Wananchi wa Burkina Faso wanapiga kura leo kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza katika kipindi cha zaidi ya miongo miwli.
Huu ndio uchaguzi wa kwanza wa huru na wa haki tangu maandamano ya raia kumng'oa madarakani rais wa miaka mingi, Blaise Compaore.
Uchaguzi huo ulipangwa kufanywa mwezi uliopita, lakini uliahirishwa kwa sababu ya jaribio la mapinduzi lilofanywa na maafisa wa kikosi cha kumlinda rais mwezi wa Septemba.
Uchaguzi huu ndio mwisho wa wa kipindi cha mpito, kilichofuata baada ya Rais Compaore kutolewa madarakani.
Waandishi wa habari walioko huko wanasema, unaweza kuwa ndio huru na wa haki kabisa katika historia ya Burkina Faso.
Usalama umeimarishwa kote huku zaidi ya maafisa 25,000 wakitumwa kote nchini kuhakikisha usalama.
''Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 50 kuna wasiwasi wa kujua nani atakuwa kiongozi mpya wa Burkina Faso.,,,,hatujui nani atakuwa rais mpya anasema Abdoulaye Somamkurugenzi wa wakfu wa kupigania katiba.
''Hili ni jambo la kujivunia na ishara nzuri kuwa mabadiliko yameanza kutekelezwa haswa katika mfumo wa uchaguzi''aliongezea kusema.
Wagombea 14 wanawania kiti cha urais baada ya kufurushwa kwa Compaore.
Duru katika taifa hilo hata hivyo zinaashiria kuwa bwana Roch Marc Christian Kabore na Zephirin Diabre ndio wanaopigiwa upatu kuwa na ungwaji mkono mkubwa miongoni mwa raia.
Bwana Diabre ambaye ni msomi na mtaalamu wa maswala ya kiuchumi amewahi kuhudumia taifa hilo kama waziri wa fedha na uchumi kabla ya kutofautiana na rais Campaore mwaka wa 2010.
Bwana Kabore kwa upande wake aliwahi kuwa waziri mkuu vilevile katika utawala wa Campaore mbali na kuwa mwenyekiti wa chama cha Congress for Democracy and Progress (CDP).
Hata hivyo Kabore alikihama chama hicho mwaka wa 2014 baada ya kukataa kuunga mkono kubadilishwa kwa katiba ya nchi ilikumruhusu rais Campaore kuendelea kutawala hata baada ya kukamilika kwa muhula wake .
Endapo wapiga kura wa Burkina Faso hawatamua nani kati ya wagombea 14 wa urais ataingia ikulu katika mkondo wa kwanza, tume ya uchaguzi italazimika kuandaa mkondo wa pili wa upiga kura kati ya mshindi wa kwanza na wa pili.
Shughuli ya upigaji kura itakamilika mwendo wa saa kumi na mbili jioni majira ya Afrika ya Magharibi sawa na saa tatu Afrika Mashariki.
Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kuanza kutolewa jumatatu jioni.
Source: www.bbc.com/swahili
0 comments:
Post a Comment