Wakati wanasiasa wengine wakiamini kuwa walimaliza Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 baada ya kupiga kura, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anasema anaamini siku hiyo ndiyo ilikuwa mwanzo wa maandalizi yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
“Mikakati yetu ACT miaka mitano ijayo ni kuongeza uwakilishi bungeni, kuongeza wabunge bungeni, kufanya kazi, kujenga chama, kuweka hoja mbele, kuhakikisha tunapata wawakilishi zaidi kwenye mabaraza ya kutunga sheria, kuongeza idadi ya wabunge na ya mabaraza ambayo tunayaongoza,” anasema.
Zitto ambaye ni mbunge pekee wa ACT anasema ajenda muhimu ya chama chake ni hifadhi ya jamii, miiko ya uongozi na kuongozwa na Azimio la Tabora.
Anasema kwa kuwa ACT ilikuwa na wagombea wengi vijana ambao pamoja na kutofanya vizuri kwa maana ya kushinda majimbo mengi kama ilivyo kwa vyama vya CUF na Chadema, wanajivunia mafanikio makubwa waliyoyapata.
“Licha ya uchanga wetu katika siasa, ACT tumepata mbunge mmoja, tumepata madiwani wa kutosha na kufanikiwa kuongoza Manispaa ya Kigoma, kwa ujumla tumepata asilimia 4.996 ya kura zote, kwetu huu ni mwanzo mzuri, ” anasema.
Anaongeza baada ya kufanya hayo, sasa nguvu zinaelekezwa katika kazi ya ujenzi wa chama kwa ngazi zote.
Mgawanyo wa majukumu
Akizungumzia mgawanyo wa majukumu ndani ya chama, Zitto anasema ACT kimeweka mikakati ya jinsi ya kuwatumia wanasiasa wake wenye uwezo na ambao hawakupata nafasi ya kurejea bungeni.
Anasema tayari wamempa jukumu aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali kujenga uwezo kwa madiwani wa chama hicho hususani katika maeneo ambayo wanaongoza manispaa.
“Machali yeye tumempa kazi ya kutusaidia kujenga uwezo wa madiwani wetu, na hasa wale ambao tunaongoza Manispaa kama Kigoma yeye atafanya kazi ya kuwasaidia na kuwajengea uwezo, na hivi karibuni tutamtangaza kuwa Katibu wa kamati kuu ya chama kama Mkurugenzi wa wabunge na madiwani, ” anasema Zitto.
Zitto anasema wanatumia fursa hiyo ya kuwajenga ili kukiwezesha chama hicho kupata vijana wapya kwenye siasa ili kuhakikisha ACT inaenda mbele na kuwa chama imara.
Mbunge mkiwa ndani ya Bunge
Zitto ni mbunge pekee ndani ya Bunge akitokea ACT na asiyefungamana na wabunge wa chama tawala na wale waliotokana na Ukawa.
Anasema kutokana na uzoefu alionao ndani ya Bunge kwa miaka takribani 10, hana wasiwasi wa kuwa mpweke ndani ya Bunge la 11.
“Mimi ni mbunge mzoefu, ukiwapanga wabunge kulingana na umri wao wa kuingia bungeni mimi ni mbunge wa 14, nina uzoefu na siasa za Bunge, najua ni namna gani nitaweza kuzicheza,” anasema
Anaongeza kuwa njia pekee na sahihi ya kufanya siasa za Bunge ni kuwa na agenda jambo ambalo yeye amekuwa muumini wake.
“Mtihani ninaouona ni kuwa kwa mara ya kwanza tuna Bunge ambalo lina chama tawala, kuna kambi ya upinzani, ukawa halafu kuna mbunge mmoja tu ambaye ni lazima awe huku au kule, hapa ni lazima kuwa na skills za kumudu changamoto hiyo” anaongeza.
Aomba kuongoza Kamati ya PAC
Je, ataomba tena kuongoza moja ya Kamati alizowahi kuziongoza, Zitto anasema ingawa anayewapanga wabunge katika kamati, lakini safari hii hakuomba kuwapo katika kamati yeyote kati ya zile alizowahi kuziongoza.
“Nimekuwa mwenyekiti wa kamati hizo kwa muda wa miaka minane, mitano kamati ya Mashirika ya Umma na mitatu Mwenyekiti wa PAC, sasa wananchi ni kama wanaihusisha Zitto na PAC, nimeona ni vema watu wengine wapewe nafasi hizo mimi nimeomba kuwapo katika kamati ya Bajeti na Nishati, ” anasema Zitto.
Anaongeza kuwa Spika wa Bunge ndiye anayeamua kupanga wabunge kwenye kamati, na kuwa atakwenda popote atakapopangwa na spika licha ya kutamani kuwepo miongoni mwa Kamati hizo mbili.
“Spika akiamua kunipeleka PAC nitaenda, lakini priority zangu ni mbili, Kamati ya Bajeti au ile ya Nishati na huko siwezi kugombea uenyekiti maana kwa mujibu wa Kanuni za Bunge wapinzani wamepewa kamati mbili tu PAC na kamati zingine wanapewa chama chenye wabunge wengi ambacho ni tawala,” anasema na kuongeza: “Tulifanikiwa, tuna Manispaa ya Kigoma, tuna mbunge, sasa ni miongoni mwa vyama vyenye wabunge, tumeingia kwenye TCD, awali hatukuwapo.”
Anasema kwa sasa hata wakienda kuzungumza na watu, wanakwenda wakiwa na nguvu kwasababu wamejitangaza na wana nguvu
Ruzuku ACT
Zitto anasema kwa mujibu wa sheria ili chama kiwe na sifa ya kupewa ruzuku kinapaswa kipate siyo chini ya asilimia 5 ya kura zote za wabunge.
Anasema ACT imepata kura 742 sawa na asilimia pata 4.996 nchi nzima kama kura za wabunge na kuwa wanasubiri chaguzi ndogo zilizosalia kuona endapo watafikia kiwango hicho ili wawe na sifa ya kuwa miongoni mwa vyama vinavyopata ruzuku nchini.
Uhusiano wake na Kafulila
Zitto anasema Bunge lijalo litawakosa waliokuwa wabunge vijana machachari kama David Kafulila ambaye alikuwa ana mchango mkubwa katika mijadala na uwezo wa kujenga hoja.
Anasema licha ya Kafulila kugombea ubunge kupitia chama tofauti na ACT, lakini haiondoi ukweli kuwa ni kijana mwenye uwezo mkubwa na ambaye angehitajika kuwapo katika Bunge la 11.
“Kilichotokea yeye aligombea na mimi niligombea… tumepishana kwenye siasa, approach yake ya siasa ni kupitia chama alichokuwapo, apoach yangu ni kwenye chama kipya ambacho alishiriki katika kukianzisha, lakini kama nilivyosema upepo wa Lowassa, ulikuwa ngumu kuukwepa, ” anasema.
0 comments:
Post a Comment