CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimekanusha taarifa zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii kwamba kimeridhia mgombea urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuapishwa na kukabidhiwa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ofisi Kuu Kisiwandui mjini hapa, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema taarifa hizo zilizorushwa katika mitandao ya kijamii, si za kweli na zimelenga kuwavunja moyo wafuasi na wanachama wa chama hicho tawala Tanzania.
Vuai alisema CCM haijaridhia Maalim Seif kuapishwa kwa sababu inachofahamu ni kwamba Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu umefutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Alisema uchaguzi huo umefutwa baada ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali za ukiukwaji wa sheria ya uchaguzi na kuufanya kuwa sio huru na haki.
“Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kinakanusha vikali kwamba hakijaridhia kuapishwa kwa Maalim Seif kuwa Rais wa Zanzibar kwa sababu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 umefutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,” alisema Vuai.
Katika taarifa iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, ilisema kwamba Chama Cha Mapinduzi pia kimeridhia Dk Ali Mohamed Shein kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Juzi baada ya taarifa hiyo kuchapishwa katika mitandao ya kijami ikiwa na saini ya kughushi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, baadhi ya wananchi wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa CUF walionekana kujikusanya katika vikundi mbalimbali huku wakifurahia taarifa hiyo.
Aidha, taarifa zilizozagaa za kuwepo kwa maandalizi ya kuapishwa kwa Maalim Seif, zimezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanachama na wafuasi wa CCM ambao wamekuwa wakifika mara kwa mara katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui na kutaka kupewa ufafanuzi wa suala hilo.
Vuai alisema CCM inachofahamu ni kwamba mazungumzo ya kuleta mwafaka wa makubaliano yanaendelea ambapo hata hivyo hayatakuwa mbadala wa kubadilisha sheria za nchi kwani suala la kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu limetangazwa na Tume ya Uchaguzi na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.
0 comments:
Post a Comment