Dar es Salaam. Rais John Pombe Magufuli amekuwa wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi kuanza nchini kutumia muda mrefu kutangaza Baraza la Mawazi kutokana na kile wasomi, wachambuzi wa siasa kusema pengine anapata wakati mgumu kupata mawaziri watakaoendana na kasi yake.
Katiba ya mwaka 1977 inamtaka Rais kumteua waziri mkuu ndani ya siku 14 tangu alipoapishwa na kulipeleka jina lake bungeni, lakini katiba hiyo ipo kimya kuhusu uteuzi wa mawaziri, hivyo Rais anaweza kutumia muda wowote.
Wakati Rais mstaafu, Benjamin Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995 aliteua baraza la mawaziri Novemba 28, siku tano baada ya kuapishwa, Jakaya Kikwete alitangaza Baraza la kwanza Siku 14 baada ya kuapishwa na Dk Magufuli hadi sasa, siku 25 zimepita tangu aapishwe Novemba 5, mwaka huu hajafanya hivyo.
Kazi ambazo Rais Magufuli ameanza kuzifanya bila mawaziri ni kuzuia safari za nje, kuzuia sherehe za Uhuru na kuanza kupambana na wabadhirifu wa fedha za umma.
Wasomi hao wakilinganisha alichokisema kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge, walisema kuwa ana njozi za Tanzania aitakayo huku akieleza wazi kuwa anatambua kuna mawaziri, wabunge wanakula rushwa na akibainisha wazi hana imani kama waliomo ndani ya CCM wanakula pia.
Mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Elijah Kondi, alisema kuwa sababu za Magufuli kuchelewa kutaja Baraza la Mawaziri ikilinganishwa na Serikali zilizopita inatokana na utendaji wa Mawaziri wa Serikali iliyopita, wengi hawakufanya vizuri na baadhi yao hata ushindi wao wa ubunge una maswali mengi.
Alisema tayari ana njozi za anachotaka kukifanya, anapata wakati mgumu wa ni nani mtu sahihi wa kumsaidia kutimiza njozi zake, hata ndani ya CCM baadhi yao hawaaminiki na amekuwa akisema hivyo mara nyingi. Alipozungumzia rushwa pia hakusita kuwahusisha walio ndani ya CCM, japo siyo moja kwa moja.
“Inawezekana waliopo wengi anaona hawawezi kuendana na kasi yake, pengine hata wale anaoona wana afadhali walishawahi kupata kashfa mbalimbali, huku yeye akiwa na njozi za kuanza upya na watu wenye utashi wa mabadiliko ya kweli na ya wote, ”alisema Kondi.
Profesa George Shumbusho, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema Rais anapata wakati mgumu kuteua mawaziri kutokana na changamoto alizozitaja siku ya kuzindua Bunge kuwa nyingi na nzito, zinazohitaji watu makini kuzitekeleza.
Alisema analazimika kufanya upembuzi yakinifu kujua ni nani na atashughulikia eneo gani kama anavyotaka yeye, liendane na kasi na utendaji wake.
“Ninachokiona anataka kuunda baraza makini hataki kurudi na kuhoji utekelezaji wa kazi, kingine anahitaji aunde litakalokaa muda mrefu na kufanya utekelezaji badala ya kuunda lingine kwa muda mfupi, ”alisema Profesa Shumbusho.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhadhiri mwandamizi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya, alisema anachukua muda kutaja Baraza la Mawaziri kutokana na kutaka litakalotambua anataka nini kifanyike katika Serikali yake ambayo amekuwa akiitaja moja kwa moja kuwa ya Magufuli.
Alifafanua kuwa hataki kukurupuka na kujilaumu baadaye kutokana na utendaji usioridhisha unaoweza kujitokeza asipokuwa makini, ndiyo maana anachukua muda na kujaribu kuonyesha ni jinsi gani inawezekana kusimamia vitu na vikaenda.
“Kwa kuangalia kasi yake, unaona kabisa anapata wakati mgumu kupata viongozi watakaofanya kazi kwa lengo moja ya mageuzi na mabadiliko, ndiyo maana anachukua muda ili akija nalo liwe makini, ” alisema Mallya.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda, alisema kwenye mitandao ya kijamii kuna utani unazunguka kuwa kwa kasi yake anaweza kufanya kazi hata bila kuwa na mawaziri.
“Ni utani, lakini ukiuchunguza mara mbili unaona kabisa hata wananchi wameona anachokifanya na wanahitaji kukiona hicho kutoka kwenye Baraza lake,” alisema.
Alisema kasi yake na kubana matumizi alikoanza nako anahitaji kuwa makini kwa sababu alitamka anataka kuwa na baraza dogo la mawaziri.
Alifafanua kuwa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne mwaka 2005, mawaziri na naibu wao idadi yao ilikaribia 60, wakitumia mashangingi yanayokula mafuta, posho, hivyo ili kudhibiti hilo atachukua muda pia, ikiwamo kuvunja baadhi ya wizara kama ataona itafaa na kumsaidia anachotaka kukifanya.
0 comments:
Post a Comment