Dar es Salaam. Baada ya nyumba yake kuwekewa alama ya kutakiwa kubomolewa muda wowote kuanzia Januari 6, Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God, Dk Getrude Rwakatare ameitaka Serikali itii uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuzuia ubomoaji.
Mwishoni mwa mwaka jana, Serikali ilianza ubomoaji wa nyumba zote zilizojengwa mabondeni, kama Bonde la Mto Msimbazi, kingo za mito, fukwe za bahari, pia maeneo ya wazi na hifadhi za barabara, kabla haijasitisha mchakato huo Desemba 22 na kutoa siku 14 zitakazoisha Januari 5 kwa wamiliki wenyewe kuzibomoa ili kuokoa mali na baadhi ya vifaa muhimu.
Licha ya kuwakumba watu wenye vipato vya chini hasa wale waliojenga maeneo hatarishi, operesheni hiyo imewahusu watu wenye ‘mahekalu’ na majengo ya biashara kama hoteli na maduka makubwa.
Akizungumza kwa niaba ya mteja wake, wakili wa kujitegemea kutoka kampuni ya Msemwa & Company Advocates, Jerome Msemwa alizitaka mamlaka zinazohusika kuheshimu haki za binadamu ambao wanajali sheria za nchi, kabla ya kutekeleza mambo yao binafsi.
“Jengo la mteja wangu limewekewa alama X ili libomolewe. Lakini ujenzi wa nyumba hiyo ulishajadiliwa na kesi yake kuhukumiwa na Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi na akaonekana hakuvunja taratibu zozote za ujenzi. Hukumu ilitolewa Mei 22 mwaka jana na nakala ipo,” alisema Wakili Msemwa.
“Ubomoaji huo ni batili na tunaziomba mamlaka zote zinazhohusika kuheshimu hukumu iliyotolewa, na endapo utekelezaji huo utafanywa itakuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki.
Jengo la mteja wangu lina thamani kubwa na hana mahali pa kwenda likivunjwa.” Nyumba iliyowekwa alama hiyo imejengwa Mbezi Beach, pembezoni mwa Bahari ya Hindi, lakini imejengwa kwenye hifadhi ya mikoko hivyo kukiuka matakwa ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc).
Lakini Msemwa alisema tayari baraza hilo lilimalizana na mteja wake tena kisheria katika chombo chenye mamlaka kamili, hivyo kuliibua tena wakati huu huku maandalizi ya ubomoaji yakiwa yameshakamilika ni kwenda kinyume na agizo lililotolewa na mhimili huo wa dola.
Wakati Msemwa akisema kuwa tayari walishamalizana na Nemc, mwanasheria wa baraza hilo, Manichare Heche alisema kama wana kibali cha kumalizana na baraza hilo, waonyeshe.
Msemwa alieleza nyumba hiyo imejengwa 60 nje ya miti ya mikoko inayoelezwa na Nemc kuvamiwa na akaonya juu ya kuwapo kwa taratibu za kisheria kwa mtu au mamlaka inayokiuka na kuvunja sheria za nchi.
Ili kuonyesha uhalali huo, Msemwa alibainisha kuwa halmashauri husika ilimpimia mteja wake eneo hilo na kumpa hati ya umiliki kabla haijamruhusu aendelee na ujenzi huo kwa ajili ya makazi yake hivyo kuiomba Serikali kuwachunguza watendaji wake walioruhusu hilo na kuwachukulia hatua stahiki kabla ya kumfikia mteja wake.
Licha ya tishio hilo dhidi ya jengo hilo liliopo kwenye kitalu namba 2019 na 2020, Dk Rwakatare, ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu kwenye Bunge lililopita, alipoteza nyumba nyingine nne zilizokuwa kwenye kitalu namba 314 Mbezi Beach baada ya kubomolewa kwa tuhuma za kuvamia eneo hilo.
Nyumba hizo zilibomolewa chini ya ulinzi wa polisi walioongozwa na maofisa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ushirikiano na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni waliokuwa wanatekeleza agizo la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Alphayo Kidata.
Nyumba ya sasa ni moja kati ya 8,000 zitakazobomolewa katika operesheni hiyo ya kuondoa makazi kwenye fukwe, kingo za mito, maeneo ya wazi na mabondeni.
0 comments:
Post a Comment