RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amesema yeye bado ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar huku akiwataka wasioamini katiba hiyo, wapeleke shauri hilo Mahakama Kuu ya Zanzibar yenye uwezo pekee wa kutafsiri katiba.
Amebainisha kuwa yeye anaongoza nchi kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kwamba kama si uwezo huo aliopewa kikatiba hana sababu ya kuendelea kukaa madarakani pamoja na serikali anayoingoza.
“Tuko madarakani na uongozi wote wa serikali… yupo Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais na mawaziri,” alisisitiza Dk Shein na kuongeza kuwa hao wanaodai kujiondoa serikalini huo ni uamuzi wao wenyewe.
Alibainisha kuwa yeye na serikali anayoiongoza kuendelea kuwepo madarakani si kwa uamuzi wake na wala hana ubavu wa kujiweka madarakani bali ni Katiba ambayo inajieleza wazi.
Dk Shein alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu kisiwani humu kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi.
Aliwaambia wananchi kuwa yako mengi yanayosemwa lakini hawapaswi kuyasikiliza kwa kuwa kama ni serikali yeye ndiye Rais hivyo wanapaswa kumuamini anachowaeleza.
“Ya mjini yapo yasikilizeni lakini kwa Serikali mimi ndiye Rais na nisiposema mimi nitawatuma wasaidizi wangu kuwaeleza,” Dk Shein alisema na kuongeza kuwa ya vyama kila mtu ana chama chake.
Alisema kama ni suala la Chama Cha Mapinduzi (CCM) yeye ndiye Makamu Mwenyekiti Zanzibar na kama kuna la kuwaeleza wana CCM na wananchi atawaeleza yeye na viongozi wenzake wa chama hicho pamoja na taarifa za vikao vya chama vyake.
Dk Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ushindani wa kisiasa si ugomvi bali ni utaratibu wa kupeana changamoto katika uongozi
Habari Leo
0 comments:
Post a Comment