Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa wa aina yake kwa sababu ya ushindani mkubwa uliokuwapo kati ya wagombea urais wawili, Dk John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa.
Pia, mwamko wa wananchi katika kushiriki mikutano ya kampeni na kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura viliongeza upekee wa uchaguzi huo.
Vyama vinne vya siasa viliungana chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kusimamisha mgombea mmoja wa urais, ubunge na udiwani katika maeneo mengi ya nchi licha ya kuwa kulikuwa na kutokuelewana kwa baadhi ya majimbo na kata.
Vyama vinavyounda umoja huyo ni Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD. Vyama hivyo vimeandika historia katika nchi hii tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi kwa kuanzisha muungano.
Hata hivyo, muungano huo unaelezwa kuwa umevinufaisha vyama husika kuweza kupata idadi kubwa ya wabunge na kuongeza kura za mgombea urais tofauti na kura walizopata wagombea wa upinzani katika chaguzi zilizopita.
Vilevile, vyama vingine kama NLD vimepata nafasi ya kujitambulisha kwa wananchi, huenda vikijipanga vizuri vitakuwa na nafasi nzuri ya kupata wawakilishi wengi bungeni. Chama cha NCCR Mageuzi kimeonekana kufanya vibaya katika uchaguzi huo kwa kupata mbunge mmoja tu kutoka idadi ya wabunge wanne waliokuwapo katika Bunge la Kumi.
Katibu Mkuu wa Ukawa, Dk George Kahangwa anasema Taifa kwa ujumla limenufaika na uwapo wa Ukawa kwa sababu kuna chombo ambacho kinapigania upatikanaji wa Katiba mpya ambayo ndiyo hitaji kubwa la Watanzania kwa sasa.
Vile vile, anasema kambi ya upinzani bungeni sasa inaundwa na vyama vitatu vya Chadema, CUF na NCCR Mageuzi. Anasema muungano huo bungeni utawafanya wapinzani wote kuwa kitu kimoja katika kukiwajibisha chama tawala na Serikali yake.
“Mafanikio yako mengi sana, vyama kufikia hatua ya kukubaliana na kusimamisha mgombea mmoja wa urais siyo jambo dogo. Sasa tuko kwenye mchakato wa kuunganisha vyama vote vinne na kuwa chama kimmoja cha siasa,” anasema Dk Kahangwa.
Anasema chama cha CUF kimenufaika zaidi na umoja wa Ukawa kwa kupata wabunge wengi ikilinganishwa na waliokuwapo wakati wa Bunge lililopita. Hata hivyo, anasema NCCR Mageuzi kimepoteza viti vyake vya ubunge hasa katika mkoa wa Kigoma kwa sababu ya chama cha ACT Wazalendo.
“Kuna sababu nyingi ya chama chetu kufanya vibaya, kwanza ni kuwapo kwa wagombea wengine katika maeneo ambayo sisi tulisimamisha wagombea, kwa hiyo tuligawana kura. Pia, ni kukubalika kwa wagombea wetu, baadhi yao walikuwa hawakubaliki kwa wananchi. Hicho ni kitu ambacho tumejifunza ni siyo kwamba kushindwa kwetu kumesababishwa na Ukawa,” anasema.
Anasisitiza kwamba Ukawa una muundo wake wa uongozi na yeye akiwa ndiyo katibu wake, una ofisi zake na sasa wako kwenye mchakato wa kuanzisha chama kimoja cha upinzani kitakachojumuisha vyama vyote vya vya Ukawa.
“Milango itakuwa wazi kwa vyama vingine vitakavyotaka kujiunga nasi, kwa sasa wataalamu wanaandaa andiko ikiwa ni sehemu ya kuunganisha vyama vyetu kisheria na kuwa chama kimoja. Hizo zote ni faida za umoja huu,” anasema.
Dk Kahangwa ambaye pia ni mwanachama wa NCCR Mageuzi, anasema vyama hivyo vikiungana na kuwa chama kimoja cha siasa, upinzani utakuwa na nguvu ya kuiondoa CCM madarakani na kuitawala nchi hii.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Sheweji Mketo anasema chama chake kimenufaika na Ukawa kwa sababu kimerudisha heshima yake kwa wapigakura. Anasema siasa zinabadilika na mabadiliko hayo ndiyo yamewafanya kujiunga na umoja wa Ukawa.
“Watu walianza kupoteza imani na chama chetu baada ya Chadema kutuita CCM ‘B’, lakini sasa wamejionea kwamba tunasimamia misingi utu na maslahi ya wananchi wetu ndiyo maana wametuchagua,” anasema.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, Mketo anasema wamefanikiwa kuongeza idadi ya wabunge na madiwani ukilinganisha na idadi ya awali. Anasema chama hicho sasa kina madiwani 279 kutoka 170 waliokuwapo na wabunge.
Mafanikio mengine ya CUF, anasema chama hicho kimefanikiwa kuongeza ruzuku yake kutokana na idadi kubwa ya wabunge waliyoipata. Anasema kigezo cha kupata ruzuku ni jumla ya kura za ubunge na idadi ya wabunge ambayo chama husika kimepata.
Mketo anasema watafanya tathmini ya uchaguzi uliopita ili kubaini mambo yaliyowafanya washindwe kufanya vizuri katika uchaguzi huo. Mkurugenzi huyo anaongeza kwamba Cuf iko tayari kuungana na vyama vingine vinavyounda Ukawa ili kuunda chama kimoja cha sheria.
Maoni ya wasomi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Benson Bana anasema Ukawa ilianzishwa kwa malengo tofauti na kitu ambacho wanakifanya sasa. Anasema walianza kwa kupigania Katiba mpya, lakini baadaye walibadilisha malengo na kutaka kushika madaraka.
Anasema kupitia umoja huo, CUF wamefanikiwa kupata viti vingi zaidi vya ubunge kwa upande wa Zanzibar, wakati Chadema kikizidi kung’ara upande wa Tanzania Bara kwa kupata wabunge wengi zaidi kuliko chama chochote cha upinzani.
“Pamoja na mafanikio machache waliyoyapata bado muungano wao ni flagile (dhaifu) kwa sababu walitoka kwenye mstari na kutaka kuchukua madaraka ya nchi,” anasema Dk Bana na kusisitiza kwamba Chadema kimekuwa na tofauti za kimsingi na CUF siku nyingi.
Dk Bana anaongeza kwamba ili kuwa na upinzani imara lazima vyama vya siasa viungane na kuwa chama kimoja kitakachoweza kupambana na nguvu ya CCM. Anasema Ukawa ikitengenezwa vizuri na kuwa chama cha siasa, utaweza kuwa na nguvu kubwa.
“Ninaamini katika umoja, sitashangaa siku za mbeleni CCM ikitafuta vyama vya kuungana navyo ili kujiiimarisha zaidi. Chadema kimevitumia vyama vingine kujikusanyia kura, ukiongeza na nguvu ya Lowassa basi mambo yao yamekwenda vizuri,” anasema.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), Gaudence Mpangala anasema umoja wa Ukawa ni mwanzo mzuri wa muungano wa vyama vya siasa ambao unaweza kuzaa matunda kama watasimamia misingi ya umoja wao.
Anasema nguvu waliyoionyesha wakati wa uchaguzi wa mwaka huu inatakiwa kuendelezwa kwa kuanzisha chama kimoja cha siasa kitakachokuwa na uwezo wa kuiwajibisha serikali na kutetea maslahi ya Umma.
“Ukawa imefanya vizuri katika uchaguzi wa mwaka huu, ninatarajia umoja wao utapiga hatua mbele kwa kuunda chama kimoja cha siasa. CCM bado ina nguvu, ili kukiondoa madarakani lazima wapinzani waungane na kuwa chama kimoja,” anasema.
Profesa Mpangala anaongeza kuwa vyama vyote vimenufaika na umoja huo kwa namna tofauti tofauti kwa sababu ya kusimamisha mgombea mmoja. Anasema hilo limewafanya wapinzani wasigane kura na kukiwezesha CCM kushinda kwa kupitia mwanya huo.
“Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa wa kipekee, lakini ninaamini uchaguzi ujao utakuwa mgumu zaidi endapo vyama vyote vya upinzani vitaungana na kuwa chama kimoja. Tena isiwe ni vyama vinne tu vya Ukawa bali iwe ni vyama vyote 22,” anasema Profesa Mpangala.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino (Sauti), Dk Charles Kitima anasema siasa za Tanzania sasa zimejenga utamaduni mzuri wa kuungana kwa vyama vya siasa ili kujiongezea nguvu ya kuleta mabadiliko.
Anasema vyama vimepata mafanikio kadhaa lakini sasa ni wakati kila chama kinatakiwa kujiimarisha ili kiwe na uwezo wa kusimama chenyewe na kuleta ushindani mkubwa katika siasa za Tanzania.
“Siungi mkono suala la vyama kuungana kwa sababu litaondoa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kila chama kijiimarishe chenyewe ili ushindani uendelee kuwapo siku zote. Tumeona baadhi ya vyama vimefunikwa ndani ya Ukawa vingine vikizidi kustawi,” anasema Dk Kitima.
0 comments:
Post a Comment