TRA INACHUNGUZA 'BANDARI' YA AZAM

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Elimu kwa Mlipa

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo. 
By Nuzulack Dausen, Mwananchi.
Dar es Salaam. Mkakati wa kudhibiti uvujifu wa mapato serikalini unazidi kushika kasi baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuiagiza kampuni ya Bandari ya nchi kavu ya Azam kusitisha uhamishaji wa mizigo katika eneo la kampuni hiyo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa makontena na ukwepaji wa kodi.
Hata hivyo, uongozi wa Azam umebainisha kuwa upotevu wa makontena hayo hauhusishi bidhaa zinazomilikiwa na kampuni hiyo na kwamba umejitoa kwa hali na mali kufanikisha uchunguzi wa sakata hilo.
Kampuni hiyo inatuhumiwa kuhusika kwa upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya Sh80 bilioni yaliyoripotiwa kupotea hivi karibuni wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Kamishna wa Forodha wa TRA, Wolfgang Salia kwa Meneja Mkuu wa Said Salim Bakhresa & Co Ltd, kampuni hiyo imezuiwa kupeka mizigo kwenye Bandari kavu namba 003.
Barua hiyo ilieleza kuwa uongozi wa kampuni hiyo ulikuwa ukitambua bayana kuwa uondoshaji mizigo katika eneo la forodha bila kulipa kodi na ushuru wa forodha ni uvunjifu wa Sheria ya Usimamizi wa Forodha wa Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na unapunguza mapato serikalini.
“Kutokana na suala hilo, imeamriwa kuwa upelekaji wa mizigo katika bandari yako ya nchi kavu usimamishwe mara moja kuanzia siku ya tarehe ya barua hii hadi hapo itakapoamuliwa. Wadau wote wanaohusika wanatakiwa kufuata amri hii,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa Novemba 17, 2015.
Barua hiyo iliyoandikwa siku 10 kabla ya ziara ya Waziri Mkuu, na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, ilisema uondoshaji wa mizigo katika eneo hilo kwenda kwa wateja utaendelea kama kawaida.
Azam ni moja ya kampuni kubwa nchini inayofanya biashara mbalimbali zikiwemo utengenezaji wa bidhaa za vyakula na vinywaji, uchukuzi, habari, na michezo.
Katika taarifa yao fupi, kampuni ya Azam wamesema barua hiyo inayosambaa kwa sasa mitandaoni, ilipokelewa kwa wakati na kwa sasa kuna uchunguzi unaofanywa na TRA na kwamba kampuni yake inatoa ushirikiano wa kina ili kuhakikisha “wote wanaohusikana na upotevu huo wanachukuliwa hatua na kodi yote ya Serikali inalipwa na wamiliki wote wa makontena yaliyo husika katika upotevu huo.”
Source: Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment