Kwanini wapenzi huumiza wenza wao?
NA HALIMA MLACHA
IMECHAPISHWA: 28 NOVEMBA 2015
MPENZI ambaye anampenda kwa dhati
mwenza wake, si rahisi kufanya jambo la kumuumiza. Mapenzi mara zote humtaka mtu
kuonesha anamjali mwenza wake kwa kila kitu zikiwamo hisia zake.
Ndio maana wapenzi wengi hujikuta
wakijitahidi kufanya mambo yasiyogusa vibaya hisia za wenza wao kama vile
kuhakikisha mara zote wana furaha, wanasaidiana kutimiza ndoto zao na hata
kusaidiana pindi wanapokumbwa na matatizo.
Kama una mpenzi au mwenza ambaye
hafanyi angalau jambo moja hapo juu, kwa kweli uhusiano huo hautakuwa na kitu
chochote kinachoitwa upendo, kwa kuwa maana halisi ya mapenzi inaendana na sifa
hizo hapo juu.
Wapo wenza wengi tu katika maisha
yetu, wanafanyiana yote hayo yaani wanapendana na kuthaminiana kwa kila kitu na
hawana wasiwasi na uhusiano wao, kwani kwa kufanyiana hivyo ni kinga thabiti ya
kutovunjika kirahisi kwa pendo lao.
Hata hivyo katika baadhi ya
uhusiano, kama mwenza mmoja anataka kuvunja uhusiano kutokana na sababu zake,
zikiwamo za hisia matokeo yake siku zote huwa mabaya. Wenza wengine wanapotaka
kuvunja uhusiano, huwa na tabia ya kukumbuka vitu vyote alivyowekeza katika
uhusiano huo awali na hapo atajisikia kuwa yote aliyoyafanya yameenda bure.
Atakuwa anajisikia kuwa mambo yote
aliyojitolea kwa miaka mingi, hayakuwa na maana hivyo kukata tamaa na hasira
zake kuishia kwa mwenza wake. Kutokana na hali hiyo ya hasira kutawala, mara
nyingi hujisahau kuwa hata kwa upande wake yeye anayetaka kukatisha uhusiano
huo anaweza kuumia.
Lakini kwa kuwa atakuwa ametawaliwa
na mawazo ya kulipiza kisasi, hujikuta akitoa uamuzi ambao baadaye wengi wao
hujutia. Hali hii ni maafa katika uhusiano, kwa kuwa inapojitokeza yale yote
mazuri katika uhusiano, hupata maumivu ambayo huweza kugeuka kovu la milele.
Ndio maana nabaki na maswali sasa
kama unampenda mwenza wako, kwanini umuumize? Kwa maoni na mapendekezo,
wasiliana nasi kupitia dimbwimahaba@dailynews-tsn.com au dimbwimahaba@yahoo.com
0 comments:
Post a Comment