WASALITI WATADHIBITIWA - DR. TULIA

Dr. Tulia Ackson
Katika toleo lililopita tuliwaletea mahojiano kati ya Naibu Spika Dk. Tulia Ackson na Wandishi wetu DEUS BUGAYWA na JOHN DANIEL, endelea na sehemu ya mwisho ya mahojiano hayo.

Raia Mwema: Mchakato wako ndani ya chama ulikuwaje?
Hiyo ni tofauti na vyama vingine ambavyo mtu leo anapewa kadi kesho anapewa ubunge. Leo amekwenda kwenye mkutano akaonwa huyu anaweza kufaa, anapewa. Wapo wabunge humu wamepata kwa namna hiyo.
Lakini kama unafuatilia, hata Viti Maalumu vya CCM ni mchakato mrefu mpaka mtu kufika hapo. Anagombea na kupigiwa kura kwenye mlolongo mrefu. Lakini huku kwingine mtu tu anakuja na majina yake mfukoni yanawekwa pale.
Kwa hiyo binafsi nisingependa kuendeleza hizo hoja kwa sababu najua mtu anyesema ni kwamba haelewi anachokisema. Hata akisema nimebebwa, labda aseme sina sifa, hapo ndiyo aniambie nimebebwa.
Anayesema atakuwa ameamua tu kwa sababu hajui au anajifurahisha. Ni kama sasa hivi kuna picha nyingi zinatumwa kwenye mtandao kwamba ni mimi, sijui labda kwa sababu hao watu ni weusi lakini si mimi. Watu wanakaa mapozi ya aina tofauti kwamba huyu ni nani alipokuwa anasoma wapi lakini its simply not me. Sasa kwa kuwa wanaona mtu mweusi basi wakaona ni lazima ni mwenyewe lakini si mimi.
Raia Mwema: Rais Magufuli ana ari kubwa ya kutaka kukabili kero za Watanzania, unadhani Bunge hili liko tayari kumsaidia kutimiza azma hiyo?

Dk. Tulia: Mimi nadhani litamsaidia. Kwa sababu wabunge hawa, wengi ni wapya na kuna wakongwe wengi hawajarudi. Matarajio hayo ya wananchi si tu kwa serikali lakini pia ni kwa wawakilishi wao waliowatuma. Wanajua kabisa kwamba kumfikia Rais wamueleze matatizo yao ni ngumu, lakini wanatumia mwakilishi wao ayafikishe. Mwakilishi amesikia mwelekeo wa serikali kuhusu afya, elimu, na kuhusu mambo yote, mbunge huyu huyu atasimama asubiri kwenye afya bajeti inasemaje, inanifikia au hainifikii.
Kwa hiyo, ninaamini usimamizi wa shughuli za serikali utakuwa ni mkubwa safari hii. Rais ameeleza mambo mengi. Bunge kazi yake ni kusimamia, je, serikali imefanya?
Kwa sababu wamemsikia aliyoahidi kwa wabunge, naamini wabunge wamemsikia Rais na aliyoyasema watayatekeleza kwa maana ya kwamba wataisimamia serikali ili ifanye aliyoahidi. Kwa hiyo ninaamini Bunge hili litajiweka vizuri kwa ajili ya zile ahadi alizoahidi.

Raia Mwema: Rais ameonyesha matumizi yasiyo ya maana kwa maslahi ya Taifa na wananchi. Bunge ni taasisi aliyoitaja kuongoza kwa matumizi ya aina hiyo, utalisaidiaje Bunge lisiingie tena katika matumizi ya aina hiyo?

Dk. Tulia: Rais amelieleza jambo hilo vizuri sana. Kuna zile safari za kujifunza na kuna safari za matibabu. Tukishaisimamia serikali, tukaboresha afya, safari za kumpeleka mbunge kwenda kutibiwa nje maana yake hazitakuwapo. Kwa hiyo, matumizi yatapungua. Safari za kwenda kujifunza nje, Rais si kwamba kazikataza. Amesema watu watajifunza ndani na nje, cha kuangalia ni huyu kile anachoenda kujifunza hawezi kujifunza hapa? Kile ambacho hakiwezekani kujifunza hapa wabunge bado wataendelea kwenda, kile kinachowezekana kujifunza hapa basi wataalamu wataletwa.
Niseme kwa ujumla kwamba Rais ametoa mwelekeo wa matumizi ya fedha. Na matumizi ya fedha sasa hivi yako kisheria. Huwezi kufanya matumizi nje ya bajeti. Kwa hiyo mambo yote ambayo ulikuwa umeyabajeti ndivyo utakavyofanya matumizi.
Ni imani yangu kwamba bajeti ya mwaka ujao wa fedha itatoa huo mwelekeo wa namna ya kuondoa matumizi yasiyostahili. Nimetoa mfano katika maeneo ya afya na mafunzo, kama tutaweza kuleta mtaalamu hapa kwa mambo ambayo hatuna utaalamu basi ataletwa. Ametushauri vizuri sana na sisi tutakaa haya mambo tutayaangalia tutayaweka vipi.
Lakini kwa yale ambayo wabunge wetu waende kujifunza huko uzoefu basi tutawapeleka. Maana hatutaweza kuubeba ule uzoefu kuuleta hapa. Lakini kimsingi ni kwamba wazo kubwa katika haya yote ni kupunguza matumizi ili fedha zielekezwe maeneo ya maendeleo, lakini pia tukumbuke maendeleo yanakuja kwa wale watendaji kujua cha kufanya.
Mwanzoni nilisema wabunge wengi ni wageni, ili uende kujifunza mabunge mengine yanafanyaje, ili uweze kujua hayo ni lazima uone wanajadili vipi, sasa huwezi kuleta wabunge wale huku ili wakuelekeze, kwa hiyo inabidi tu uende ukaone wao wanajadili vipi. Katika mazingira hayo safari zitakuwa ni za lazima lakini pale ambapo ni kujifunza kwamba kanuni hizi zinasemaje, huhitaji mtu kutoka nje kukuelekeza, hizi tutajifunzia hapa hapa.

Raia Mwema: Kumekuwa na mazoea ya kutunga sheria na baada ya muda mfupi zinarejeshwa tena bungeni kufanyiwa marekebisho. Utalisaidiaje Bunge kutunga sheria ambazo zinaishi muda mrefu bila kulazimika kubadilishwa mara kwa mara?

Dk. Tulia: Kimsingi marekebisho ya sheria yanatokea siku zote na sababu zake zipo, moja inaweza kuwa ni hiyo, kwamba wakati wa kutunga kuna jambo hawakuliona vizuri au waliliona kwa namna tofauti lakini baadaye utekelezaji wa sheria umeleta shida. Jingine ni sheria kubadilishwa kutokana na mazingira. Pengine mazingira yamebadilika, lazima sheria iendane na mabadiliko hayo, jambo ambalo halikuwa kosa mwaka jana mwaka huu unaweza kulifanya kuwa kosa kwa sababu ya mazingira yaliyotokea.
Kwa mfano, kuna mambo mengi yanasemwa kuhusu ile Sheria ya Makosa ya Mtandao. Kuna mambo ambayo unaweza kusema hapa kidogo utekelezaji wake ni shida, lakini yako mazuri mle, kwa hiyo huwezi kusema sheria yote ni mbaya.
Inapotokea katika utekelezaji kwamba hili jambo litiliwe mkazo, hili liondolewe kabisa kwa sababu wananchi wanaonewa, linaondolewa. Kwa hiyo mabadiliko ya sheria katika hii tasnia ya sheria huwa ni ya kawaida sana. Hata Katiba, ndiyo maana huwa inabadilishwa muda kwa muda, kutegemea jambo lenyewe mnataka kubadilisha kwa sababu gani.
Mfano mwingine ni huo aliosema Rais kuhusu Sheria ya Manunuzi. Wakati ikitengenezwa kulikuwa na sababu za msingi za kuifanya iwe hivyo ilivyo. Lakini katika utekelezaji wake inaonekana kuna vifungu vinaleta matatizo zaidi na kufanya matumizi ya fedha yawe makubwa zaidi kuliko kupunguza.
Mazingira kama hayo si kwamba Bunge lililopita lilikuwa halijaona mambo kama hayo. Ni kwamba wakati ikitengenezwa ilikuwa sawa sawa lakini wakati wa utekelezaji inaonaekana ni lazima mambo kadhaa yabadilishwe.

Raia Mwema: Katika kutimiza vipaumbele vya Rais kunaweza kutokea usaliti, unadhani Bunge litamsaidia vipi hali hiyo ikianza kutokea?

Dk. Tulia: Rais ameahidi kupasua majipu, Bunge litamsaidia kwa maana ya kushirikiana naye na kama alivyosema, ametaja sheria chache, lakini ziko sheria nyingi zitakazopaswa kubadilishwa ama nyingine kutungwa ili kuweza kuyafanya yale yote aliyoyasema, si yote kwamba sheria ipo na itaunga mkono namna yeye anavyotaka kwenda.
Kwa hiyo sisi tutamuunga mkono kwa kuweka mazingira ambayo serikali inaweza kuyafanyia kazi kwa sababu serikali haiwezi kufanya jambo ambalo halijatungiwa sheria na Bunge. Lakini pia tutamsaidia kwa maana ya kwamba vile vyombo alivyosema ataanzisha, kwa mfano ametaja Mahakama ya Mafisadi, kwa hiyo mswada wa sheria inabidi uje, sisi tutamsadia kuitengeneza hiyo sheria kuwa vizuri ili wale watu wakamatwe.
Umeuliza kuhusu usaliti mimi ningependa kuamini kwamba watu wataangalia mwelekeo wa Rais ni upi, kwa hiyo ule usaliti wao lazima tu utadhibitiwa. Naamini watamwelewa Rais na watafanya yale ambayo ameagiza. Kama mtu anajishughulisha na dawa za kulevya ataacha kwa sababu Rais yuko serious, kama mtu anafanya ufisadi ataacha, kwa sababu katika hali ya kawaida hutegemei kwamba Mkuu wa nchi anatoa maagizo halafu hayo maagizo hayatafuatwa.
Lakini kama mtu atakwenda kinyume basi adhabu ya msaliti itajulikana. Sheria ipo. Watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria, watapelekwa mahakamani, wengine watafungwa, sidhani kama kuna mtu atakuwa amejipanga mahali anasubiri yeye afungwe.

Raia Mwema: Dk. Tulia atakuwa Naibu Spika wa aina gani?

Dk. Tulia: Kazi ya Naibu Spika ni kumsaidia Spika kuliongoza Bunge katika vikao vyake na kutimiza wajibu wake kwa hivyo, huyu Tulia atakachofanya ni kusaidiana na Spika kuendesha Bunge kwa mujibu wa kanuni, sheria na Katiba ili kwanza kutimiza yale ambayo Bunge ni kazi yake.
Unajua yako mazingira ya Bunge kufikiri linaweza kuwa Mahakama na linaweza kuwa Serikali. Katiba imeweka mipaka ya mihimili ili kila mhimili ufanye kazi yake.
Kwa hiyo ile kazi ambayo kikatiba ni ya Bunge ndiyo hiyo nitalisaidia Bunge kufanya kazi nikimsaidia Spika. Kazi ambayo siyo ya Bunge nitakachofanya ni kuwakumbusha wabunge hilo tunalofanya tunaweza kujadili kama mtu mwingine anavyojadili lakini kama wabunge shughuli yetu kwenye hili ni hii kwa sababu Katiba inatutaka tufanye hili na siyo lile.
Ninaamini hili litakuwa Bunge la kufuata sheria kanuni na taratibu likiheshimu mihimili mingine ya Dola.

Raia Mwema: Hiyo ndiyo kusema Dk. Tulia atakuwa Naibu Spika mkali sana, wa wastani, mpole au wa namna gani hasa?

Dk. Tulia: Kusema ukweli nadhani yote hayo uliyoyataja yatakuwapo kulingana na mazingira yatakavyokuwa. Siwezi kusema nitakuwa mpole ikiwa mtu atakuwa amekaidi kufanya yale ambayo sheria inataka, lakini pia sitaweza kuwa mkali kama hakuna sababu ya kuwa mkali, sasa unamkalipia nani.
Niseme sisi wote ni binadamu ninachomuomba Mwenyezi Mungu ni kwamba anisaidie nisiwe na hasira wakati wa kufanya maamuzi, niweze kufanya haki kwa kila mbunge, kwa sababu siyo jambo jema mtu akifanya kosa unamwadhibu mwingine akafanya kosa hilo hilo unamwacha, hilo linaleta shida. Natamani niwe Naibu Spika atakayeweza kutenda haki kwa wabunge wote.

Raia Mwema: Umri wako wa miaka 39 na majukumu uliyonayo, mtu anajiuliza umevukaje vikwazo vyote vikiwemo vya unyanyasaji wa kijinsia, mpaka kufikia nafasi hiyo, vijana wanaweza kujifunza kitu gani kutoka kwako?

Dk. Tulia: Kuna mambo mawili. La kwanza mimi naamini katika Mungu. Kwa sababu ya imani hiyo huwa naamini kwamba Mungu ameweka mwisho wa kila mwanadamu. Njia ya kufikia ule mwisho pia huwa anaitengeneza.
La pili ni ile njia anayoiendea huyu mwanadamu kufikia njia aliyowekewa na Mungu, ni bidii katika kazi. Si kwamba watu wengine ambao hawatapata fursa ya kufika nafasi hii kwamba hawafanyi bidii, si maelezo ninayotaka kutoa.
Ninachotaka kusema ni kwamba katika hali ya kawaida ninaweza kusema labda mimi nina bahati. Kwa sababu wapo watu wengi ambao wamefanya bidii sana katika mambo wanayoyafanya lakini hawajafika pale nilipo.
Mambo mawili haya nimeyaweka pamoja kwa sababu kule mwisho ili uweze kufika na ile njia unayopita inahitaji bidii, siyo kila mtu atakuwa amewekewa njia kama ya kwangu, kwa sababu Naibu Spika kwa miaka mitano atakuwepo mmoja tu, kwa hiyo hamuwezi kuwa wote mmewekewa hiyo njia kwa kipindi hicho.
Ukiwa na imani kwa Mungu katika hilo hilo unalolifanya ukifanya bidii utafika kule ulikopangiwa kwenda. Pengine si katika umri wangu lakini mimi naamini kwa bidii tu utafika.
Niseme kwa vijana na wengine ambao ninaweza kuwa inspire, cha kwanza wamuamini Mungu, lakini cha pili wafanye bidii katika chochote wanachofanya.

Raia Mwema: Uanachama wako kwa CCM umezua mjadala mkubwa, ni lini ulianza kuwa mwanachama wa chama hicho?

Dk. Tulia: Katiba inataja makundi matatu ambayo hayaruhusiwi kuwa kwenye vyama vya siasa. Unachoruhusiwa ni kitu kimoja tu, kushiriki kwenye uchaguzi kwa kupiga kura.
Kundi la kwanza ni majeshi yote, kundi la pili ni Mahakama, mahakimu na majaji wa ngazi zote hawaruhusiwi kuwa wanachama wa chama cha siasa. La tatu ni wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi.
Mimi kama Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Katiba haijanikataza. Kwa hiyo swali la kwamba nilijiunga lini na CCM halipo kwa kuwa Katiba hainikatazi. Lakini utasema ziko sheria za Utumishi wa Umma, sheria zile hakuna mahali zinanikataza mimi kuwa mwanachama wa chama chochote.
Kilichopo ni masharti ya mimi kushiriki siasa, wakati huo mimi kama mtumishi wa umma sipaswi kushiriki siasa (active participation) yaani kupanda majukwaani au kumnadi mgombea au kuzungumza mambo dhidi ya chama fulani, lakini sikatazwi kujiunga na chama.
Lingine ambalo kama mtumishi wa umma huruhusiwi kufanya ni kujishughulisha na siasa muda wa kazi, au kuvaa sare za chama katika muda wa kazi.

Raia Mwema: Katika njia yako kuelekea hapa ulipofika ni jambo gani ambalo unakumbuka lilikupa wakati mgumu na pengine hutalisahau kirahisi?

Dk. Tulia: Katika mambo ambayo yalikuwa magumu kwangu ni wakati nafanya shahada ya tatu ya Uzamivu (PhD). Hiyo ilinipa changamoto kwa sababu ndiyo nilikuwa nimeolewa halafu ikabidi niache mume na kwenda shule.
Katika hali ya kawaida huwa si jambo jepesi hivyo. Watu huwa wanakwenda kusoma shahada ya tatu akiwa hana familia kabisa au akiwa nayo anakuwa ameshazaa halafu anaanza kusoma tena.
Lilikuwa gumu si tu kwangu lakini pia kwa mume wangu na familia, lakini lilienda vizuri. Haya mengine ni changamoto za kawaida.

Raia Mwema: Watanzania wangepeda kujua maisha ya kijamii ya Naibu Spika wao yakoje na namna anavyoweka uwiano kati ya majukumu ya familia na kazi.

Dk. Tulia: Mimi ni mke wa mume mmoja. Tuna mtoto moja ana miaka minne. Namna ya kuweka uwiano wa majukumu ya kitaifa na familia ziko support structures (miundo saidizi), tunasaidina na baba yake kulea. Pamoja na kwamba anafanya kazi lakini muda mwingi anashiriki malezi ya mtoto kwa karibu.
Source: Raia Mwema
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment