ZITTO AIBUA UFISADI WA TRIL. 1.2/-

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama hicho, amesema Taasisi ya Serious Fraud Office ya nchini Uingereza (SFO), inafanya mazungumzo na Benki ya Standard Group ya Afrika ya Kusini kuhusu tuhuma za rushwa zinazotokana na ununuzi wa dhamana za Serikali ya Tanzania (bonds) zenye thamani ya sh. trilioni 1.2.


Katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Zitto alisema ni jambo la kawaida kwa Serikali yoyote duniani kuuza dhamana zinazofahamika kama hati fungani ambapo mwaka 2011/12, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha iliuza hati fungani kwa dola za Marekani milioni 600.


Alisema dhamana hizo zilinunuliwa na benki ya kigeni (Stanbic) ambayo ni mali ya Standard Group ya Afrika ya Kusini, yenye Makao Makuu yake London, nchini Uingereza.

Alisema kuwa cha ajabu ni kwamba sehemu ya fedha hizo haikuingia kwenye akaunti za Serikali ya Tanzania na gharama za hati fungani zilipaishwa kupitia Wakala wa katikati hivyo kusababisha rushwa ya dola za Marekani milioni 60 kutolewa kwa maafisa waliothibitisha biashara hiyo.

"Taasisi za kiuchunguzi nchini Uingereza ikiwemo inayoshughulikia makosa ya rushwa (Serious Fraud Office-SFO), tayari imefanya uchunguzi wa awali kwa kuhusisha pande zote zinazohusika na wamegundua kuwepo kwa rushwa kubwa katika mchakato huo.
"Jambo hilo liliwafanya washauri wa benki hiyo nchini, kuondolewa na kurejeshwa Uingereza kwa hatua zaidi...SFO na Standard Group wanataka kulimaliza jambo hili kama walivyomaliza suala la rada,” alisema.

Kabwe alisema, chama chake kinazitaka mamlaka za kiuchunguzi nchini, kuwachukulia hatua na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wote waliohusika na upotevu wa sh. trilioni 1.2 katika sakata hilo. Alisema fedha hizo ni nyingi sana ikilinganishwa na makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); hivyo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na FIU Tanzania, waweke hadharani taarifa ya uchunguzi wao, kueleza kwa nini hawajachukua hatua hadi sasa.

"ACT-Wazalendo, tunaunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli za kutumbua majipu hivyo tungependa kuona akichukua hatua katika jambo hili ambalo lina masilahi mapana ya nchi yetu hasa ikizingatiwa uzoefu tulionao katika masakata kama haya yanayohusisha nchi za kigeni.

"Mfano mzuri ni sakata la rada ambalo vyombo vyetu vya uchunguzi vilisema hakukuwa na rushwa, baadaye Serikali ya Uingereza ilithibitisha pasipo na shaka kuwa kulikuwa na rushwa, Serikali yetu ilirudishiwa sehemu ya fedha zilizozidi katika manunuzi,” alisema Kabwe.


Aliongeza kuwa, chama hicho kinasubiri taarifa ya makubaliano kati ya SFO na Benki ya Standard Group (Benki mama ya Stanbic) ili kushauri zaidi hatua za kuchukua.

"Ikumbukwe kuwa, Benki ya Stanbic ndiyo ilihusika na kashfa ya Tegeta Escrow, hadi sasa haijachukuliwa hatua zozote kama ilivyoagizwa na Bunge kuwafichua waliochota fedha hizo, hadi leo kimya,” alisema. 

Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment