WATATU WASIMAMISHWA KAZI BANDARI

Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa TPA, Janeth

Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa TPA, Janeth Ruzangi. 
By Nuzulack Dausen, Mwananchi
Dar es Salaam. Mapya yamezidi kuibuka katika sakata la upotevu wa makontena 349 na ukwepaji kodi, baada ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuwasimamisha kazi maofisa wake watatu kupisha uchunguzi.
Mbali na kusimamisha watumishi hao wanaohusika na usimamizi wa shughuli za Bandari kavu, TPA pia imepoteza mapato katika sakata hilo lilisababisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupoteza Sh80 bilioni.
Hatua hiyo ya TPA kuwasimamisha watumishi wake imekuja mara baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini upotevu wa mizigo hiyo.
Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Janeth Ruzangi alisema jana katika mahojiano kuwa maofisa hao watatu walisimamishwa Jumamosi ya wiki iliyopita, ikiwa ni siku moja baada ya ziara ya Majaliwa.
“Kama sehemu ya uwajibikaji, tumewasimamisha ofisa mkuu wa kitengo kinachosimamia ICD na makarani wawili ili kupisha uchunguzi.
“Uchunguzi huo unaendelea ili kufahamu iwapo walihusika na upotevu huo ama la au walijua au hawakufahamu suala hilo,” alisema Ruzangi huku akikataa kuweka bayana majina ya watumishi hao.
Kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha muongozo wa gharama za bandari wa mwaka 2013, mizigo yote ya ndani inayopitia bandarini hutozwa asilimia 1.6 ya thamani ya mzigo iliyobainishwa na TRA wakati ile ya nje hutozwa asilimia 1.25 katika tozo ijulikanayo kama “wharfage”.
Hata hivyo, katika makontena hayo 349 TPA ilipata mapato yaliyohusu usimamizi pekee wa ushushaji wa mizigo hiyo huku ikipoteza yale yanayotegemea tathmini ya TRA, ambayo kwa taarifa ya Waziri Mkuu haikufanyika kiasi cha Serikali kupoteza Sh80 bilioni kama kodi.
Ruzangi alisema fedha zilizotajwa kupotea kama ukwepaji kodi katika upotevu wa makontena hayo, hazihusu mapato ya Bandari.
“Ni kweli hayo mapato ya awamu ya pili bila shaka na sisi tuliyakosa,” alisema Ruzangi alipoulizwa kupoteza kiasi hicho cha fedha ambacho alibainisha ni asimilia 1.6 ya Sh80 bilioni ambazo ni thamani inayodai TRA.
Alisema Sh934.5 milioni zimepotea kama mapato ya bandari katika sakata hilo linaloihusisha Kampuni ya Bandari Kavu ya Azam. Hata hivyo, menejimenti ya Azam juzi ilikana kumiliki mali yoyote ya shehena hiyo, zaidi ya kueleza kuwa makontena hayo yalikuwa ya wateja na kwamba walikuwa wakitoa ushirikiano kufanikisha uchunguzi.
Ruzangi alisema makontena hayo 349 yaliingia kati ya Mei na Oktoba mwaka huu na kwamba upotevu huo ni mkubwa kuwahi kutokea katika historia ndani na nje ya bandari ukifuatiwa na upotevu wa makontena 21 ya vitenge mwaka 2012.
“Bandari yetu kwa sasa ni salama hakuna wizi tena kama miaka ya nyuma. Kwa sasa tunafunga kamera za ulinzi 485 eneo lote la bandari, kufunga wavu kwenye kuta na kuimarisha mfumo wa kielektroniki wa ulinzi magetini,” alisema.
Ruzangi alisema mfumo wa Tehama wa TPA hauingiliani na ule wa TRA uitwao Tancis, jambo ambalo baadhi ya wadau wanahisi ilitumika njia ya kutumia udhaifu huo kukwepa mapato, lakini akaeleza mfumo unaoingiliana utaanza kazi mwakani.
Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakala wa Shehana na Forodha, (TAFFA), Edward Urio alisema katika sakata hilo, TRA ndiyo wanahusika zaidi kutokana na kusimamia mchakato mzima wa uingizaji wa mzigo.
“Mali zote zinazoingia ni za TRA. Sitegemei bandari wawe na rekodi, halafu TRA wasiwe nazo,” alisema Urio.
“Kuna wasiwasi huenda rekodi za mzigo huo zilifutwa au hazikuingizwa kabisa japo taarifa za mzigo huwafikia mapema kabisa kutoka kwa kampuni ya meli inayosafirisha,” alisema.
Urio ambaye huusika na biashara ya uwakala wa shehena na forodha, alisema Bandari Kavu zimekuwa zikiendesha biashara zao kwa makandokando mengi yakiwemo kuongeza gharama zisizokuwa na mashiko.
Tayari watumishi tisa wa TRA wakiongozwa na Kamishna Mkuu wa mamlaka hayo, Rished Bade wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa sakata hilo la kwanza katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli.
Source: Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment