TRA YAWEKA REKODI YA SHS 1.4 TRILIONI DESEMBA

Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Kulia  ni Kaimu Kamishna wa Kodi za Ndani, Yussuf Salum. Picha na Omar Fungo 
By Fidelis Butahe na Colnely Joseph, Mwananchi
Dar es Salaam. Serikali ya Awamu ya Tano imekusanya ziada ya Sh900 bilioni kupitia kodi katika kipindi cha miezi miwili tangu aingie madarakani.
Wakati Novemba makusanyo hayo yalikuwa Sh1.3 trilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh400 bilioni, Desemba makusanyo hayo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yalifikia Sh1.4 trilioni sawa na ongezeko la Sh500 bilioni kutoka wastani wa makusanyo ya Sh900 bilioni zilizokuwa zinakusanywa kila mwezi na Serikali ya Awamu ya Nne.
Iwapo makusanyo hayo ya ziada ya Sh900 bilioni yangeelekezwa kwenye ununuzi wa magari ya wagonjwa, yangenunuliwa magari 3,000 kwa gharama ya Sh300 milioni kila moja na kuwezesha kila mkoa kupata magari 120.
Takwimu za ongezeko la Desemba zilitolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata ambaye alisema kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, mamlaka yake ilikuwa imekusanya wastani wa Sh6.4 trilioni ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 95.5 ya lengo la kukusanya Sh6.5 trilioni.
Kidata alisema sababu za ongezeko la makusanyo hayo ni kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuweka mifumo mizuri ya ufuatiliaji.
Katika hatua nyingine, Kidata alisema jumla ya Sh11.8 bilioni zimekusanywa kutoka kwa wafanyabiashara walioondosha makontena katika Bandari Kavu kinyume na taratibu za forodha.
Alisema kuwa makusanyo hayo yanajumuisha Sh5.3 bilioni kutoka kwa kampuni na wafanyabiashara 19 ambao wamemaliza kulipa kodi za makonteza yao na wengine 19 ambao wamelipa sehemu ya kodi wanayodaiwa.
Yafafanua madai ya Bakwata
Wakati huohuo; TRA imefafanua madai ya kuwapo upendeleo katika kutoa masharti ya ufuatiliaji wa misamaha ya kodi kwa taasisi zisizo za kiserikali na mashirika ya dini, ikisema unafanywa kwa kufuata taratibu na sheria.
Tamko la Kidata kwa vyombo vya habari limekuja kufuatia kauli iliyotolewa hivi karibuni na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), kuwa kumekuwapo na sintofahamu katika agizo la TRA lililowataka kupeleka taarifa kuhusu magari yaliyosamehewa kodi na matumizi yake ndani ya siku saba, likihoji iwapo agizo hilo lilitolewa pia kwa taasisi nyingine.
Kidata alisema Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania inaipa mamlaka hiyo kusimamia, kukagua na kuhakiki mapato ya Serikali na kuzuia aina yoyote ya ukwepaji wa kodi kwa maendeleo ya Taifa.
“Mamlaka inayo dhamana ya kusimamia kusiwepo na matumizi mabaya ya misamaha ya kodi ambayo hutolewa kwa mujibu wa sheria kifungu cha 5 (3) cha TRA,” alisema Kidata. Alisema TRA haina upendeleo na haibagui wala kulenga taasisi moja ya kidini.
Katika taarifa hiyo Kidata alisema kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2015, TRA iliwaandikia barua walipakodi 65 na katika wahusika hao kuna taasisi na mashirika ya dini ni 39.
Kidata alisema ukaguzi huo husaidia TRA kupata taarifa muhimu ili kuishauri Serikali namna bora ya kutoa misamaha kwa manufaa ya Taifa.
Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment