, watoe ushirikiano kila wanapoona kuna kitu siyo cha kawaida kinafanyika, wataona jinsi ilivyo na ufanisi, kwa sababu hakuna aliye juu ya sheria,” alisema Usaje.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo aliyekuwapo eneo la tukio alisema baada ya kuarifiwa, walituma kikosi cha kwanza cha doria, kwa ajili ya kuzunguka eneo hilo na kukamata makontena hayo yakiwa na mizigo ambayo kwa kila dalili ilionekana haijalipiwa kodi kutokana na njia za kufika hapo kuwa za siri, ikiwamo kusafirishwa usiku.
Alisema kibali cha kusafirisha makontena hayo kilionyesha ni cha Septemba 17, mwaka huu, hivyo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za bandari kimepitwa na wakati na mzigo huo umetoka kiujanja ujanja, bila kufuata taratibu za utoaji mizigo.
Alifafanua kuwa siyo tu kibali kimepitwa na wakati bali hata nyaraka za makontena hayo zinaonyesha yalikuwa yapelekwe Kituo cha Uwekezaji EPZ eneo la Ubungo External, badala yake yalipelekwa kwenye ghala hilo ambalo si bandari kavu na wala halitambuliwi na TPA wala TRA.
Kayombo alimtaja mmiliki wa makontena hayo kuwa ni Heritage Empire Company Limited, wakala wa forodha akiwa anatambulika kama Nipoc Africa Company Limited. Baada ya kuyafungia makontena hayo, Kayombo alitangaza kutoa saa 24 kumtaka wakala husika ajitokeze na kutolea maelezo mzigo huo na asipofanya hivyo watayataifisha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alipoulizwa alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu halihusiani na wizi wala upotevu wa mali, bali wenye mamlaka ya kuzungumzia hilo ni watu wa Bandari na TRA.

PMM yakanusha
Baadaye jana taarifa ya kampuni ya PMM ICD iliyotumwa kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa makontena hayo yametoka kihalali na yamefuata sheria na taratibu za kulipa kodi na nyaraka zinazoonyesha uhalali zipo. Taarifa hiyo iliyosainiwa na Philip Mhina kwa niaba ya mkurugenzi, ilieleza kuwa kilichotokea ni wanahabari na maofisa wa TRA na TPA kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu makontena hayo. Ilieleza kuwa makontena hayo yalikuwa yanatoka Bandari Kavu ya PMM na huko yalikokutwa yalikuwa yanapelekwa kwenye yadi kwa makubaliano na mteja wao.

Makontena yafunguliwa
Baadaye jioni makontena hayo yalifunguliwa, manne kati ya hayo, yalikutwa na nguzo za chuma na mabati ya kuingiza mwanga kwa ajili ya ujenzi na hadi tunakwenda mitamboni mengine yalikuwa yanaendelea kufunguliwa.

…Lanaswa na magogo 290
Katika hatua nyingine, polisi kwa kushirikiana na maofisa wa TRA mkoani Mbeya wamekamata kontena moja likiwa na magogo 290 ya mti aina ya mkula katika eneo la Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia. Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Ahmed Msangi alisema magogo hayo yalikamatwa mwishoni mwa wiki baada ya polisi na maofisa hao kukagua njia za panya na kukutana na lori likiwa na kontena.
Alisema lori hilo lilipelekwa kituo cha Polisi Tunduma na kumtaka dereva achukue nyaraka za kusafirisha magogo hayo, lakini mpaka jana hakuonekana.
Vilevile, maofisa hao waliyakamata magari manane yakidaiwa kubadilisha namba kinyemela bila ya kulipia kodi halali ya Serikali.
Msangi na Ofisa Forodha Mwandamizi TRA, Jommassa Nsindo walisema magari hayo yalitolewa bandari ya Dar es Salaam yakidaiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa namba za IT, lakini yalipovuvuka Tunduma kwenda Zambia yakapewa namba za Tanzania na kurudi nchini.
Nyongeza na Lauden Mwambona
Source: Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment