UTEUZI WA MAWAZIRI WENGI, WAPONGEZWA

WATU wa kada mbalimbali wamepongeza uamuzi wa Rais John Magufuli kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri kwamba hatua hiyo itasaidia kuwa na watu wachache watakaofanya kazi ya kusaidia kuinua uchumi wa nchi. Aidha, uteuzi wake wa Baraza la Mawaziri umewagusa viongozi wa taasisi mbalimbali na wasomi nchini ambao wamelitaja baraza hilo kuwa ni la viwango lililozingatia weledi.
Kwa upande wao, viongozi wa dini wamempongeza Dk Magufuli kwa uteuzi wa Baraza la Mawaziri ambalo wamesema ni dogo lenye weledi lililobeba vijana wachapakazi. Jana, Dk Magufuli alitangaza Baraza jipya la Mawaziri ambalo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, ndio baraza lenye idadi ndogo ya wizara na mawaziri wake. Lina wizara 18, zenye mawaziri 19, ambapo kati ya hao, wizara nne hazijapata mawaziri, huku idadi ya manaibu waziri ikiwa ni 15.
Wangwe apongeza idadi ndogo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini (REPOA), Profesa Samuel Wangwe, amesifu Rais kupunguza mawaziri kwa maelezo kuwa mawaziri ni watu wa kusimamia sera tu na watendaji wakubwa ni makatibu wakuu, wakurugenzi na watumishi wengine. Kuhusu mawaziri wa zamani kurejeshwa kwenye baraza, Profesa Wangwe alisema mawaziri waliorudi ni wazuri na wana kasi kubwa na ndio maana Dk Magufuli amewaamini na kuwateua wamsaidie kufanya kazi.
“Watu wanabadilika kulingana na mawaziri, wengine ni watendaji wazuri ila inategemea na kiongozi wao,” alisema Profesa Wangwe na kuongeza “Sio suala la kuangalia ku-balance (kuweka uwiano) mikoa, baraza hili ni la kazi.”
Naye Mwanaharakati wa Masuala ya Haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa amepongeza hatua ya Dk Magufuli ya kupunguza Baraza la Mawaziri kwa maelezo kuwa nchi haiwezi kutegemea wanasiasa kufanya kazi, bali wanaotakiwa kufanya hivyo ni watendaji walioko kwenye wizara ambao wamedumu humo kwa muda mrefu.
“Ukiangalia wanasiasa hawa wanakaa muda mfupi wanaondoka kwa kubadilishwa au kufukuzwa, hivyo Dk Magufuli ana haki ya kupunguza baraza lake,” alisema Olengurumwa na kuongeza kuwa, wananchi walitarajia angekuja na sura nyingi mpya, lakini badala yake amerejesha nusu ya baraza la serikali iliyopita jambo ambalo alisema linampa wasiwasi kama wanaweza kumudu kasi ya Rais huyo.
Kuhusu wizara nne kutokuwa na mawaziri, Olengurumwa alisema ni jambo jema kwa kuwa wizara hizo ni nyeti zinahitaji kuwa na watu makini, kwani ndio uti wa mgongo wa nchi.
Bana:
Rais amezingatia weledi, uzoefu Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Siasa, Dk Benson Bana alisema Rais ameteua baraza hilo kwa kuzingatia weledi wa kila waziri kwa maana ya uzoefu na maarifa.
Aidha, alisema amevutiwa na kitendo cha Rais Magufuli kuiweka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) chini ya ofisi yake, kwa kuwa wizara hiyo ndio inayogusa wananchi kwa maana ya huduma na ulinzi na usalama wao.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Amani kwa Waislamu ya Islamic Peace Foundation (TIPF), Sadiki Godigodi amepongeza hatua ya Rais kupunguza idadi kwa kiasi kikubwa ya mawaziri, kwani ameonesha kujali maslahi ya nchi.
Alisema kwa sura chache za zamani zilizorudi anaamini amefanya uchambuzi wa kina katika utendaji wao, hivyo kutaka kuendana na kasi ya Rais huyo mpya ili wasimuangushe, kwani amewaamini kuwapa nafasi hizo.
Alisema kuacha kuteua mawaziri wa wizara nyeti kama Fedha, Uchukuzi na Ujenzi, Maliasili na Utalii na Elimu ni kuonesha asivyokuwa na masihara katika masuala nyeti na kutaka atakaowateua kuwa na kasi zaidi kama ilivyokuwa enzi zake akiwa Waziri wa Ujenzi.
Tucta yamsifu kwa umakini Naye Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alisema amefurahi kwa baadhi ya mawaziri watendaji kurudi kwa lengo la kumsaidia Rais kwenda na kasi yake akiwemo William Lukuvi aliyekuwa ameanza vizuri kazi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Alisema ameonesha jinsi alivyo makini kwa kuteua baraza dogo, lenye watu makini na Baraza la Mawaziri aliloteua litamsaidia kupeleka mbele nchi na iwapo angekosea kazi aliyofanya kwa muda mchache isingekuwa na maana. Kilaini avutiwa na vijana Akizungumzia uteuzi huo, Askofu wa Kanisa Katoliki, Methodius Kilaini alisema baraza aliloliteua Rais John Magufuli ni zuri na dogo ambalo limebeba vijana wengi ambao wataendana na kasi yake.
Alisema mawaziri waliokuwepo katika Serikali ya Awamu ya Nne na sasa hawakuchaguliwa hawakuwa wabaya, lakini wengi wao wasingeweza kuendana na kazi ya kiongozi huyo ambaye ameonekana kutaka kushirikiana na watu wenye kasi. ‘Mseto’ wamvutia Shehe wa Dar Naye Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema Baraza la Mawaziri lililoteuliwa na Rais Magufuli ni la kipekee ambalo kila Mtanzania anapaswa kupongeza hatua hiyo.
Alisema kitendo cha kuchanganya vijana ambao ni wachapakazi na mawaziri wazoefu ambao miaka yote ya uongozi wao, utendaji wao umeonekana kuwa mzuri utasaidia kuendana na kasi ya Rais Magufuli. “Mchanganyiko huu wa vijana wachapakazi na waadilifu pamoja na ambao wameshawahi kuwa mawaziri ni wazi kuwa watafanyakazi kuendana na kaulimbiu ya Rais Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu.’
“Kuanzia viongozi wakubwa wa zamani na hawa vijana wapya wote wako vizuri wanaonekana ni wachapakazi, kikubwa ni kuwapa ushirikiano lakini pia tuwaombee ili waweze kututumikia vizuri sisi wananchi,” alisema Shehe Alhad. Alisema uteuzi huo wa baraza hilo dogo la mawaziri unapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania ili lifikie malengo yaliyowekwa na Rais ya kuwatumikia wananchi ipasavyo.
Baregu:
Lingebanwa zaidi Naye aliyekuwa Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Profesa Mwesiga Baregu alisema Baraza lililotangazwa jana ni dogo kuliko lile lililopita, lakini lingeweza kuwa dogo zaidi na lenye tija.
Alitolea mfano wa Marekani kuwa ina Baraza la Mawaziri 15 na China 20 na kwamba hata katika mapendekezo ya Tume hiyo katika Rasimu ya Pili ya Katiba ilieleza umuhimu wa kuwa na baraza lenye watu sio chini ya 15.
Alisema kikubwa ni kufahamika kuwa waziri sio sehemu ya mgawo wa kula, badala yake kutambulika kuwa ni kazi. Kuhusu waliotajwa katika Baraza la Mawaziri, Profesa Baregu alisema kuna waliotajwa akitolea mfano wa Profesa Sospeter Muhongo ambaye alikuwa na mtazamo hasi jambo lisiloweka wazi ni ujenzi wa taswira ipi alionao.
Alisema baraza hilo limeibua maswali mengi zaidi ya majibu hasa kutokuwa na semina elekezi ambayo kwa hilo, haioneshi baraza hilo litawajibika kwa Rais ama litawajibika kwa umoja kama timu shirikishi kwa Watanzania.
Dodoma yamshangilia Muhongo Mkoani Dodoma, wakazi wake wamesifu uteuzi huo wakisema umefanyika baada ya kufanyika utafiti wa watu wanaoweza kwenda na kasi ya Rais, na wamefurahishwa na uteuzi wa Profesa Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Mhadhiri wa Utafiti, Mitaala na Ufundishaji wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John (St John’s), Dk Michael Msendekwa alisema uteuzi umefanikiwa kutokana na kufanyika kwa utafiti wa kina. Alisema uteuzi huo ni wa kitafiti zaidi, kwani kuna wizara zimeachwa wazi, ikimaanisha Rais yuko makini kutafuta watu wanaofanya kazi kweli.
Alisema anataka kuhakikisha walioteuliwa wanakuwa mfano bora wa utendaji. Alisema uteuzi wa Muhongo ni mzuri, kwani ni mchapakazi na kwa uteuzi huo amepatia licha ya kipindi kilichopita mambo ya chuki na siasa yaliingilia kumtoa.
Naye mkazi wa Zuzu, Amos Magimba alisema amefurahishwa na uteuzi huo hasa Profesa Muhongo kwani anaamini sasa vijiji vyote vitapata umeme na kwamba baraza hilo ni la kisayansi zaidi na kuwataka walioteuliwa wakachape kazi ili kupunguza changamoto ya umasikini nchini. Mkazi wa Viwandani, Mary Aloyce alisema amefurahishwa na uteuzi huo, akisema haukuwa wa kiupendeleo.
Imeandikwa na Halima Mlacha, Shadrack Sagati, Theopista Nsanzugwanko, Sophia Mwambe, Katuma Masamba, Lucy Lyatuu (Dar), na Sifa Lubasi, Dodoma.
Source: Habari Leo
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment