Nchemba alisema hayo baada ya kubaini kuwepo kwa utafunwaji wa mapato ya serikali ya vibali vya mifugo, yanayokusanywa katika Mnada wa Pugu, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Alibaini kuwepo kwa hujuma hizo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza ya kukagua mnada huo na machinjio ya Vingunguti yaliyopo Manispaa ya Ilala juzi usiku.
Baadaye alitangaza hatua kadhaa, ikiwemo Mkuu wa Mnada huo wa Pugu na watumishi waliokuwa zamu Desemba 24 mwaka jana na Januari Mosi mwaka huu, kesho Jumatatu wafike ofisi ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Pili, Mwigulu alisema kuanzia sasa amesitisha ukusanyaji wa ushuru kwenye eneo la Mnada wa Pugu, badala yake makusanyo yote ya fedha za Serikali, yatafanyika kwenye Machinjio la Vingunguti kwa kutumia mashine za kielektroniki za Mamlaka ya Mapato Tanzania (EFDs).
Alisema mnada wa Pugu sasa utakuwa unatumika kutoa vibali tu vya mifugo ili kudhibiti ubora wa mifugo inayotakiwa kuchinjwa. “ Sitakuwa na huruma na hatua stahiki zichukuliwe kwa mtu yeyote mwenye dhamana ya kusimamia sekta hiyo atakayebainika kutowajibika kwa mujibu wa Sheria,” alisema.
Akizungumza katika machinjio hayo, Nchemba alisema ubadhirifu uliopo ni wa uandikaji wa vibali kwa mifugo wachache kwa ajili ya kwenda machinjioni, tofauti na idadi ya mifugo inayoingizwa machinjioni hapo. Alisema mifugo mingi inaingizwa machinjioni bila kibali.
Katika ukaguzi huo, Mwigulu alibaini uwepo wa utafunwaji wa kodi ya mifugo zaidi ya 1,107 kwa siku, kati ya mifugo 1450 iliyolipiwa ushuru, kwa ajili ya kupelekwa katika machinjio hayo kutoka Mnada wa Pugu.
“Kwa hatua za awali nimekutana na ubadhirifu wa kutafunwa kwa kodi ya mifugo zaidi ya 1,107 kwa siku, kati ya mifugo 1450 iliyolipiwa ushuru kwa ajili ya kuja kwenye machinjio ya Vingunguti kutoka Mnada wa Pugu Desemba 26,2015,” alisema.
Aidha, Nchemba alisema alisikiliza kero na maoni ya wananchi wanaotumia machinjio hayo pamoja baadhi ya viongozi wenye dhamana na kusimamia juu ya uendeshwaji wa machinjio hayo.
Nchemba aliagiza uongozi wa machinjio hayo, kukutana kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika kukiuka taratibu na sheria. Uchinjaji wa ng’ombe na mbuzi katika machinjio hayo, hufanyika nyakati za usiku kuanzia saa 4 hadi 10 alfajiri.
Habari Leo
0 comments:
Post a Comment