>> Aponzwa na ufisadi wa TRA, Bandari
>> Zuio safari za nje laanza kung’ata
Imechapishwa jana. Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
RAIS Dk. John Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah kwa kile alichodai mwenendo wa utendaji kazi wake hauendani na kasi yake anayoitaka.
Dk. Hoseah anakuwa kigogo wa 79 kutoka taasisi nne za umma ambao tayari wameonja machungu ya Serikali ya awamu ya tano na kaulimbiu yake ya ‘hapa kazi tu’.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ilisema Rais Magufuli amefikia uamuzi huo kutokana na namna taasisi hiyo ilivyotekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa, hususani kwenye upotevu wa mapato ya Serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema kutokana na hatua hiyo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Valentino Mlowola kukaimu nafasi hiyo.
“Rais Magufuli amechukua hatua hii baada ya kujiridhisha kuwa utendaji kazi wa Takukuru chini ya Dk. Hoseah hauwezi kuendana na kasi anayoitaka.
“Eneo mojawapo la upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali, ni bandarini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)…Rais amesikitishwa na kitendo cha taarifa za kuwapo vitendo vya rushwa katika eneo hili kwa muda mrefu, lakini kasi ya Takukuru kuchukua hatua haiendani na kasi anayoitaka,” alisema Balozi Sefue.
WATUMISHI WALIOSIMAMISHWA
Katika hatua nyingine, Balozi Sefue alisema Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa taasisi hiyo ambao walisafiri nje ya nchi, licha ya kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma.
Watumishi hao, ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas, ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka kwa rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
Kutokana na hali hiyo, Balozi Sefue amewataka watumishi wengine wa umma kutii agizo la Rais Magufuli na kuonya atakayekiuka atachukuliwa hatua kali.
Kabla ya wafanyakazi hao wanne kusimamishwa jana, habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilikuwa nazo, zinasema walisafiri kwenda nchini Zambia kuhudhuria warsha bila kibali cha Ikulu.
Wafanyakazi hao, wanadaiwa kuondoka nchini Novemba 23, mwaka huu, licha ya kunyimwa kibali.
Takukuru iliiandikia Ikulu barua ya kuomba kibali kwa ajili ya safari hiyo, lakini kabla ya kujibiwa wafanyakazi hao waliamua kusafiri.
Novemba 7, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza kufuta safari za nje ya nchi kwa maofisa wa Serikali, ila tu itakapokuwa lazima na kwa ruhusa ya Ikulu.
KASI YA MAGUFULI
Kasi ya Dk. Magufuli ilianza kuonekana siku moja tu baada ya kuapishwa Novemba 5, ambapo alifanya ziara ya kushtukiza kwenye Wizara ya Fedha Novemba 6.
Novemba 9, alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukuta mashine ya MRI na CT-Scan hazifanyi kazi jambo lililomfanya avunje bodi ya wadhamini ya hospitali hiyo iliyokuwa na wajumbe 11.
Mbali na kuvunja bodi hiyo, Rais Magufuli alimsimamisha kazi Dk. Hussein Kidanto aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukurugenzi wa hospitali hiyo na kumrudisha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jami.
Baadaye Novemba Novemba 27, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kukutana na uozo mkubwa uliosababisha kusimamisha maofisa 36 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Vigogo hao ni pamoja na Kamishina Mkuu wa TRA, Rished Bade aliyesimamishwa na Dk. Magufuli.
Katika kile kilichoonekana kwamba ni upepo wa Dk. Magufuli, Desemba 6, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilisimamisha maofisa saba kwa kile kilichodaiwa ni kutokana na makosa mbalimbali ikiwamo wizi na ubadhirifu.
Kasi ya Dk. Magufuli iliendelea tena Mamlaka ya Bandari (TPA) ambako alifyeka vigogo 23 ikiwa ni pamoja na kuvunja bodi ya mamkala hiyo.
Rais Magufuli, alitengua uteuzi wa mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Joseph Msambichaka na mkurugenzi wake, Awadhi Massawe kutokana na upotevu wa zaidi ya makontena 2,300.
PROFESA BAREGU
Akizungumzia uamuzi uliochukuliwa na Dk. Magufuli ndani ya Takukuru, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu, alisema umedhihirisha kuwa Rais Magufuli ana taarifa za kina za kila mtumishi wa Serikali.
“Kwa sababu hii, watumishi wasibweteke wakidhani rais hajui chochote, ni ukweli ulio wazi kuwa Takukuru ni taasisi ambayo imekuwa ikipigiwa kelele mno kwa kushindwa kuchukua hatua zozote kuhusu kashfa mbalimbali.
“Kulikuwa na kashfa za Escrow, EPA na nyingine nyingi ambazo zote ukichunguza huoni nini kilichofanywa na taasisi hii katika kushughulia matukio hayo.
“Lakini pia inawezekana vigogo hawa wameondolewa kwa kukiuka masharti au maagizo ya rais kwamba wasisafiri, wao wakasafiri, hivyo yamkini wameondolewa kutokana na kasoro za kiutendaji,” alisema Profesa Baregu ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT).
- BANA
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema hatua ya Rais Magufuli imelenga kuibua watumishi watakaoendana na kasi ya utendaji kazi wake.
“Anataka mtumishi atakayeendana na kasi ya kauli zake, nadhani amekuwa akizungumzia sana suala la uadilifu, amekuwa katika mchakato mzito wa kuhakikisha hakuna makandokando yanayobaki katika Serikali yake.
“Tumpongeze Dk. Hoseah kwa hatua aliyofikia, amefanya kazi nyingi, ukweli ni kwamba alikuwa mtumishi wa umma hivyo lazima siku moja angekaa kando,” alisema.
PROFESA MKUMBO
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo, alisema suala la Dk. Hoseah kutakiwa kuondolewa kwenye taasisi hiyo lilikuwa wazi.
Alisema hiyo ni hatua njema kwa Magufuli ili aweze kupata nafasi ya kujipanga vizuri katika safu yake kiutendaji.
Mtanzania
0 comments:
Post a Comment