Dar es Salaam. Wakati Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) likiendesha bomoabomoa katika maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam, Abdallah Bulembo, aliyekuwa meneja kampeni wa Rais John Magufuli amepinga operesheni itakayofanyika nje ya maeneo ya Bonde la Msimbazi na amemshauri Rais aingilie kati ili isitishwe.
Bomoabomoa hiyo, inayolenga nyumba zilizojengwa mabondeni, kwenye fukwe za bahari, kingo za mito na maeneo ya wazi, imekuwa ikipingwa vikali na wamiliki na wakazi wa nyumba hizo kwa maelezo kuwa hawakupewa taarifa na hawajaandaliwa sehemu mbadala ya kwenda.
Wakazi hao wamefikia hatua ya kumlaumu Rais Magufuli kwa kutojitokeza na kukemea ubomoaji huo, ambao katika baadhi ya maeneo umesimamishwa na Mahakama Kuu kwa muda.
Jana, Bulembo, ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, aliiambia Mwananchi katika mahojiano maalumu kuwa anakubaliana na bomoabomoa inayofanyika Jangwani na maeneo hatarishi ya Bonde la Msimbazi, lakini akaitaka NEMC kuacha kubomoa nyumba ambazo haziko kwenye bonde hilo.
Bulembo, ambaye aliambatana na Rais Magufuli kwa siku 52 katika kampeni za urais alisema kuwa operesheni hiyo inamjengea chuki Rais Magufuli kwa wananchi.
Bulembo, ambaye alikuwa na mazungumzo na Rais Jumatatu wiki hii, alisema kuendelea kuwabomolea wananchi nyumba walizokuwa wakiishi miaka mingi, ni kuvuruga imani waliyonayo kwa kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambaye wakati wa kampeni zake aliwaahidi neema.
Kauli hiyo imekuja wakati takribani nyumba 16,000 zimeshawekewa alama ya kutakiwa kubomolewa na tayari nyumba 700 zikiwa zimebomolewa jijini Dar es Salaam, hali iliyowaacha baadhi ya wakazi wakiwa hawana sehemu za kujihifadhi, baadhi kupoteza fahamu na wengine kufungua kesi Mahakama Kuu.
“NEMC wasiwe kama wameshuka kutoka mbinguni na kukuta watu wamejenga mabondeni. Wasituharibie imani ya wananchi kwa Rais,” alisema Bulembo ambaye alikuwa na Magufuli katika kampeni za nchi nzima na kuwezesha CCM kushinda katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.
“Kwani (NEMC) walikuwa wapi siku zote mpaka wafanye shughuli hiyo sasa baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani? Sikubaliani na bomoabomoa hiyo isipokuwa hiyo ya Jangwani na sehemu hatarishi za Bonde la Msimbazi.”
Kwa nini Jangwani
Akijenga hoja yake ya kukubaliana na ubomoaji wa nyumba za Jangwani katika Bonde la Msimbazi, Bulembo alisema eneo hilo kwa sasa ni hatarishi, hasa kutokana na tishio la mvua za El Nino.
“Kuna maeneo hatarishi kama Jangwani na Bonde la Msimbazi, huko bomoabomoa hiyo iendelee,” alisema.
“Mbali na eneo la Jangwani kuwa hatarishi kwa usalama wa watu, baadhi ya wakazi wake waliwahi kuondolewa na kupewa viwanja eneo la Mabwepande, lakini wakaviuza na kurejea upya.
“Lakini maeneo mengine kama ya Ali Maua, kwa nini uwabomolee watu wakati hatujasikia wamepata mafuriko na watu hao wako hapo kwa miaka yote?”
Bulembo alisema kuna maeneo mengine ambayo kuna mabonde, lakini hayajawahi kuleta madhara kwa wananchi hivyo hakuna haja ya kuwabomolea nyumba watu wa maeneo hayo wakati wameishi kwa miaka zaidi ya 20 au 30.
“Kuna watu wamekaa mahali kwa miaka 24 au 30 hawajawahi kupata mafuriko, hata kama wapo karibu na bonde, lakini si eneo hatarishi kwanini wabomolewe? alihoji kiongozi huyo wa zamani wa soka nchini.
“NEMC waache kuleta hasira za wananchi kwa Rais wao, walikuwa wapi mpaka wanasubiri sasa,” alisema Bulembo.
Rais hapendi umaskini
Wakati wakazi hao wanaobomolewa nyumba mabondeni wakidai kuwa operesheni hiyo inawaondoa kwenye umaskini na kuwafanya mafukara, Bulembo alisema anaamini hata Rais hafurahii kuona walalahoi wakiteseka kwa kuwa hata wakati wa kampeni alionyesha kulisikitikia kundi hilo.
“Moja ya mambo yaliyomsikitisha Rais wakati wa kampeni ni umaskini wa Watanzania. Alisema anaomba kura za wanyonge na ndiyo maana aliahidi kuondoa kero mbalimbali, ikiwamo kodi za wafanyabiashara wadogo,” alisema.
Nyumba 16,000 kubomolewa
Wakati Bulembo akisema hayo, NEMC walikuwa wakiendelea na ubomoaji na uwekaji alama ya “X”, ikiathiri wananchi wengi zaidi baada ya idadi ya nyumba zinazopaswa kubomolewa kufikia zaidi ya 16,000.
Kwa wastani wa kaya moja kuwa na watu wanne na nyumba moja kuwa na kaya kuanzia tano, ubomoaji wa nyumba 16,000 utasababisha watu 300,000 kukosa makazi, huku wanafunzi walio mwaka wa mwisho wa elimu ya msingi na sekondari wakiathirika zaidi.
Hali hiyo imezidi kuwatia wasiwasi wakazi hao huku wengine wakiporomosha vilio na kuzimia kutokana na mawazo ya kukosa mbadala wa makazi.
Ofisa mwandamizi wa NEMC, Arnold Kisiraga aliwaambia wanahabari jana kuwa kati ya nyumba 16,000 tayari 700 zilizokuwapo bonde la Mkwajuni, Hananasif na Suna zimeshabomolewa.
Kisiraga alisema huenda idadi ya nyumba zitakazobomolewa itaongezeka kutokana na utaratibu unaoendelea wa kubaini zilizojengwa mabondeni na kwamba leo watahamia Kigogo baada ya jana kumaliza Ulongoni, Gongo la Mboto na Pugu Mnadani.
Kwa jana pekee, alisema walibaini nyumba 885 zinazopaswa kubomolewa kutokana na kujengwa katika mazingira hatarishi, ikilinganishwa na juzi wakati walipobaini nyumba 647 zilizokuwa bonde la Mto Msimbazi--kuanzia Stakishari, Ukonga hadi Gongo la Mboto. “Hili zoezi la uwekaji alama ni moja na lile la ubomoaji linaloendelea Kinondoni. Ni vizuri zaidi wakaondoka wenyewe baada ya kuwekewa alama. Huu muda wangetumia vizuri kujipanga kuondoka kwa sababu yale ni maeneo hatarishi,” alisema Kisiraga wakati wa uwekaji alama hizo. Kuhusu uchambuzi wa nyumba 681 zinazotakiwa kuachwa katika bomoabomoa kutokana na zuio la Mahakama Kuu, alisema wanaendelea kuzibainisha na watakapomaliza wataanza kuzibomoa haraka zile zisizohusika na kesi.
‘Ni msiba mkubwa’
Wakati uwekaji alama hiyo ukiendelea, vilio vilitanda na baadhi wakihoji tarehe rasmi ya kubolewa makazi yao.
Yunis Amos, mkazi wa Ulongoni aliangusha kilio baada ya kuona nyumba yake ikiwekwa alama.
“Ni msiba mkubwa sana,” alisema Yunus huku akishika kichwa.
“Presha hapa inapanda na kushuka. Tutaishije na watoto hawa na wengine ni yatima? Huyu Magufuli anataka tuishije?”
Mkazi wa Bangulo, Saida Ally yeye aliwajia juu vibarua wa NEMC wanaoweka alama hizo, akiuliza eneo la kwenda baada ya nyumba yake kubainishwa kuwa itabomolewa. “Wanasema nianze kutoa bati sasa, nizipeleke wapi? Wanasema utaratibu utafuata baadaye, ni muda gani tuwe tumehama na tutahamaje? Sehemu ya kwenda sisi hatuna labda wakibomoa tutaenda kulala kwa huyo mwenyekiti wetu wa mtaa, hakuna namna,” alisema.
Azimia kwa kushindwa kuhimili
Ofisa mipango miji wa Ilala, Alfred Mbyopo alisema wananchi wengi wametaharuki baada ya nyumba zao kuwekewa alama za kutakiwa kubomolewa na juzi kuna mkazi mmoja alizimia.
“Kuna taharuki kubwa sana katika operesheni hiyo. Juzi kuna bibi mmoja pale Ulongoni A nasikia alizimia kwa kushindwa kuhimili uchungu wa nyumba yake kuwekewa alama ya kubomolewa. Lakini sisi tunawaokoa na hatari ya baadaye,” alisema Mbyopo.
‘Kidogo leo naweza kula’
Wakati baadhi wakilia, kwa Erasto Nyakiegi, kwa mkazi wa Mtaa wa Mwanapindi, Bangulo, mambo yalikuwa tofauti baada ya kutoka kwenye ‘kifungo’ cha sintofahamu kutokana na nyumba yake kukoswakoswa na alama hiyo.
“Tulikuwa tukiishi kwa wasiwasi sana na familia yangu tukijua ni nyumba zote za mabondeni. Karibu mwezi mzima nilikuwa sina hamu ya kula wala kulala, lakini leo naona nipo huru zaidi kwa kuwa nyumba yangu ipo nje ya zinazotakiwa kubomolewa. Kidogo leo naweza kula,” alisema Nyakiegi.
Hata hivyo, Mbyopo ambaye yumo kwenye uwekaji alama hizo, alisema kuna uchimbaji mkubwa wa mchanga ambao umesababisha Mto Msimbazi kuzidi kuliwa kingo zake na kuwaingiza baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye maeneo salama, kukumbwa na bomoabomoa.
Imeandikwa na Kizitto Noya, Irene Mapendo na Nuzulack Dausen
0 comments:
Post a Comment