IMEANDIKWA NA HALIMA MLACHA.
RAIS John Magufuli ametangaza kiama kwa wafanyabiashara wote wenye tabia ya kukwepa kulipa kodi na kusisitiza kuwa kamwe Serikali yake ya Awamu ya Tano, haitovumilia kitendo hicho. Kutokana na hayo, Dk Magufuli ametoa siku saba kwa wafanyabiashara wote nchini waliokwepa kodi wakiwemo wale wa makontena takribani 349 yaliyopitishwa bandarini bila kulipa kodi, waende wakalipe kodi hiyo mara moja, vinginevyo sheria itafuata mkondo wake.
Aidha, amewatoa hofu wafanyabiashara wa sekta binafsi nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatambua mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi, hivyo watumie fursa za rasilimali zilizopo na kuwekeza kwa manufaa yao, lakini waweke kwanza uzalendo mbele kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla. Dk Magufuli aliyasema hayo wakati alipokutana na wafanyabiashara hao Ikulu, Dar es Salaam jana, ambako pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa Serikali yake imejipanga kuwatumikia Watanzania kwa kuhakikisha wananufaika na rasilimali za nchi.
Alisema si vyema kuhangaika kuficha makontena ambayo kiuhalisia si rahisi kuyaficha, kwani kwa namna yoyote yataonekana. “Jamani kontena si kama sindano, hebu jitokezeni mkalipe kodi zetu, maana kuyakimbiza hayo makontena yatakuja kuwaangukia na kuwakandamiza bure,” alisema Dk Magufuli.
Alisisitiza kuwa endapo mfanyabiashara yeyote aliyekwepa kodi, atakiuka kujitokeza na kuilipa ndani ya siku saba zilizotolewa, baada ya hapo Serikali haitokuwa na huruma na mtu yeyote na sheria itafuata mkondo wake. Alisema kutokana na ukwepaji kodi, wizi na ubadhirifu wa baadhi ya watendaji, Serikali imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa fedha kiasi cha matumizi mengine kuchelewa au kushindwa kufanyika.
“Nilipoingia Ikulu nimekuta kwa takribani miezi sita tangu bajeti ya mwaka 2015/2016 ipitishwe, hakuna hata shilingi moja ya fedha za maendeleo iliyopelekwa kwa wizara yoyote, mwezi huu ndio tumetoa shilingi bilioni 120 za maendeleo hata fedha za matumizi ya kawaida (OC) ni tatizo,” alisisitiza.
Alisema kwa sasa kampeni za uchaguzi zimeisha na sasa Serikali yake imejipanga kuwatumikia wananchi ; na itaendelea kuchukua hatua dhidi ya wabadhirifu na wala rushwa, si kwa sababu ya kiburi, bali ni kwa ajili ya Watanzania. Alisema atashirikiana na sekta binafsi, kufanyakazi na ndio maana alijiepusha na mchango wowote wa wafanyabiashara kwenye kampeni zake za siasa.
“Na kama yupo mfanyabiashara aliyenipa hata shilingi mbili aseme, nilikwepa hili nikijua kuwa mimi ninachotaka hapa ni kazi tu,” alitanabaisha Rais. Aliwataka wafanyabiashara hao kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa, lakini pia kuzingatia maslahi ya Watanzania. “Yaacheni ya Kaizari yaende kwa Kaizari, kuna watu hapa wanatumia vibaya fedha zao kuwakandamiza wananchi nawajua na ninajua mnawajua,” alieleza.
Alisema Serikali yake haitovumilia mtu yeyote, anayetumia uwezo wake wa fedha ku wakandamiza wengine kwa maslahi yake na kuwatahadharisha wale wote wanaochukua maeneo ya wazi ya umma kwa manufaa yao. “Nawaambia wazi hili katika Serikali yangu halitavumiliwa,” alieleza. Aidha, Dk Magufuli aliwataka wafanyabiashara hao, kuwafichua watendaji wowote walioko chini ya uongozi wa Rais huyo, watakaobainika kuwakwamisha au kuwachelewesha kwa namna yoyote katika majukumu yao.
Alisema Serikali yake imejipanga kuhakikisha inatengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuijengea uwezo sekta binafsi ambapo itahakikisha inaaangalia uwezekano wa kuondoa vikwazo vya uwekezaji nchini, ikiwemo utitiri wa kodi unaolalamikiwa. Alikiri kutambua kuwa kuna baadhi ya maeneo yanahitaji kuangaliwa kwa macho mawili na kupunguziwa idadi ya ushuru ili kumuwezesha mkulima kuinua kipato chake, lakini mlaji naye kupata bidhaa husika kwa gharama nafuu.
“Nilipokuwa mikoa ya Kagera na Kilimanjaro katika kipindi cha kampeni za uchaguzi, nilishuhudia zao la kahawa kuwa linalipishwa kodi zaidi ya 26, sasa hali hii hasa Kagera iliwalazimisha wakulima kupitisha kwa njia za panya zao hilo hadi Uganda, ambako hakuna kodi kama za kwetu. Haya tutayafanyia kazi,” alisema. Pamoja na hayo, Dk Magufuli alisema Serikali na sekta binafsi ni vyombo ambavyo vinategemeana, hivyo kuna haja ya kufanyakazi kwa pamoja na kuhakikisha utajiri uliopo nchini unanufaisha Watanzania.
Aliwataka wafanyabiashara hao, kuangalia maeneo nyeti yanayowezekana kuwekezwa na wazalendo, jambo litakaloungwa mkono na Serikali. “Naomba niseme ukweli haiingii akilini mfano sekta ya madini eti nchi inayoongoza duniani kuuza madini ya tanzanite iwe India ikifuatiwa na Kenya wakati wazalishaji wa madini hayo ni Tanzania…
“Nilitegema sekta binafsi mngekaa na kujadiliana namna ya kuondoa hali hii, kwa nini mruhusu wale watu wachimbe waondoke na mchanga kwenda kuuchuja huko kwani nyie hamuwezi kuchuja, nitafurahi sana nikisikia mfanyabiashara hapa amefungua kiwanda cha kuchuja mchanga wa madini,” alisisitiza.
Alisema pia zipo fursa nyingi, ikiwemo kuanzisha na kufufua viwanda vilivyopo ili kuongeza tija ya bidhaa nchini kutokana na ukweli kuwa nchi ilikuwa na viwanda vingi, lakini kwa sasa vingi vimekufa na kugeuzwa maghala ya kufugia mbuzi.
Pia aliwataka wafanyabiashara hao hasa wazalendo kujitokeza na kuwekeza katika rasilimali mbalimbali ikiwemo gesi bila woga kwani Serikali ipo kwa ajili ya kuwasaidia. “Hakuna haja ya kupiga kelele kuwa eti hamuwezi, hakuna Serikali yoyote duniani inayofanikiwa bila kusaidia watu wake, sasa hata nyinyi kama mnaweza kuwekeza kwenye gesi wekezeni,” alieleza.
Alisema kwa muda mrefu amekuwa akipiga kelele kutoka moyoni kwamba nchi imegeuzwa kuwa shamba la bibi, sasa ni wakati wa kuondokana na matatizo hayo na badala yake Serikali yake inatoa fursa kwa wafanyabiashara nchini kuwa mstari wa mbele kushika uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi alisema taasisi hiyo imeridhishwa na kuwa na imani na utendaji wa Dk Magufuli hasa kwa kuyashughulikia ipasavyo masuala yanayokwaza uchumi wa Tanzania.
Alisema taasisi hiyo inatambua kuwa adui mkubwa wa maendeleo ni rushwa na kwa bahati mbaya wapo pia baadhi ya wafanyabiashara wanaojikita katika vitendo hivyo, na hivyo kumtaka Dk Magufuli kuifanyia marekebisho Sheria ya Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007 ili Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) iwe na meno.
“TSPF tunatambua mchango wako kwa kipindi kifupi ulioonyesha dhidi ya rushwa na tunakuunga mkono katika vita hii, na kusisitiza juu ya uanzishwaji wa mahakama za kushughulikia kesi za ufisadi.
Lakini pia tunatambua kuwa ili nchi iendelee lazima ilipe kodi, tunakuhakikishia hili tutalitimiza kikamilifu,” alisema Mengi. Alitaja changamoto zinazoikabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na utitiri wa kodi, ubovu wa miundombinu hasa ya reli na barabara, uhaba wa maji na umeme, utendaji duni na bandari, rushwa na ubadhirifu, kasi ndogo ya utekelezaji wa maamuzi ya kisiasa na kutokuwepo kwa uwazi katika eneo la ununuzi wa umma.
Source: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment