Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba amesema wanachama wa chama hicho watakaoguswa na kasi ya utendaji wa Rais John Magufuli, waache kulalamika kwa sababu ana lengo la kuijenga Tanzania mpya.
Katika taarifa yake ya chama kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Makamba alisema wapo wanaCCM maslahi yao yatagushwa na kasi hiyo, hivyo wasilalamike bali wakae na kujitathimini kama walichokuwa wakikifanya kina faida kwa Taifa na Watanzania.
Alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kwa kila mwanachama kuunga mkono kila hatua anazochukua Rais Magufuli za kutaka kuleta mabadiliko ya kweli yanayotakiwa na Watanzania wote.
“Tusikae kimya, hii ni vita ninaamini Watanzania wote wanamuunga mkono lakini kwa kuwa anatekeleza ahadi za chama chetu, tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kumuunga mkono kwa kauli na vitendo,” alisema Makamba.
Alisema katika kipindi kifupi alichokaa ofisini, Rais Magufuli ameonyesha utendaji uliotukuka kiasi cha kuzua ari ya matumaini mapya kwa Tanzania inayoitakiwa na wananchi. Alisema tayari ameanza kuziba mianya ya upotevu mapato ya nchi na kuchukua hatua ya kupunguza matumizi ya fedha za Serikali yasiyo ya lazima.
Hadi sasa, Rais Magufuli ametekeleza baadhi ya ahadi zake alizoahidi alipokuwa akiwaomba ridhaa Watanzania ya kuongoza nchi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 25.
Source: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment