Dar es Salaam. CCM imesema kauli ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa wafadhili wa Chadema wananyanyaswa, ina lengo la kuichonganisha Serikali na walipa kodi na kumtaka ataje waliofanyiwa vitendo hivyo.
Juzi, Lowassa alikaririwa na vyombo vya habari kutoka Monduli akisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa maelekezo ya Serikali imekuwa ikiwatoza kodi kubwa wafanyabiashara kwa sababu waliifadhili Chadema kwenye kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.
Lowassa aliwahi kutoa kauli kama hiyo jijini Mwanza akiwa kwenye msiba wa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema wa mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo aliyeuawa kwa kushambuliwa kwa mapanga.
Pia wakati wa harambee ya Chadema iliyofanywa Septemba 22 mwaka jana, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema kulikuwa na matajiri watano wenye uwezo kiuchumi ambao walikuwa tayari kukisaidia kwenye shughuli zake za kampeni, lakini hawataki kutajwa majina yao kwa hofu ya kufuatiliwa na vyombo vya dola.
Jana, akizungumza na waandishi wa habari jijini, Abdallah Bulembo, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, alisema kauli ya Lowassa haina ukweli wowote na kwamba ina lengo la kuigombanisha Serikali na walipakodi ambao wanahitajika sana kipindi hiki.
“Kama kweli Lowassa anawafahamu wafanyabiashara au kampuni ambazo zinatozwa kodi kubwa kwa sababu walikuwa wamekifadhili chama hicho, basi ni vizuri awataje ili wajulikane na waseme wao wenyewe,” alisema Bulembo ambaye wakati wa kampeni alikuwa bega kwa bega na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli.
Akijibu suala hilo, Lowassa alisema kuna wafanyabiashara wengi waliokuwa wakikifadhili chama ambao wanalalamika kutozwa kodi kubwa.
“Kuna watu wengi wanalia kutozwa kodi kubwa,” alisema Lowassa ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema baada ya kuihama CCM Julai mwaka jana.
“Suala hapa si kuwataja majina, mkihitaji majina yao fanyeni research (utafiti) mtawapata. Lakini mfahamu kwamba kuna tatizo hilo.”
Alisema ana uhakika vyombo vya habari vitawapata watu hao na kwa kuwa ni wengi watatoa malalamiko yao.
Akifafanua zaidi, Bulembo alisema kauli ya Lowassa inadhoofisha nguvu ya Rais Magufuli ambaye ameongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh850 alipoingia madarakani hadi Sh1.3 trilioni kwa mwezi.
“Tunawahitaji walipakodi wengi wakati huu kwani tunahitaji kupata fedha zaidi ili kutekeleza ahadi tulizowaahidi wananchi. Kauli ya Lowassa inatugombanisha na walipakodi,” alisema.
Alisema anachofahamu ni kwamba kodi inatozwa bila kumpendelea mfadhili wa CCM au kumwonea mfadhili wa Chadema.
“Masuala ya vyama ya siasa yameshapita, sasa hivi ni kujenga nchi na kodi inatozwa bila kuangalia vyama vya siasa,” alisema Bulembo.
Alimwomba Lowassa kumsaidia Magufuli katika kazi ya kutafuta mapato ili kuwaletea wananchi maisha mazuri
“Namwomba Lowassa tujenge nchi yetu, huu si wakati wa kufanya siasa, asubiri mwaka 2020 kama atagombea tena urais tutakutana kwenye majukwaa,” alisema.
Alisema kuendelea kupigana vijembe kipindi hiki ni kurudisha nyuma maendeleo ambayo yanahitaji zaidi walipakodi.
“Kodi zina vipimo vyake kama kuna watu wameonewa ukweli utajulikana,” alisema Bulembo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Alisema Serikali ya CCM itaendelea kutenda haki kwa wananchi wake ili kukiwezesha chama hicho kushinda uchaguzi kwa kishindo mwaka 2020.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, mkurugenzi wa idara ya elimu na huduma kwa walipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema mamlaka hiyo haijapata malalamiko yoyote.
Alisema mamlaka hiyo inafanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na haifanyi kazi kwa kufuata maagizo ya vyama vya siasa.
“Sisi hatuko kwenye siasa tunafanya kazi zetu kwa kuongozwa na sheria na kanuni. Hatumwonei mtu wala kupendelea,” alisema.
Kauli kama ya Lowassa ilitolewa pia na mkuu wa idara ya habari ya Chadema, Tumaini Makene aliyesema hoja ni kueleza kuwapo kwa tatizo ambalo halitaishia kwenye ubaguzi wa kiitikadi.
“Ukianza kubagua watu kivyama, huwezi kuishia hapo. Utaanza kuwabagua kikabila, kikanda na hata kidini. Hii ni kinyume na ahadi ya Rais Magufuli kuwa atakuwa Rais wa watu wote,” alisema Makene.
Makene alitoa mfano wa kukataliwa kwa misaada ya vifaatiba katika zahanati za Serikali mkoani Kagera uliotolewa na mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare.
Mara baada ya kuingia Ikulu, Rais Magufuli alikutana na watumishi wa Hazina na kuwaelekeza kukusanya kodi bila ya kuangalia sura, huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifanya ziara za mara kwa mara bandarini ambako ameibua kashfa za ukwepaji kodi na upitishaji makontena kifisadi.
0 comments:
Post a Comment