Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kumtangaza mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mwishoni mwa juma, Zitto alidai katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mshindi alikuwepo, hivyo ZEC watumie busara na kuepusha shari kwa kumtangaza mshindi.
“Na wangefanya mapema tu, wamtangaze Maalim Seif aunde Serikali, naamini wakifanya hivvyo, hawatapoteza chochote maana kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar wataendelea kuwa ndani ya Serikali ya Mseto,” alisema Zitto.
Alisema hakuna namna CCM inaweza kuishinda CUF Zanzibar hata kama uchaguzi utarudiwa na kushauri ni vema watu wakaanza kujiandaa kisaikolojia kwa kukubali matokeo yaliyopo.
Wakati Zitto akisema hayo, tayari ZEC imekwishatangaza katika Gazeti la Serikali kuwa uchaguzi huo umefutwa rasmi na utarudiwa kabla ya Februari.
Zitto ambaye ni mbunge pekee kutoka ACT, alisema vipo viashiria vingi vinavyodhihirisha ushindi wa Maalim Seif katika uchaguzi uliopita.
Alitaja kitendo cha CUF kuvunja ngome ya CCM Unguja kwa kunyakua viti tisa badala ya viwili ilivyokuwa ikipata katika chaguzi zilizopita, kuwa ni moja ya kielelezo kuwa chama hicho cha upinzani hakishikiki tena Zanzibar.
“Hili halikuwahi kutokea katika chaguzi zilizopita. Katika chaguzi zote CUF imekuwa ikiambulia viti viwili au visivyozidi vinne huko Unguja, lakini sasa tunaona wamepata viti tisa, hata kama wakirudia uchaguzi na CUF wakaamua kushiriki, lazima watashinda,” alisema.
Zitto anasema ushindi wa CUF Zanzibar kuwa ni CCM kupoteza viti vyake vya udiwani Pemba. Alisema chama hicho kimekuwa kikipata viti vitano vya udiwani kiswani humo, lakini katika uchaguzi huu hakikuambulia kitu.
“CCM walikuwa na madiwani Pemba sasa hawana hata mmoja, yaani hakuna jinsi watashindwa Zanzibar. Wanachokifanya ni kujidanganya mpaka watakapogundua hawana hiyo nguvu tena ndipo watakapoachia madaraka,” alisema.
Hata hivyo, Zitto alisema changamoto anayoiona ni suala la kikatiba ambalo linasema mtu akishakuwa Rais wa Zanzibar anakuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano.
“Changamoto ninayoiona hapa ni pale Katiba inapotoa ruksa kwa Rais wa Zanzibar kuingia kwenye Baraza la Mawaziri la Muungano. Hii itasababisha kuwapo kwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano ambaye siyo CCM,” alisema.
Alihoji: “Ikitokea hivyo wataendeshaje? Maana katika Baraza la Mawaziri, sera zinazotekelezwa ni sera ya chama ambacho kinaongoza Serikali ambacho ni CCM.”
Zitto alisema anachokiona ni kuwa huenda CCM wakalazimika kuingia makubaliano mengine na CUF upande wa Tanzania Bara ili kuunda Serikali ya Mseto.
Zitto anatabiri kuwa endapo Maalim Seif atatangazwa kuwa Rais wa Zanzibar hali ya kisiasa itabadilika nchini kutokana na upinzani kuwa na mtu ambaye tayari anaendesha Serikali kama Rais.
“Wapinzani wanaweza wakaitumia nafasi hiyo vizuri na kujikuta wakiwa na nguvu kubwa,” alisema.
Kwanini hakuungana na Ukawa
Akizungumzia kwanini alibaki ndani wakati Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alipokuwa akiingia bungeni siku ambayo Rais John Magufuli alipolihutubia Bunge, Zitto alisema alifanya hivyo kwa kuwa hamtambui kiongozi huyo.“Sikumtambua Dk Shein nikaamua kukaa, alipoingia Rais Magufuli nikasimama kwa sababu namtambua, kwa maoni yangu Ukawa walikuwa sahihi mpaka Shein alipokaa, walipaswa kuishia pale,” alisema Zitto.
Source: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment