SIRI YA JINA JANET NA KUWA MKE WA RAIS

Kila mzazi anapokaribia kupata mtoto, moja ya mambo muhimu ambayo hufikiria juu ya jina la kumpatia baada ya kujifungua na mtoto kuishi duniani. Wazazi wengi huchukua muda kufikiria ni jina gani zuri la kumpa mtoto wao.
Kuna wakati baadhi ya wazazi hufikia hatua ya kuvutana kuhusu jina tu. Kuvutana huko kunatokana na umuhimu wa jina kwa sababu inaaminika kila jina lina maana yake na tabia zake zitaakisiwa nalo.
Kuna majina ambayo hupendwa sana kutokana na dhana kwamba watu wanaopewa majina hayo huwa na tabia nzuri, upeo mkubwa, uvumilivu na wengine bahati.
Je, ikitokea unabahatika kupata mtoto wa kike uliyemtafuta kwa muda mrefu, utampa jina gani?
Huenda jina Janeth likawa miongoni mwa matatu au 10 utakayoorodhesha ili kuchagua moja la kumpa binti yako. Kama halitakuwapo basi fanya mpango wa kuliweka kwa sababu jina hilo ndiyo habari ya mjini kwa sasa.(VICTOR)
Kwa nini jina la Janeth ni habari ya mjini?
Siku Dk John Magufuli alipopitishwa na CCM kuwania nafasi ya urais, baadhi ya watu walidai ikiwa angepata nafasi hiyo Afrika Mashariki ingeongeza idadi ya wake wa marais wenye majina ya Janeth. Imekuwa hivyo, mke wa Rais Magufuli aliyeapishwa jana anaitwa Janeth.
Mke wa Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni anaitwa Janet Museveni, na mke wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame anaitwa Jeanette.
Licha ya kwamba jina la mke wa Kagame linaandikwa tofauti na mengine, lakini matamshi ya majina hayo ni sawa.
Kwa mujibu wa kamusi ya Encyclopaedia jina la Jeannette, asili yake ni Ufaransa ndiyo maana linaandikwa tofauti na Janeth ambalo asili yake ni Scotland.
Kama hujui wakati jina Janeth hupewa mtoto wa kike kinyume cha jina hilo ambao hupewa mtoto wa kiume ni John. Kwa hiyo majina ya Janeth na John Magufuli yameshabihiana vilivyo.
Kutokana na utuki huo majina ya wake za marais hao sasa yamekuwa habari ya mjini. Kuna baadhi ya watu wanatamani kuwapa majina watoto wao kwani huenda wakawa ‘ma First Lady’ watarajiwa.
Gumzo kwa sasa au watu wengi wanahoji iwapo marais hao watakutana wakiwa na wake zao, likataitwa jina hilo, itakuwaje?
Maana ya jina Janeth
Kwa mujibu wa kamusi ya tafsiri ya majina, jina Janeth (Kiebrania) ambalo asili yake ni Uingereza linamaanisha Mungu ni mwenye neema.
Sifa za wanawake wenye jina hilo zimedadavuliwa zaidi na tovuti ya ‘sevenreflections’.
Tovuti hiyo inawaelezea wanawake wenye jina hilo kuwa ni waaminifu, wema, wenye vipaji na wavumbuzi wa mambo.
Wanawake wenye majina hayo ni jasiri, wavumilivu, wabunifu, wadadisi, wanafahamu nini wanataka, siyo tegemezi na viongozi wazuri.
Janeth Magufuli
Kitaaluma ni mwalimu. Alikuwa anafundisha Shule ya Msingi Mbuyuni masomo ya Jiografia, Historia na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Lakini ameacha kutokana na wadhifa huo mpya aliopata mumewe. Hata hivyo, hakuwa maarufu wakati alipokuwa anafundisha shuleni hapo licha ya kuwa mke wa waziri mchapakazi na sasa rais.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Dorothy Malecela anamzungumzia kama mwalimu mchapakazi na anayefahamu majukumu yake, mwenye upendo, mnyeyekevu na asiye na makuu, sifa ambazo zinaendana na jina lake.
Janet Museveni
Licha ya kuwa Mke wa Rais Museveni tangu mwaka 1986 mumewe alipoingia madarakani, pia ni mwanasiasa, na ni Waziri wa Karamoja.
Jeannette Kagame
Alipata wadhifa wa mke wa rais tangu mwaka 2000, Kagame alipoingia madarakani hadi sasa akiwa pia mwanaharakati, mwanzilishi wa taasisi ya Imbuto inayosaidia katika shughuli za maendeleo katika sekta ya afya, elimu na uchumi.
Mwanamke mwingine maarufu duniani mwenye jina hilo ni Janeth Jagan, aliyekuwa Rais wa Guyana kati ya mwaka 1997 na 1999.
Source: Mjengwa Blog
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment