Ukawa kidedea umeya, CCM ‘yatia mpira kwapani’
Dar es Salaam. Figisufigisu la umeya katika manispaa za Ilala na Kinondoni limefika mwisho kwa Chadema kuibuka kidedea kwa nafasi za umeya, mshirika wake katika Ukawa, CUF, ikichukua nafasi za manaibu meya huku madiwani wa CCM Ilala ‘wakiweka mpira kwapani’.
Mbali na madiwani wa CCM kususia uchaguzi huo wakipinga wabunge viti maalumu kutoka Zanzibar kuzuiwa, wale wa Ukawa walilalamika kuwaweka madiwani kwenye kambi na kutumia kalamu maalumu walizodai zinachukua picha ya kura walizopiga ili kuzuia hujuma.
Katika uchaguzi huo, Diwani wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob alishinda umeya wa Kinondoni kwa kura 38 dhidi ya 20 alizopata Benjamin Sitta wa CCM. Naibu Meya alichaguliwa Jumanne Mbunju wa Kata ya Tandale (CUF) aliyepata kura 38 dhidi ya 19 za John Manyama (CCM).
Kwa upande wa Ilala, aliyeshinda ni Charles Kuyeko (Chadema) aliyepata kura 31 na naibu ni Omari Kumbilamoto (CUF) ambaye pia alipata kura 31 za madiwani wa Ukawa, baada ya wale wa CCM kususia. Madiwani waliotakiwa kupiga kura walikuwa 54.
Awali, uchaguzi katika manispaa hizo uliharishwa mara ya mbili, kutokana na CCM kutaka kuwatumia kuoiga kura wabunge wa viti maalumu kutoka nje ya Dar es Salaam na mawaziri walioteuliwa na Rais.
Mgogoro huo ulitinga mahakamani mara mbili na kutupwa kisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachaweze kuamua uchaguzi huo ufanyike si zaidi ya jana.
Meya Kinondoni
Kabla ya kuanza kwa upigaji kura, madiwani walianza kwa kula kiapo, kisha wagombea wa umeya, Boniface na Sitta kupewa fursa kujielezea kwa dakika tano na kuomba kura.
Sitta alisema akipata nafasi hiyo atahakikisha analeta mabadiliko kwa sababu Kinondoni bado ina changamoto nyingi ukiwamo usafi.
Jacob aliahidi kusimamia ukusanyaji wa mapato, udhibiti wa matumizi mabaya ya fedha na utumishi uliotukuka.
“Nitafanya kazi kwa staili ya utatu, yaani wananchi, utaalamu na utumishi. Hii ndiyo itakuwa dira ya utumishi ili nitimize malengo nikishirikiana na madiwani wenzangu,” alisema.
Baada ya kujinadi upigaji kura ulianza saa 11.45 hadi 12.07. Msimamizi wa uchaguzi, Celestine Onditi aliwaita wagombea wawili mbele na kisha kufungua sanduku la kura na kuzimwaga katika meza wajumbe wote wakishuhudia na baada ya kuhesabu alimtangaza Jacob kuwa meya na Mbunju naibu na ukumbi ulilipuka kwa shangwe.
Watoa shukrani
Jacob aliahidi kufanya kazi na kila mjumbe bila kujali itikadi za vyama na kuwataka wajumbe kuwa kitu kimoja huku Mbunju akisema atakuwa mshauri wa karibu wa Jacob na kuwataka wajumbe wote bila kujali itikadi wampe ushirikiano.
Siri ya ushindi
Baadhi ya madiwani wa Chadema kwa nyakati tofauti walitaja siri ya mafanikio ya ushindi huo kuwa ni kucheleweshwa kwa uchaguzi na kukwepa hujuma.
Diwani wa Kijitonyama, Athuman Uloleulole alisema kuharishwa kwa uchaguzi huo kuliwapa faida kubwa kwa sababu walitumia muda huo kukaa katika moja ya hoteli Kijitonyama na kupewa mikakati ya namna ya kukabiliana mbinu za washindani wao.
“Kambini tulikuwa tunaingia saa tisa alasiri hadi saa 12 asubuhi. Tukiwa kambini tulikuwa tunajengewa uwezo na viongozi wetu wa CUF na Chadema,” alisema.
Alisema walikaa kambini mara tatu kwa nyakati tofauti, ikiwamo usiku wa kuamkia jana, ambao walikaa katika hoteli moja iliyopo Sinza na kupewa mbinu na msimamo wa nini cha kufanya katika uchaguzi huo.
Alisema wajumbe wa Ukawa walipewa peni maalumu kwa ajili ya kupigia kura jambo ambalo ililiwawia vigumu kusaliti na kumpigia mgombea wa CCM.
“Hii ni kama teknolojia tuliyoitumia, hizi peni ukifungua kizibo ina kamera inayokuonyesha kitu unachotaka kukifanya. Hivyo siyo rahisi kusaliti kwa sababu ukiipigia kura CCM utajulikana tu, halafu kingine Jacob ni mpambanaji, wajumbe wote wa Ukawa tulikuwa na imani naye,” alisema.
Diwani wa Mbezi (Chadema), Hamphrey Sambo alisema kwa kuahirisha uchaguzi, CCM walidhani wanawakomoa Ukawa, kumbe ilikuwa kinyume chake kwa kuwa walijipanga dhidi ya figisufigisu kutoka upande wa pili.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alisema siri ya ushindi huo ni Ukawa kusimamia mambo matatu; sheria, mbinu za kuwadhibiti wajumbe wasilaghaiwe na matumizi ya peni za kamera.
“Tulimwambia mapema mkurugenzi kuwa tunataka sheria ifuatwe ndiyo maana leo (jana) umeona idadi kamili ya wajumbe, hakuna aliyezidi,” alisema Mdee.
Aliungana na Uloleulole kuwa kila mjumbe wa Ukawa alipewa peni maalumu kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo na kila peni ilikuwa na jina la mjumbe husika.
“Hii peni (anaonyesha) ukiifungua tu ina kamera. Ukianza kuitumia kuna mtu maalumu alitayarishwa kwa ajili ya kuangalia wajumbe wote wa Ukawa wanaopiga kura ili kusitokee usaliti. Sasa kama kuna mjumbe wa Ukawa kachukua fedha halafu hajaipigia kura CCM huyo atamalizana nao mwenyewe,” alisema Mdee.
Alisema baada ya kumpata meya huyo peni hizo maalumu zimekusanywa na kuhifadhiwa kwa ajili ya matukio mengine.
Mawaziri waliopiga kura
Mawaziri watatu jana walitinga ukumbini kupiga kura akiwamo Dk Augustine Mahiga wa Mambo ya Nje, Profesa Makame Mbarawa wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki.
Mbali na hao alikuwapo Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
Hali ilikuwa tofauti na chaguzi kadhaa zilizoharishwa kwani safari hii wafuasi wa CCM waliojitokeza walikuwa wachache ukilinganisha na Ukawa.
Meya Ilala
Uchaguzi wa meya wa Ilala uliosusiwa na madiwani wa CCM wakidai kutoridhishwa na taratibu za kuwatambua madiwani waliokuwa na sifa ya kupiga kura, ulitanguliwa na mabishano ya hoja na rabsha zilizosababisha polisi kuingilia kati.
Hatua ya CCM kususia ilitokana na msimamo wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi ambaye alisema katika vikao walivyofanya awali na viongozi wa vyama husika, walikubaliana kuwaondoa wabunge watatu wa viti maalum kutokana Zanzibar, wakizingatia mwongozo uliotolewa na Simbachawene.
“Waziri alituelekeza kwamba madiwani wanapaswa kutambulika kutokana na maeneo waliyotoka, walipochukulia fomu zao kuomba nafasi hizo.”
Alisema Chadema wana wabunge watano kutoka Bara wa viti maalumu, CCM wapo tisa, watatu ndiyo wanatoka Zanzibar.
Aliongeza; “sasa tumekubaliana kuwa hawawezi kuhusika huku, hivyo hawaruhusiwi kupiga kura kwenye uchaguzi huu.”
Kauli hiyo ilisababisha Mbunge wa Viti Maalumu kutokana Zanzibar, Anjela Malembeka kusimama na kuomba mwongozo akieleza kuwa Bunge ni moja la Jamhuri ya Muungano, nao wanatoka kwenye mkoa uliopo Zanzibar, hivyo ana haki kama wabunge wengine kuwa diwani wa Ilala kwa kuwa fomu yake aliiombea huko.
“Msitubague, sisi sote ni wabunge wa viti maalumu tumeletewa barua za kuhudhuria hapa iweje mseme waliotoka Zanzibar haturuhusiwi hata kama kasema waziri, yeye siyo sheria,” alisema Malembeka na kuugwa mkono na madiwani wa CCM kwa kumshangilia.
Mkurugenzi hakukubaliana naye hivyo akaagiza hatua za kupiga kura kuanza ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi huo unakamilika.
“Sasa kwa kuwa tulijadiliana na kiongozi wenu kabla lakini mnakataa, ninatangaza kuwa nimeamua kufuata mwongozo wa NEC, hivyo kila chama ni mbunge wake mmoja tu wa viti maalumu ndiye atakayeruhusiwa kupiga kura, CCM atakuwa Sophia Simba,” alisema Mngurumi kabla ya madiwani wa CCM kupiga kelele kupinga.
Ndipo rabsha zikazuka kabla ya mmoja wa madiwani wa CCM ambaye hakujulikana jina lake kuchukua sanduku la kupigia kura na kulificha ili kuzuia upigaji kura.
Polisi waliingilia kati kudhibiti hali hiyo na kuzuia vifaa vya kupigia kura kuondolewa ukumbini, kisha mkurugenzi akaanza kuita majina na upigaji kura kuanza saa 7.48 mchana. Baada ya uamuzi huo, madiwani wa CCM walianza kutoka nje huku mkurugenzi huyo akiagiza mlango ufungwe bila mafanikio.
Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyeushuhudia hali hiyo akiwa na mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, alisema ushindi huo ni uamuzi wa wananchi na anaamini watailetea maendeleo manispaa hiyo kutokana na kuwa na vingi vya mapato.
“Hakuna ubishi kwamba meya alikuwa wetu lakini imekuwa na vikwazo tangu Novemba mwaka jana, ushindi huu ni uamuzi wa wananchi bila shaka mabadiliko yataonekana katika ukusanyaji wa mapato maana kumekuwa na ufisadi,” alisema.
Akizungumzia uchaguzi huo, Diwani wa Upanga (CCM), Adnan Kondo alisema hatua ya kumtambua mbunge mmoja tu wa viti maalumu kuwa ndiye anayestahili kupiga kura ni kinyume na taratibu zinazojulikana.
“Tumeshindwa kumuelewa mkurugenzi, kwa nini mbunge Sofia Simba ndiye aonekane ana haki hiyo na wengine wamepatikana Ilala kwa mchakato huohuo, viongozi wetu wanakutana wanajadili hatua zaidi ya kuchukua,” alisema Kondo.
0 comments:
Post a Comment