RAIS MAGUFULI AJIWEKEE VIPAUMBELE VINAVYOTEKELEZEKA



Profesa Ibrahim Lipumba

Profesa Ibrahim Lipumba 
By Ibrahim Lipumba,Mwananchi
Rais John Magufuli amelifungua Bunge la Kumi na Moja kwa kutoa hotuba nzito inayoonesha azma yake ya kupambana na kero zinazowakabili wananchi. Kwa yeyote aliyemsikiliza vizuri aliamini kuwa ile ni hotuba yake inayowafahamisha Watanzania nia yake thabiti ya kupambana na kutatua matatizo yao.
Alianza hotuba yake kwa kuanisha mambo na kero takribani 22 alizoyabaini kuwa zililalamikiwa na wananchi wakati wa kampeni.
Kero hizo ni pamoja na rushwa iliyokithiri katika maeneo yote yanayowagusa wananchi wa kawaida, utendaji mbovu wa Serikali za Mitaa hususani upotevu wa mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango na migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, mipango miji, kujenga maeneo ya wazi.
Mwingine ni rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu kwenye bandari zetu; kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma ya maji kupatikana mbali na makazi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutofanya kazi kwa ufanisi kutokana na kuwapo na ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa kushindwa kukusanya kodi.
Pia, kukatika kwa umeme mara kwa mara na uwapo umeme wa mgao unaosababishwa na utendaji mbovu wa TANESCO. Ujangili ambao lazima idara husika za Maliasili na Utalii zinashiriki, migogoro ya mipaka kati ya vijiji na Hifadhi na upotevu wa mapato.

Huduma za afya
Huduma duni za afya ambazo ziko mbali na wananchi, ukosefu wa madawa, hujuma kwenye vifaa vya vipimo, msongamano wa wagonjwa na tozo zisizostahili, lugha mbaya za watumishi kwa wagonjwa, uhaba wa majengo na vitendea kazi.
Rasilimali watu na fedha, kushindwa kukusanya mapato yanayowahusu, kutoa hovyo hati za uraia na vibali vya kuishi nchini kwa wageni, kushindwa kusimamia ajira za wageni hususan kwa kazi zinazoweza kufanywa na wazawa na elimu duni inayosababishwa na uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya lazima.
Malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni pamoja na majengo, madawati na ukosefu wa nyumba za walimu.
Polisi wanalalamikiwa kuwabambikia kesi wananchi , upendeleo, madai ya malipo ya askari, ukosefu wa nyumba za askari, ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa; zimamoto kuchelewa kufika kwenye matukio na kufika kwenye matukio bila vitendea kazi kama maji.
Kucheleweshwa kwa magari yanayosafiri kwenye maeneo ya mizani, mrundikano na ucheleweshwaji wa kesi katika mahakama, wenyeji kutofaidika na sekta ya madini, kampuni za madini kutolipa kodi stahiki na vilio vya wachimbaji wadogowadogo kutengewa maeneo ya uchimbaji na kupatiwa mikopo na usumbufu wa kulipwa fidia.

Kilimo
Kero nyingine ni uhaba wa pembejeo za kilimo na mifugo, tatizo la masoko, wakulima kukopwa mazao ya, ukosefu wa wataalamu wa ugani, upungufu wa maghala, mabwawa, malambo na majosho, vifaa duni vya uvuvi ukosefu wa masoko, uvuvi haramu, na uwekezaji mdogo katika sekta ya uvuvi hususan viwanda vya mazao ya uvuvi na hasa katika ukanda wetu wa bahari.

Reli
Uchakavu wa miundombinu ya reli, kutokuwapo kwa usafiri wa uhakika wa reli, upungufu wa bandari kavu, mizigo mingi kusafirishwa kwa barabara na Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) lina wafanyakazi zaidi ya 200, wanalipwa mishahara ila wana ndege moja.
Haki za makundi maalumu ya wazee, walemavu, wanawake na watoto zimekuwa zikikiukwa; mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, kulinda haki na masilahi ya wafanyakazi, wasanii na wanamichezo.
Baada ya kuainisha kero alizozibaini, Rais Magufuli alieleza mkakati wake wa kushughulikia matatizo hayo. Ninakiri kuwa mambo mengi aliyoyazungumzia yanafanana na sera za Chama Cha Wananchi (Cuf) tulizokuwa tunazijadili katika mikutano yetu na Ilani zetu za uchaguzi.
Rais alisisitiza umuhimu wa miundombinu ikiwa nia pamoja na kuendeleza ujenzi wa barabara mbalimbali za kuunganisha miji yetu mikuu ya mikoa na wilaya; barabara ziendazo kwenye maeneo muhimu ya kimkakati na kiuchumi; na upanuaji wa barabara za miji kama Dar es Salaam kwa kujenga ‘flyovers’, barabara za pete ‘ring roads)’.

Ilani ya CCM
Ilani ya CCM imeweka malengo ya kumalizia miradi ya sasa ya ujenzi wa barabara za kilomita 2,440, kujenga barabara nyingine za lami kilomita 5,427, kukamilisha upembuzi yakinifu wa kilomita 6,531, kumaliza ujenzi wa madaraja makubwa sita, kukarabati na kujenga madaraja mapya saba, kujenga flyovers tisa Dar es Salaam, kujenga kilomita nyingine 43 za mabasi ya abiria – BRT na barabara nyingine za lami kilomita 139 jijini Dar es Salaam.
Gharama za miradi yote hii siyo chini ya dola milioni 8000 sawa na asilimia 17 ya pato la taifa.

Kuhusu reli
Kuhusiana na reli, Rais Magufuli akizingatia Ilani ya CCM amejiwekea malengo makubwa ya kuelekeza nguvu za Serikali katika kwa miaka mitano ijayo katika ujenzi wa reli mpya katika kiwango cha kimataifa (yaani standard gauge).
Reli ambazo Serikali yake inakusudia kuanza kuzijenga ni reli ya kati Dar es Salaam – Tabora – Kigoma na tawi lake la Tabora – Mwanza yenye urefu wa km 1629.
Reli mpya ya kutoka Uvinza kwenda Musongati, Burundi yenye urefu wa kilomita 195. Reli mpya ya kilomita 386 kutoka Isaka kwenda Kigali Rwanda. Nyingine ni reli ya Mtwara – Songea – Mbamba Bay na matawi ya kwenda Mchuchuma na Liganga yenye urefu usiopungua kilomita 1050. Reli ya Tanga – Arusha – Musoma nayo ni kilomita 1047 na reli ya Kaliua – Mpanda – Karema yenye urefu wa kilomita 251.
Jumla kilomita 4,558 za reli mpya kwa kiwango cha standard gauge. Ikiwa gharama ya maandalizi na ujenzi wa kilomita ya reli ni dola milioni 2, zitahitajika dola milioni 9116 sawa na asilimia 19 ya pato la taifa la mwaka 2014.

Bandari
Rais Magufuli ana lengo la kuimarisha bandari zetu. Ilani ya CCM inaeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano Serikali itakamilisha uboreshaji wa magati saba, kujenga magati mengine mawili na gati moja la magari katika bandari ya Dar es Salaam. Itakamilisha ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo na Mwambani, Tanga. Bandari ya Mtwara itajengewa magati mapya manne. Serikali pia itajenga bandari ya Nyamisati kurahisisha usafiri wa kwenda Mafia.

Maji
Rais Magufuli amejiwekea lengo la kuwatua kina mama ndoo za maji vichwani. Serikali yake “itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 95 kwa maeneo ya mijini ifikapo 2020.”
Hivi sasa ni asilimia 45 ya wananchi vijijini na asilimia 75 ya wananchi mijini ndiyo wanaopata huduma za maji. Maji yenyewe siyo safi na salama.
Kuhusu nishati ya umeme, Ilani ya uchaguzi ya CCM inalenga kuongeza uwezo wa kufua umeme kwa karibu mara tatu, kutoka megawati 1308 za sasa mpaka kufikia 4915 mwaka 2020. Kuunganisha mikoa yote kwenye gridi ya taifa na kuhakikisha asilimia 60 za kaya zote zinatumia umeme.
Huduma za afya zinatarajiwa kuboreshwa kwa kuhakikisha kila kijiji kina zahanati, kila kata ina kituo cha afya, kila wilaya ina hospitali yenye madaktari na vifaa na kila mkoa una hospitali ya rufani. Pia Serikali itajenga hospitali za rufani kubwa za Kanda ya Kusini, Kanda ya Kati na Kandaa ya Magharibi. Bohari kubwa za kisasa za dawa zitajengwa Tanga, Tabora, Dar es Salaam na Mtwara.
Elimu ya msingi na sekondari, kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure kuanzia mwezi Januari 2016. Serikali itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi. Pi itahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu na madawati.

Mahitaji ya fedha ni makubwa
Mipango na sera za Rais Magufuli na Ilani ya Uchaguzi ya CCM inahitaji matumizi makubwa ya fedha. Mapato ya Serikali ya mwaka 2014/15 yalikuwa Sh10,507 bilioni sawa na dola za Marekani 5.2 bilioni. Pamoja na Rais Magufuli kujiwekea lengo la kuongeza mapato ya serikali na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima bado mahitaji ya fedha ya kutekeleza ahadi zake na Ilani ya uchaguzi ya CCM ni makubwa. Ni muhimu kwa Rais kujiwekea vipaumbele vinavyowezwa kutekelezwa katika miaka mitano ijayo.
Source: Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment