SERIKALI YAWASAKA WANAOISHI NCHINI KINYUME CHA SHERIA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yussuf
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yussuf Masauni akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Picha  na Said Khamis 
By Tumaini Msowoya, Mwananchi
Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani imeanza operesheni ya kuwasaka raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria ili warudishwe makwao.
Operesheni hiyo imeanza ikiwa zimepita siku chache tangu Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Anthony Mavunde kumuagiza kamishna wa kazi nchini kufuta vibali vya kazi vya muda kwa wageni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema wameanza operesheni hiyo baada ya kubaini kuwapo kwa raia wengi wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria.
“Serikali haiwezi kukaa kimya wakati vijana wanakosa ajira huku kazi zile walizotakiwa kufanya zikifanywa na raia wa kigeni. Kibaya zaidi kuna baadhi ya kampuni, viwanda na taasisi zilizoajiri wageni zinawadhalilisha na kuwanyanyasa wafanyakazi wa Kitanzania, tumeanza kuwabaini na wataondolewa,” alisema.
Masauni aliwataka maofisa Uhamiaji kuwachukulia hatua za kinidhamu wote watakaobainika kuhusika kutoa vibali kinyume cha sheria. Aliiagiza Uhamiaji kutoa ripoti ya kila kinachoendelea kwenye operesheni hiyo.
Aidha, alitaka operesheni hiyo isitafsiriwe kuwa Tanzania haitaki raia wa kigeni, isipokuwa lazima sheria na kanuni zilizopo zifuatwe.
Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Msumile aliwataka wananchi kutoa ushirikiano wakati wa operesheni hiyo na kwamba, wanatarajia kuwakamata wageni zaidi ya 350.
“Tumeanzia Kariakoo na tutasambaa kwenye manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam, naomba kila mmoja ashiriki kwenye operesheni hii ya kuwaondoa raia hawa wa kigeni wanaoingia nchini kinyume cha sheria,” alisema.
Kuhusu vibali vya muda, Masauni alisema Serikali inaandaa utaratibu mwingine wa kushughulikia wageni waliotakiwa kupewa vibali vya muda baada ya kupata malalamiko juu ya suala hilo.
“Tumepata malalamiko kupitia balozi zetu juu ya kufutwa vibali hivi kwa sababu vilianza kutolewa kwa kukiuka sheria, kwa kuwa vina umuhimu wake, Serikali inaangalia namna ya kushughulikia jambo hili,” alisema.
Alisema ushughulikiaji wa suala hilo utakwenda sambamba na kuwabaini waliokuwa wakikiuka sheria kwa kutoa vibali hivyo kiholela na kuisababishia Serikali hasara.
Pia, alisema Serikali ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mahakama ya kijeshi ya Uhamiaji ili kukomesha vitendo vya rushwa na ukiukwaji mwingine wa sheria unaofanywa na baadhi ya watumishi wa idara hiyo.
Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment