AMANI KARUME AHUDHURIA MAULID KWA MAALIM SEIF


Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (wa pili kulia), Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume (wa pili kushoto), Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) na Hassan Nasoro Moyo kwenye Maulid jana.  
Zanzibar. Rais wa awamu iliyopita wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume amehudhuria hafla ya Maulid iliyoandaliwa na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad katika kipindi ambacho Zanzibar inahaha kutatua mgogoro wa kisiasa uliotokana na Uchaguzi Mkuu.
Hafla hiyo, ambayo pia ilihudhuriwa na Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omary Kabi, iliandaliwa na mgombea huyo wa urais wa Zanzibar na kufanyika kwenye Hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Zanzibar iliingia kwenye mgogoro wa kisiasa baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani, kwa madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi.
Alitangaza kuwa uchaguzi huo utarudiwa ndani ya siku 90 na tangu wakati huo kumekuwa na mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mgogoro huo yanayomuhusisha Maalim Seif, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na makada wengine watano, akiwamo Dk Karume.
Pamoja na Maalim Seif na Dk Shein kuwa kwenye mazungumzo hayo ya kutafuta suluhisho, kumekuwapo na kurushiana maneno baina ya CCM na CUF kuhusu uamuzi wa mazungumzo hayo, na juzi yalichukua sura mpya baada ya rais huyo wa Zanzibar kujitangaza kuwa ndiye kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, akiwataka wasioamini kwenda mahakamani.
Jana kwenye hafla hiyo, Maalim Seif alipata nafasi ya kumjibu Dk Shein ingawa hakueleza moja moja kauli yake kwa rais huyo wa Zanzibar.
“Nawasihi muendelee kuwa watulivu wakati huu ambao nchi yetu imekabiliwa na mkwamo wa kisiasa. Naamini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutaweza kukwamuka, Inshaallah,” alisema Maalim.
Kwenye hafla hiyo, Maalim Seif, ambaye amekuwa akieleza kuwa ndiye aliyeshinda kwenye uchaguzi huo, aliwataka Wazanzibari kutobabaishwa na maneno ya baadhi ya watu wanaotaka kuwavunja moyo na kuwataka wawe watulivu. Imekuwa nadra sana kwa viongozi wa CCM, hasa aliyewahi kushika nafasi ya juu kama Dk Karume kuhudhuria hafla za wapinzani visiwani Zanzibar ambako upinzani wa kisiasa ni mkubwa, ingawa shughuli ya jana iliandaliwa na familia ya Maalim Seif.
Mwaka jana, mmoja wa waasisi wa Muungano, Nassor Moyo alitimuliwa uanachama wa CCM kwa madai kuwa amekuwa akihudhuria mikutano ya CUF na kuhutubia.
CUF inadai kuwa Dk Shein si rais tena wa Zanzibar kwa kuwa muda wake uliisha tangu nchi ilipopiga kura kumchagua, lakini CCM inamtetea kuwa ndiye mwenye haki ya kuendelea kuongoza hadi Rais mpya atakapochaguliwa.
Wakati CCM inawataka wafuasi wake kuanza kujiandaa kwa marudio ya uchaguzi, CUF imekuwa ikieleza kuwa ZEC inatakiwa imtangaze mshindi wa uchaguzi na haitakuwa tayari kurudia kupiga kura.

Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment