MAONI YA MHARIKRI: WALIOFELI KIDATO CHA PILI WARUDIE DARASA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg5_YOcUmmQnqWQQpZX8IkGv0bBWnHvO_S_rJW8isjsvnSKpfXg8kypln4VeaejFWQ0vsRz5A1VyIFEDuadvc3Vjaxa0_EigdvyWCAEuKYkPigTWJgNnchMMdyK7S8if4avv2AVJ1gezsci/s1600/NECTA_full.jpg

MAONI YA MHARIRI: Waliofeli kidato cha pili warudie darasa

Kwa ufupi
Juzi, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilitangaza matokeo ya Taifa ya mtihani wa kidato cha pili ya mwaka 2015 ambayo yanaonyesha kwamba wanafunzi 324,068 sawa na asilimia 89.12, wamepata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema alipokuwa akitangaza matokeo hayo kwamba wanafunzi 39,567 hawakupata alama za kuwawezesha kuendelea na kidato cha tatu.
Hata hivyo, Januari 2014 ilielezwa kuwa Serikali imetangaza kwamba wanafunzi wa kidato cha pili walioshindwa kupata wastani wa alama 30 wataruhusiwa kuendelea na masomo ya kidato cha tatu.
Badala yake, wanafunzi hao walielezwa kwamba watapewa mafunzo rekebishi (remidial classes) wakiwa kidato cha tatu, ambayo yatawasaidia kufanya vizuri katika mitihani yao ya kidato cha nne.
Kwa kuwa hatujasikia taarifa tofauti na hiyo ya kuendelea na kidato cha tatu hata kwa wale walioshindwa kufikia wastani, tunaamini kwamba huo ndiyo msimamo wa Serikali na kwamba wanafunzi wote waliofanya mtihani huo wa kidato cha pili mwaka 2015, wataendelea na masomo hadi kumaliza kidato cha nne mnamo mwaka 2017.
Kadhalika, taarifa ya Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde ya matokeo ya upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili iliyotolewa juzi, haikuzungumzia suala la wanafunzi waliofeli kurudia masomo, bali ilisisitiza kuwa kwa masomo ambayo hayakufanyika vizuri, walimu wafanye juhudi kuhakikisha ufundishaji na ‘ujifunzaji’ wa masomo hayo unaimarishwa katika kidato cha tatu ili kuinua ufaulu wa wanafunzi kabla ya kuingia kidato cha nne.
“Aidha, baraza linawasihi maofisa elimu wa mikoa na wilaya, wadhibiti ubora wa elimu kwa kufanya ufuatiliaji katika kuhakikisha kuwa ufundishaji na ujifunzaji wa maeneo yanayohitaji kutiliwa mkazo unafanyika ipasavyo.”
Ikiwa Serikali haina mpango wa kuwarudisha madarasa wanafunzi wanaofeli, tunashauri ifikirie upya kwani utaratibu huu wa waliofeli na waliofaulu wote kusonga mbele, una madhara makubwa kwa mustakabali wa elimu ya Tanzania sasa na hata siku zijazo.
Athari za mapema kabisa za mpango huo ni kuondoa kama siyo kupoteza kabisa hadhi na umuhimu wa mitihani hiyo inayogharimu fedha nyingi za walipa kodi wa Tanzania.
Kama mwanafunzi anafahamu fika kwamba mitihani hiyo haiwezi kumwathiri kwa lolote kumaliza kidato cha nne, shime ya kusoma inapungua au inakosekana kabisa.
Athari ya baadaye ni matokeo mabovu ya wahitimu wa kidato cha nne hasa kwa kuwa maandalizi na kupimwa kwao katika madarasa ya chini yalikuwa duni na hayakupewa uzito mkubwa uliostahili.
Tunaisihi Serikali kuliangalia na kulitafakari suala hili kwa kina hasa ikizingatiwa changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kuendesha mafunzo rekebishi.
Tunatoa ushauri huo kwa kuwa hatujasahau hali ilivyokuwa miaka ya nyuma pale wanafunzi waliofeli mitihani hiyo walipokuwa wanarudia darasa, ari yao ya kusoma ili waweze kuvuka kizingiti hicho ilikuwa juu na hiyo iliwasaidia wafanye vizuri katika mitihani ya madarasa ya baadaye.
Tunaamini kwamba Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ambaye ameonyesha kukerwa na mabadiliko ya mfumo wa upangaji wa madaraja ya kidato cha nne, atakunjua makucha pia katika hili la kidato cha pili.     
Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment