Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeifunga baa maarufu ya Maryland ya jijini Dar es Salaam kwa madai ya kukwepa kulipa kodi inayokadiriwa kufikia Sh139 milioni.
Meneja wa baa hiyo, Yona Haule jana alithibitisha maofisa wa TRA kuifungia baa hiyo iliyopo Mwenge Manispaa ya Kinondoni tangu Novemba 30 baada ya kudai wamegundua kuwa hakukuwa na makato ya kodi tangu mwaka 2011.
Hata hivyo, alisema baa hiyo ina mashine ya kielektroniki ya kulipia stakabadhi (EFD) na wamekuwa wakikatwa kodi kwa kipindi chote walichokuwa wakifanya biashara.
“Tuna mashine na kodi zinakatwa, lakini wanasema haikuwa ikikatwa, naona kuna walakini hata hivyo, mhasibu wetu anaendelea kujadiliana nao,” alisema.
Mkurugenzi wa Umma wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema kufungwa kwa baa hiyo ni kazi ambayo itakuwa endelevu nchi nzima kusaka wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi.
“Hilo zoezi ni la nchi nzima, kila mfanyabiashara ambaye anakwepa kodi atafikiwa, hata kesho tutaendelea na mchakato huo,” alisema Kayombo.
Vilevile Novemba 25, TRA walilifunga duka la simu la Sapna lililoko maeneo ya Posta Mpya kwa kudaiwa kodi.
Kayombo alisema tangu Novemba Mosi, TRA imeokoa Sh1.9 bilioni kupitia ukaguzi huo huku wafanyabiashara 10 wakinaswa kwa kukwepa kulipa kodi ya Sh6.7 bilioni katika operesheni iliyofanyika jana pekee.
“Kuna utaratibu wa muda wa kulipia deni la kodi, watakuwa salama kama wakieleza jinsi gani watapunguza deni, vinginevyo tutataifisha mali zote,” alisema.
Operesheni hiyo pia iliyakumba mabasi ya Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), kwa kukamata baadhi ya mabasi kutokana na malimbikizo ya kodi.
0 comments:
Post a Comment