MAALIM SEIF KUPASUA JIPU LEO

Seif_Sharif_Hamad
Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif  Hamad, leo anatarajia kufichua siri ya mazungumzo ya kusaka suluhu, baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kufutwa mwaka jana.
Habari za uhakika ambazo zimelifikia MTANZANIA jjini Dar es Salaam jana zinasema kwamba, Maalim Seif atakutana na waandishi wa habari kueleza kwa kina mwenendo wa mazungumzo hayo baina ya CUF na  CCM yalipofikia.
Maalim Seif, anachukua uamuzi huo wakati hali ya kisiasa visiwani humo ikizidi kuwa ngumu kwa pande zote, licha ya Rais Dk. John Magufuli kuahidi kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Maalim Seif anajitokeza leo, wakati wiki iliyopita Rais Magufuli  alikutana na  viongozi wastaafu, ambao kwa pamoja walizungumza mambo mazito ya kitaifa pamoja na kutakiana heri ya mwaka mpya.
Wiki iliyopita Rais Dk. Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye alimhakikishia kumpa ushirikiano atakapohitajika kufanya hivyo.
Katika kumhakikishia kuwa yuko tayari kufanyakazi atakayomtuma, taarifa za ndani zinaeleza kuwa moja ya jambo kubwa ambalo Mkapa anaweza kulisimamia ni suala la kusaka suluhu ya Zanzibar.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Mkapa alisema lengo la mkutano huo ni kumpongeza Rais Dk. Magufuli kwa dhamana aliyopewa na Watanzania na kumtakia heri ya mwaka mpya.
Mkapa alimhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wakati wowote na kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo.
Licha ya Mkapa, Rais Magufuli pia alikutana na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ambaye alikabidhi baadhi ya nyaraka kwa Rais Magufuli.
Kikwete alikabidhiwa nyaraka hizo zinazohusiana na mgogoro huo na aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, Novemba 4, mwaka jana.
Inaelezwa kuwa Maalim Seif alikabidhi nyaraka mbalimbali, zikiwamo fomu za matokeo ya Uchaguzi  Mkuu kwa vituo vyote vya Zanzibar.
Mbali na kukutana na watangulizi wake hao pia alikutana na aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba.
Katika mazungumzo hayo, licha ya Jaji Warioba, kumtakia heri ya mwaka mpya, alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri, lakini pia wakazungumzia mchakato wa Katiba mpya na hali ya kisiasa Zanzibar.
MAALIM KUUNGURUMA LEO
Naye Maalim Seif,  leo natarajia kuzungumza na waandishi wa habari kueleza hatima ya mazungumzo ya kisiasa ya kutafuta mwafaka Zanzibar
“Maalim Seif kesho (leo), atazungumza na wahariri na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa mazungumzo ya maridhiano Zanzibar,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana.
Dk. Shein na Magufuli
Desemba 24, mwaka huu Rais Magufuli alikutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu, Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa mazungumzo hayo na hali ya kisiasa visiwani humo.
Mazungumzo hayo yalifanyika, ambapo taarifa ya kukutana kwa viongozi hao ilitolewa kwa vyombo vya habari jioni na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.
Taarifa hiyo ilieleza baada ya mazungumzo ya viongozi hao, Rais Shein alieleza kuwa lengo la mazungumzo yao ilikuwa ni kumpa taarifa Rais Magufuli kuhusu hali ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa Zanzibar.
Taarifa ilieleza kuwa Dk. Shein alisema mazungumzo hayo  yanaendelea vizuri chini ya Kamati Maalumu ya kutafuta suluhu iliyopo chini ya uenyekiti wake.
Mbali ya Dk. Shein, wajumbe wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Rais mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Wengine ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume na Rais Mstaafu wa awamu ya tano wa Zanzibar, Salmin Amour.
Dk. Shein alisema amemtaarifu Rais Magufuli kuwa kamati yake ilianza mazungumzo Novemba 9, mwaka huu  na hadi sasa bado inaendelea na kazi yake.
“Nimekuja kumpa taarifa Rais Magufuli kuhusu maendeleo ya mazungumzo yetu ili aweze kujua kinachoendelea akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu yake, na sisi ni jukumu letu kumpa taarifa,” ilieleza taarifa hiyo.
Kabla ya kukutana na Rais Shein, tayari Desemba 21, mwaka jana Rais Magufuli alikutana na Maalim Seif, Ikulu Dar es Salaam na kuzungumzia mgogoro huo wa Zanzibar.
TAASISI NA UCHAGUZI
Wiki iliyopita, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) na Taasisi za Kiislamu zilitoa waraka  kwa pamoja zikipinga kurudiwa Uchaguzi visiwani humo, kwa hoja kuwa  hazioni busara yoyote kwa  sababu Uchaguzi wa awali ulifanyika kwa ufanisi wa hali ya juu.
Waraka wa viongozi wa dini ya Kiislamu uliosainiwa na Katibu Mtendaji wa JUMAZA, Muhidin Z. Muhidini, ambaye ulisema Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana  ulikuwa na waangalizi katika majimbo yote ya Unguja na Pemba na kasoro zilizoripotiwa ni ndogo mno, ikilinganishwa na Uchaguzi wowote uliopita tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe mwaka 1992.
KARUME
Kwa upande wake, mwanadiplomasia wa siku nyingi, Balozi Ally Abeid Karume amejutia kitendo kilichofanywa CCM kukubaliana na viongozi wa CUF  kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Akizungumza wakati wa kongamano lililoandaliwa na vijana wasomi wanaounda Shirikisho la Wasomi wa Elimu ya Juu wa CCM jana, Ally ambaye pia ni mtoto wa kwanza wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume alisema kitendo hicho ndicho kinachowapa shida CCM hadi leo.
“Nafikiri tulikurupuka, waliposimamia viongozi wetu waliteleza kwa sababu hawakupata maoni ya wanachama juu ya suala hili, chama kinachoshinda kijenge Serikali na wale wengine wabaki kuwa wapinzani… imani yao ilikuwa tuwe kitu kimoja, haki na amani ipatikane, imekuwa sivyo.
“Tumejikuta wenzetu tumewapa uwezo, umaarufu, nyezo katika uchaguzi wameleta shida. Waziri Kiongzi Mstaafu ‘Shamsi Vuai Nahodha’ niliwahi kukwambia siku moja  katika miaka mitano iliyopita, walianza kusema hakuna SUK, bali  ipo ya CUF na hadi wakurugenzi walisema wa kwao hadi uchaguzi umesimamiwa na wao. Hakuna utaratibu huo duniani.
“Tuliteleza tukafika huko tulipofika, mkiona mmeharibikiwa lakufanya si kunyoosheana vidole, bali kurekebisha pale ambapo tuliona haikutusaidia,”  alisema.
Aliwataka Wazazibari kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni ili CCM ipate ushindi wa kishindo.
“Tujitokeze kwa wingi ili tushinde kwa kishindo,baada ya hapo turekebishe Katiba kwa sababu tatizo hili linatokana na Katiba lazima ieleze kwamba Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi lazima atokane na CCM, ingawa vyama vyote vya siasa vitaruhusiwa kushiriki uchaguzi na kubakia wapinzani  kama ambavyo Uingereza inafanya kiongozi anatoka katika familia ya Malikia na hakuna malalamiko,” alisema.
NAHODHA
Kwa upande wake, Waziri Kiongozi Mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha alisema silaha kubwa itakayowakomboa Wazanzibari wakati wakitafakari mapinduzi ni elimu.
“Binafsi ninapotafakari juu ya mapinduzi leo, yapo mambo yanayonitia shaka juu ya uwezo na dhamira yetu ya kuyadumisha, unaweza kuwa na uwezo usiwe na dhamira au ukawa na dhamira huku uwezo huna lazima haya yaende sambasamba.
“Wapo baadhi yetu tukizungumza namna ya kuyadumisha wanadhani kazi yetu kama vijana na viongozi ni kudumisha vielelezo vya mapinduzi kama vile majengo ya maendeleo yaliyojengwa vijijini na michenzani.
“Nilikwenda China mwaka 2003, walikuwa na nyumba kama zetu za wanyonge, nikaenda tena 2011 sikuziona, nilipoenda 2013, nikakuta wamejenga majengo mengine ndio maana nasema sisi kazi yetu si kudumisha vielelezo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Zainab Abdalah alisema wataendelea kutoa ushirikiano kwa Rais Dk. John Magufuli kwa kumwonesha majipu makubwa na kuyatumbua yale madogo.
Alisema wataendelea kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwaelimisha Wazanzibari wote juu ya umuhimu wake.
Mtanzania
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment