Dar es Salaam: Mwanasheria wa kujitegemea nchini, Fatma Karume amemshauri Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein kuachia madaraka.
“Dk Shein lazima aondoke kwa sababu kuendelea kubaki madarakani ni kuwanyang’anya Wazanzibari haki yao ya msingi,” alisema Fatma ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Fatma alisema kuwa mzozo wa Zanzibar umesababishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufutwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo wakati hana mamlaka kisheria kufanya hivyo.
Fatma alisema Jecha hana mamlaka kikatiba na kisheria kufuta matokeo hayo kwa kuwa maamuzi kama hayo yanatakiwa kufanywa na ZEC yenye mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe watano; watatu kutoka CCM na wengine wawili kutoka CUF.
“Akidi ya vikao vya ZEC ni mwenyekiti na wajumbe wanne. Kama kikao kilifanyika, akidi ilitimia na jambo hilo likakubaliwa na tume hiyo, basi waonyeshe ni wapi walipokubali wajumbe wengine. Hata makamu mwenyekiti hajashiriki kwenye maamuzi hayo kwa sababu kisheria uchaguzi hauwezi kufutwa bila kupata akidi hiyo,” alifafanua Fatma.
Mwanasheria huyo alisema kuwa amekuwa akiwasikia baadhi ya wana CCM Zanzibar wakisema kuwa Jecha ndiyo tume na tume ndiyo Jecha, hivyo ana haki ya kufuta uchaguzi. Lakini Fatma alisema Jecha hana mamlaka kusema jambo ambalo halijakubaliwa na tume.
Alipoulizwa ikiwa hatua ya aliyekuwa mgombea urais kupitia CUF, Seif Sharrif Hamad ya kutangaza matokeo aliyodai yalimpa ushindi si kosa, Fatma alisema, “Sikumuona Maalim Seif alipokuwa anatangaza matokeo hayo hivyo sijui kama alijitangaza kuwa mshindi au alitangaza matokeo kama yalivyobandikwa kwenye vituo.
“Katika nchi zilizokomaa kidemokrasia mgombea anaweza kuona mwelekeo wa matokeo na akampigia mwenzake kumpongeza. Nadhani Maalim Seif alisoma jumla ya matokeo ya uchaguzi kama yalivyobandikwa kwenye vituo, hivyo hilo si kosa ati,” alisema na kuongeza: “Ninasikitishwa na tabia hii. Sikutegemea kama CCM watatumia nguvu kutaka kubaki madarakani kwa njia hii. Sikutegemea kama watavuruga katiba…ndiyo maana nina huzuni.”
Jambo jingine alilosema litazua mgogoro Zanzibar ni mamlaka yenye haki ya kuidhinisha fedha za uchaguzi wa marudio ikiwa watalazimisha ufanyike.
“Kisheria fedha hizo ni lazima zikubaliwe na Baraza la Wawakilishi. Baraza lipo wapi? Ili mtu awe waziri lazima awe mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Rais alivunja Baraza Agosti na kwa hiyo hadi ilipofika siku ya kuapishwa rais mpya, Zanzibar hakuna Baraza wala Waziri. Ina maana fedha za wananchi zinatumiwa bila idhini ya Baraza, ” alisema.
Alisema kinachofanyika Zanzibar ni ‘ukoloni’ wa watu weusi dhidi ya watu weusi ambao unawakosesha Wazanzibari haki yao msingi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.
“Hali si shwari Zanzibar. Watu wamekata tamaa kwa sababu unapokuwa na Serikali ambayo inanyang’anya haki ya wananchi ya kupiga kura, kuandamana, watu wanakosa imani na Serikali hiyo,” alisema.
Kurudia uchaguzi
Kuhusu kurudiwa uchaguzi nchi nzima, Fatma alisema ulipofanyika uchaguzi mwaka 2000 ambao Amani Karume aligombea kwa mara ya kwanza, zilitokea dosari katika majimbo 10 ya Unguja. CUF walipotaka uchaguzi urudiwe nchi nzima, CCM chini ya Benjamin Mkapa waligoma wakasema ni katika majimbo yenye dosari tu.
“Nini kimetokea mwaka huu? Kama dosari zilijitokeza Pemba kama wanavyodai kwa nini urudiwe Unguja? Kwa nini hawataki kutumia uamuzi wa mwaka 2000 wa kurudia maeneo yenye dosari tu?” alihoji.
“Mkapa alisema wazi kwenye kipindi cha Hard Talk cha BBC akihojiwa na mtangazaji Tim Sebastian uchaguzi hauwezi kufutwa ila utarudiwa tu katika baadhi ya majimbo. Kwa nini leo mambo yamebadilika na CCM inataka uchaguzi mpya?” alihoji.
Fatma ambaye alikataa kueleza msimamo wake kisiasa, alisema iwapo uchaguzi huru na wa haki utafanyika leo Zanzibar, CCM haiwezi kushinda kwa sababu Wazanzibari wanajionea yale ambayo wanafanyiwa na chama hicho.
“CCM imeshindwa Zanzibar kwa sababu ilishindwa kuwashawishi watu wake na badala inawakemea, ikawanyima haki zao. Kisaikolojia wapiga kura wanataka haki zao na wasibaguliwe lakini ukiwapelekea jeshi na vifaru, unazidi kuwapoteza,” alisema.
Sherehe za Mapinduzi
Wakati zikiwa zimesalia siku nne kufikia kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar, Fatma alisema kwa hali ilivyo haina maana kutokana na CCM kung’ang’ania kukaa madarakani kwa nguvu.
“Ninajisikia kusalitiwa. Madhumuni ya Mapinduzi haikuwa kuiweka CCM madarakani milele bali kurejesha madaraka kwa wananchi,” alisema.
Alisema aliambiwa kuwa waliofanya mapinduzi (wakiongozwa na Abeid Amani Karume) walitabiri kuwa ipo siku Zanzibar itakuwa na uchaguzi au Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini CCM hawataki.
“Wakati hao waliofanya mapinduzi wakisema hivyo, CCM haikuwepo, ilikuwepo ASP. Hao ASP hawakuwa wakijiaminisha kuwa watakaa madarakani milele,” alisema.
“Wakati tunaadhimisha mapinduzi ya Zanzibar, ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa malengo ya mapinduzi hayo yalikuwa ni kuondoa ubaguzi wa aina yoyote na kuweka misingi ya kidemokrasia lakini CCM wamevuruga,” alisema Fatma.
0 comments:
Post a Comment