MWAKYEMBE - NITAENDA SAWA NA MAGUFULI



Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema atafanya kazi kwa kasi ya Rais Magufuli katika kukabiliana na changamoto zilizopo katika wizara hiyo.
Amesema changamoto ziko nyingi kuanzia chini mpaka juu, katika Mahakama, magereza na kwingineko, hivyo aliomba apewe muda kuangalia hali ikoje ili abadilishe mifumo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Akizungumzia suala la Katiba Mpya, alisema Rais alieleza vizuri kuwa litafanyiwa kazi, kwani halikuishia pabaya hivyo muda ukifika litakamilika.
Alisema watafanya kazi kubwa ili mfumo wa sheria usiwe pingamizi, bali uendeleze kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli. Nape Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye alisema atatengeneza utaratibu katika wizara hiyo, ili kuondoa utamaduni wa mtu mmoja kufanya mambo mengi peke yake na kuahidi kuwa msikivu na kutengeneza sheria, ili kila mmoja atimize wajibu.
Akizungumzia changamoto katika michezo, Nape alisema tatizo katika michezo ni usimamizi wa sheria na kutokuwa na nidhamu kwa kila mtu kufanya anavyotaka. Alisema zamani wanamichezo walikuwa wakifanikiwa kutokana na nidhamu, hivyo watasaidiana na wadau mbalimbali kurudisha nidhamu.
Manyanya na elimu ya juu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya, alisema kinachosubiriwa ni kasi ya kuleta mabadiliko kwa muda muafaka na jambo la msingi ni kazi na kila mtu ahakikishe anatimiza wajibu wake.
Alisema changomoto katika wizara hiyo ni nyingi, ikiwemo suala la mikopo ya elimu ya juu na kusisitiza kwamba wanafunzi wote wenye sifa ya kupata mikopo, wanapaswa kupewa kwa kuwa huo ni mkopo ambao wataurudisha.
Manyanya alisema wizara hiyo haitamvumilia mwalimu yeyote mzembe, atakayetumia muda wake vibaya kwa kutotimiza wajibu, kwa kuwa hatua zitakazochukuliwa ni kumfukuza kazi na sio kuhamishwa kituo cha kazi.
Mhagama, Kairuki Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alimshukuru Rais kutambua mchango wake katika Serikali iliyopita na kilichobaki ni kutimiza wajibu wao katika wadhifa huo.
“Rais katambua mchango wangu, nashukuru na sasa ni kuhakikisha nakwenda na kasi yake, ili tumsaidie kutimiza ndoto za wananchi na hasa kuondokana na tatizo la ajira,” alisema Mhagama.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema anawiwa deni kubwa kuhakikisha anakwenda na kasi ya utendaji kazi ya Rais Magufuli.
Habari Leo
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment