Tufanyie kazi tahadhari ya mafuriko
TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazotajwa kuwa na uwezekano wa kukumbwa na mafuriko makubwa, kutokana na kuwepo dalili za kunyesha kwa mvua za El nino mwezi huu hadi Machi.
Tahadhari kama hizo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na taasisi mbalimbali kuanzia Agosti mwaka jana, ambapo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), iliweka wazi kuwa zitanyesha mvua za El nino kubwa kuliko zilizowahi kunyesha miaka ya nyuma.
Kabla ya tahadhari ya kunyesha mvua Januari hadi Machi, Mamlaka hiyo ilieleza kuwa mvua hizo zingenyesha kati ya Septemba na Desemba mwaka jana, jambo linaloonesha kuwa mvua hizo hata kama zitachelewa ni lazima zitanyesha.
Kadhalika, Umoja wa Mataifa (UN) nao ulieleza juzi kuwa, upo uwezekano wa kutokea mafuriko makubwa nchini wakati huu hadi kufikia mwezi wa Tatu, kwa sababu mvua za El nino zinazotabiriwa kunyesha zitakuwa kubwa sana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya UN iliyotolewa, wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea na bomoabomoa ya nyumba za makazi ya watu kwenye maeneo hatarishi ya mabondeni na sehemu zisizoruhusiwa, wakati wa kuchukua hatua za tahadhari umefika, ili kuhakikisha maafa hayatokei.
Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi katika umoja huo, anayehusika na Misaada ya Kibinadamu na Uratibu wa Misaada ya Dharura, Stephen O’Brien alisema Tanzania inahitaji kujiandaa kukabili kadhia inayoweza kuletwa na mafuriko hayo.
Katika taarifa yake iliyowakilishwa mbele ya wajumbe wa nchi wanachama wa UN na nakala yake kutumwa kwa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye umoja huo, O’Brien alisisitiza kuwa, nchi zinazotarajiwa kukumbwa na mafuriko zinapaswa kujiandaa ipasavyo kwa kutoa misaada ya kibinadamu kwa wananchi watarajiwa wa athari za mafuriko.
Ikumbukwe kuwa mvua kama hizo ziliwahi kunyesha nchini mwaka 1998 na kusababisha maafa, ikiwemo watu kadhaa kufa, maelfu wengine wakijeruhiwa, kupoteza makazi na miundombinu kuharibika.
Kutokana na ukweli wa ukali wa maafa, tunawasihi Watanzania wenzetu mnaokaa mabondeni na kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kuishi binadamu kuondoka katika maeneo hayo kabla mvua hizo hazijaanza kunyesha.
Tunafahamu ni vigumu mtu kuamini kuwa bondeni alipojenga hapafai kwa usalama wake na mali zake, lakini ufike wakati tuwaamini wataalamu na kukubali ushauri wao ili tubaki salama.
Kufuatia tahadhari hizo, tunawashauri waliojenga pasipostahili wahame bila shuruti kuepuka maafa. Haipendezi kujiandaa kukumbwa na maafa na wala haivutii kusubiri balaa na kutaka misaada.
Habari Leo
0 comments:
Post a Comment