Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amelipa siku saba Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutoa maelezo kwa kubadili mfumo wa kupanga madaraja ya matokeo ya kidato cha nne na sita, kutoka jumla ya pointi kwenda wastani wa pointi (GPA).
Aidha, waziri huyo aliyewahi kuwa katibu mtendaji wa Necta, kwa miaka tisa, amelitaka baraza hilo kueleza sababu za watahiniwa binafsi kuanza kufanya mitihani ya upimaji endelevu.
Maagizo hayo yalitolewa na Profesa Ndalichako alipokutana na menejimenti ya baraza hilo jana Dar es Salaam baada ya Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde kueleza kuwa walifanya mabadiliko hayo kutekeleza maelekezo kutoka Wizara ya Elimu.
“Hakikisheni mnakuwa na misingi mizuri ya kimaamuzi na msikubali kufanya maamuzi yasiyo na tija kwa Taifa letu,” alisema Profesa Ndalichako huku akitolea mfano jinsi alivyokataa kwa barua watahiniwa binafsi kufanya mtihani wa upimaji endelevu, wakati akiwa katibu mtendaji wa baraza hilo.
“Tunawapa wiki moja mtupe maelezo. Tunataka kujua ninyi kama Baraza mliona sababu gani za msingi kubadili huu mfumo; faida zake nini, na mliwashirikisha watu gani. Kazi ya kuhakikisha utendaji wa taasisi zetu unakuwa mzuri ndiyo imeanza,” alisema Profesa.
Majibizano
Sakata hilo lilianza baada ya Dk Msonde kueleza sababu za mabadiliko hayo, huku akisisitiza mara kadhaa kuwa lengo lilikuwa kurahisisha udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu.
“Yalikuwa maagizo ya kuzitaka taasisi zote za serikali na serikali yenyewe kuwa na mifumo inayofanana yaani mifumo ya matokeo ya Necta ihusishwe na mifumo ya udahili ya TCU (Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania) na Nacte (Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi),” alisema Dk Msonde.
Aliongeza; “Mfumo wa wastani wa pointi haujabadili chochote kuhusiana na mfumo wa jumla ya pointi. Tumeutumia katika matokeo ya kidato cha pili, cha nne na cha sita na haujaleta matatizo. Wananchi na wanafunzi wa ngazi zote wanauelewa.”
Majibu hayo yalimzindua Profesa Ndalichako na kuhoji, “Hivi ni lini TCU walisema kuna ugumu wa kudahili kwa sababu ya uwapo wa mfumo wa jumla ya pointi? Tueleze kulikuwa na athari gani awali mpaka muanze kutumia GPA?”
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila akitoa ufafanuzi kuhusu udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu alisema, “Mfumo wa udahili unaangalia taaluma si GPA. Mtu kama anakwenda kusoma taaluma fulani wanatazama masomo aliyosoma tu. Kama anakwenda kusoma sayansi watatazama masomo ya sayansi aliyosoma.”
Kutokana na kukosekana majibu sahihi, ndipo Profesa Ndalichako alitoa agizo hilo, huku akisisitiza kuwa ili Wizara ilielewe baraza hilo, lazima litoe sababu za msingi badala ya hizo walizoeleza jana.
Kuhusu mtihani wa upimaji endelevu, Profesa Ndalichako alisema haiwezekani watahiniwa binafsi kila somo wakafanya mitihani miwili, na kwamba ikiwa Necta haitatoa majibu ya kuridhisha, mitihani ya upimaji endelevu itafutwa.
Awali, akizungumza na wafanyakazi wa baraza hilo, Profesa Ndalichako alipongeza utaratibu wa kutoa vyeti mbadala kwa waliopoteza vyeti vyao halisi.
Pia, alilitaka baraza hilo kuwasilisha majibu ya mitihani ya watahiniwa wote ili wizara iyapitie.
Alisisitiza kuwa wakati mwingine wanafunzi hushindwa kujibu chochote au kwa ufasaha kutokana na matatizo ya walimu.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment